*Man City wafuzu kucheza Ulaya
Matumaini ya Wigan Athletic kufanya maajabu yake mwishoni mwa msimu kama miaka iliyopita yanaelekea kuota mbawa, baada ya kufungwa 3-2 na Swansea na kubaki hatarini kushuka daraja.
Wakicheza nyumbani – DW Stadium Jumanne hii, Wigan walianza vyema kwa kufungua kitabu cha mabao sekunde chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza, lakini Swansea walirejea kwa kishindo na kusawazisha.
Kocha wa Wigan, Roberto Martinez na mmiliki wa klabu, Dave Whelan walionekana kujawa furaha vijana wao walipoongeza bao la pili dakika chache baadaye, lakini hali ya hewa ilianza kubadilika Swansea wanaofundishwa na Michael Laudrup waliposawazisha.
Makunyanzi yaliwarejea nyusoni Wigan pale Swansea wanaoshika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi walipofunga bao la tatu, na nusura wapate la nne, huku tatizo la Wigan likionekana kutojiamini katika ngome na kiungo, pamoja na pasi kutokuwa za uhakika.
Golikipa wa Swansea, Michel Vorm aliondoshwa uwanjani kwa machela baada ya kugongana na beki wake, ambapo mechi iliongeza dakika tisa, na kukaribia kuchezwa kwa dakika 100, kwani ilibidi kwanza atibiwe uwanjani kabla ya kubebwa kupelekwa kwenye matibabu zaidi.
Matokeo ya leo yanawaacha Wigan wakiwa na pointi zao 35 baada ya mechi 36, zikiwa ni pointi tatu pungufu ya washindani wao wa karibu wenye pointi 38 na tofauti ya uwiano wa mabao, ambao kuanzia chini kwenda juu ni Newcastle United, Norwich City na Sunderland.
Iwapo Wigan wangeshinda leo, wangeweza kuwavuka Newcastle, kutegemeana na idadi ya mabao ambayo wangepata, maana kwa sasa wanafungana kwa uwiano wa mabao (-23) na Newcastle, wakiwa chini kwa bao moja dhidi ya Norwich, lakini Sunderland wapo vizuri kwenye eneo hilo, kwani wana -12.
Kwa mechi mbili zilizobaki dhidi ya Arsenal wanaowania nafasi nne za juu na dhidi ya Aston Villa wanaopambana kuepuka kushuka daraja, ni wazi Martinez atalazimika kutafuta mbinu za medani, ikizingatiwa kwamba wikiendi hii wana mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City uwanjani Wembley.
Katika mechi nyingine Jumatano hii, Manchester City walipata ushindi mwembamba dhidi ya West Bromwich Albion, baada ya kupata bao moja, hivyo kufikisha pointi 75, wakipunguza pengo lao dhidi ya Manchester United hadi pointi 10 na kujihakikishia nafasi moja kati ya tatu za juu.
Timu moja tu ndiyo inayotafutwa kushuka daraja, kwani Reading na Queen Park Rangers (QPR) zilishajikatia tiketi mapema, huku United wakiwapokonya City ubingwa, na nafasi mbili za uwakilishi wa Ulaya zinawaniwa na Chelsea, Arsenal, Tottenham Hotspurs na Everton kwa mbali.