Wiki ngumu sana hii kwa timu ya taifa ya Tanzania katika kutafuta nafasi ya kucheza fainali ya mataifa ya Afrika ambapo hatua ya sasa ni kuisaka nafasi hiyo.
Ugumu wa Stars unakuja katika mechi inayokuja mbele yao dhidi ya Tunisia wiki hii Novemba 13 uwanja wa Mkapa.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta hatokuwepo katika michezo yote miwili kutokana na kuumia wakati akiitumikia timu yake ya klabu Fenerbahçe ya uturuki.
Mbwana Samatta ambaye ni mshambuliaji jina lake lipo kwenye orodha ya wachezaji 27 walioitwa kuunda kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kwa sasa Stars chini ya Kocha Mkuu, Ettiene Ndayiragije imeweka kambi nchini Uturuki ambapo nyota huyo anacheza nchini humo.
Habari zinaeleza kuwa Samatta hayupo kwenye mazoezi na timu ya Taifa ya Tanzania kwa kuwa ana matatizo ya kiafya na ameshauriwa na madaktari kutocheza ili arejee kwenye ubora wake.
Ugumu wa Stars kuipasua ngome ya Tunisia kwa mechi mbili huku inahitaji angalau alama nne iweze kuwa na matumaini ya kusonga mbele.
Tanzania ilionja raha ya kucheza michuano ya mataifa ya Afrika baada ya kuikosa kwa miaka 39, Tanzania ilipata nafasi ya kushiriki tena miaka miwili iliyopita.
Maswali ya kujiuliza ni kweli itapata nafasi tena na kuwapa raha Wabongo kuishangilia timu hiyo kimataifa.
Wachezaji wengi wanacheza ligi ya ndani japokuwa na baadhi yao wanacheza timu za nje ya taifa hilo.
Baadhi ya nyota wanaocheza nje ya nchi hiyo ni Lamti Marc kijana mdogo kabisa yeye anacheza ligi kuu nchini Ujerumani katika timu ya Bayer 04 Leverkusen nafasi ya beki wa kati.
Skhiri Ellyes kiungo mkabaji ‘Defensive Midfielder’ anacheza timu ya FC Köln ya nchini Ujerumani.
Wengine ni Dudziak Jeremy (Hamburger SV), El Mizouni Idris (Cambridge United, England), Rafia, Hamza (Juventus U23 Torino) Azouni Larry (KV Kortrijk) pamoja na nyota wengine.
Kikosi chao kimesheheni wachezaji nyota lakini ligi yao pia iko katika ushindani wa hali ya juu sana.
Kocha wa Tanzania Etiene Ndayiragije anatakiwa kufanya kazi ya ziada kuwapa elimu ya ndani ya uwanja na nje ya uwanja ili waweze kuwa makini pande zote.
Kama walizoea waamuzi wa ndani kuwa na aina fulani ya uchezeshaji basi wabadilike wafahamu kuwa wanaenda kulipigania taifa.
Mashabiki wa Tanzania hamu yao kubwa kuiona timu yao ikikwea pipa tena kwenda kushiriki michuano ya kimataifa huenda ikaleta hamasa nyingine.
Ile furaha ambayo ilipatikana wakati wa kufudhu inatakiwa ipatikane tena mwaka huu, isiwe kama ilivyokuwa wakati ule msubiri hadi washidani wenu wafungwe ndio mshangilie.
Safari ya soka la Tanzania bado ndefu sana inatakiwa weledi utumike badala ya mabavu ili mambo yaende sawa.
Kwa upande wa mashabiki wanatakiwa wabadilke wajue mpira sio matokeo mazuri pekee bali hata kufungwa nayo matokeo.
Baadhi ya nyota walioitwa Tanzania ni pamoja na Juma Kaseja, Metacha Mnata, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Simon Msuva na Farid Mussa.
Stars ilikubali kichapo cha goli 1-0 kutoka kwa timu ya taifa ya Burundi katika mchezo wa kirafiki ambapo baada ya ushindi huo mataifa jirani ikiwepo Kenye walishangilia kama wameshinda wao.
Mastaa wa Tanzania wanaocheza nje ni pamoja na Simon Msuva, Himid Mao, Kibabage, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta ambaye hatokuwepo.