Klabu ya West Ham inayoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL) imeingia
katika wakati mgumu, kutokana na mkuu wake wa masuala ya usajili, Tony
Henry kutoa kauli ya kibaguzi, akisema hawataki wachezaji Waafrika
tena.
Wakati awali kauli hiyo ilivuja kupitia barua pepe aliyokuwa
akiwaandikia mawakala wakati wa Dirisha la Usajili la Januari, alikuja
kukiri kwamba wachezaji Waafrika huwa na matatizo hasa wasipopangwa
mechi, na mwisho wake huwa ghasia.
Alipoulizwa ikiwa huo ni msimamo wa klabu alisema ndio, na kwamba
alikuwa anapendekeza sera kama hiyo, lakini baada ya mambo kuonekana
mazito, uongozi wa klabu umemruka na kuchukua hatua ya kumsimamisha
kazi kupisha uchunguzi.
Henry alizungumza kwa kujiamini, ambapo alisema imekuwa kawaida kwa
wachezaji Waafrika kukaa kivikundi, jambo analosema baadaye huweza
kuwa ghasia, lakini akasisitiza kwamba hakuwa akiwabagua japokuwa
ameshuhudiwa wakiwa na mwelekeo huo klabuni hapo, hivyo akawaambia
mawakala kuwa hawahitaji Waafrika tena.
Lakini klabu imekuja kumbadilikia, ikatoa kauli rasmi kali dhidi yake,
ikisema: “West Ham hatutavumilia aina yoyote ile ya ubaguzi, kwa hiyo,
tumechukua hatua haraka kutokana na ukubwa wa tuhuma hizi.”
Pamoja na hatua hiyo, bado West Ham wapo katika hali ngumu na
wamepakwa picha mbaya na Henry, kwa sababu hata barua yake hiyo kwa
mawakala ilinakiliwa kwa kiongozi mwandamizi wa klabu hiyo, lakini
walioibua sakata ni wanahabari walionasa barua pepe hiyo.
Wachezaji waandamizi walipokea suala hilo kwa mshangao na hali ya
kuchanganyikiwa, klabu ikiingia kwenye siku ya mwisho ya dirisha la
usajili katika hali haribifu mno kwao, ambapo walimkosa Islam Slimani
kutoka Leicester, kutokana na maneno machafu yaliyotolewa na Makamu
Mwenyekiti wa West Ham, Karren Brady dhidi ya uongozi wa Leicester.
Ripoti iliyotolewa na gazeti la Daily Mail inamnukuu Henry akimwambia
wakala hawataki Waafrika tena, kisha akaliambia gazeti hilo “ni kwa
sababu wana mtazamo mbaya …wanasababisha ghasia na mtafaruku.”
Henry ni mshirika mkubwa sana wa Kocha wa West Ham, David Moyes na
alitumia muda wa mwisho wa Dirisha la Usajili la Januari kujaribu,
pasipo mafanikio, kupata saini ya Leander Dendoncker wa Anderlecht.
Moyes alikuwa ameanza kuwanasua timu kutoka mfululizo wa kushindwa,
lakini sasa doa kubwa limeingia linaloweza kuwa gumu kufuta.
Tayari Mwenyekiti wa Kick It Out – Mpango Dhidi ya Ubaguzi, amesema
kwamba kauli pamoja na barua pepe ya Henry vilikuwa si tu kwamba ni
kinyume na haki, bali ni kinyume cha sheria.
Alipobanwa, Henry alikana kuwa sera ya namna hiyo ni ya kibaguzi,
akisema walikuwa wakikwepa watu wa aina aliyowataja na kuongeza kwamba
menejimenti ya klabu ilikuwa inaunga mkono hilo, jambo ambalo
limekanushwa na uongozi wa juu wa West Ham.
Mambo yanaweza kuwa magumu bado, kwa sababu ikiwa ni kweli na uongozi
umeamua kumkana Henry, anaweza kuwageuka kwa kutoa ushahidi ikiwa anao
ili wakose wote mithili ya suala la mmoja akimwaga mboga mwingine
anamwaga ugali.
Tuhuma dhidi ya Henry zilikuwa moja ya mada moto kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo vya West Ham Alhamisi hii, ambapo klabu ina
wachezaji saba wenye asili ya Afrika au kutoka Afrika na sasa hakuna
raha kwenye kikosi hicho.
Mchezaji mmoja ameeleza masikitiko yake kwamba maoni kama hayo
yangeweza kuja kutolewa mwaka 2018 wakati mchezaji mwandamizi hapo
kutoka Senegal, Cheikhou Kouyaté, alieleza hisia zake kwa selfie
katika Instagram na kuweka maelezo ya picha: African and prou”, maana
yake kwamba anajivunia Uafrika wake.
Viongozi walio karibu na Henry klabuni hapo wameendelea kushikilia
kwamba Henry si mbahuzio na alijaribu kurekebisha mambo kwa na walio
kwenye kikosi hicho lakini akagonga mwamba. West Ham imeuza wachezaji
wake nwawili Waafrika.
Mmoja aliyeondoka ni Diafra Sakho aliyetundika picha na maelezo
mtandaoni akisema kwamba Waafrika wameanza kuondoka mmoja mmoja kwa
sababu hawapendwi. Aliuzwa Rennes, Ufaransa wakati wakimruhusu André
Ayew kurudi Swansea kwa pauni milioni 18 baada ya raia huyo wa Ghana
kuomba kuondoka.
Wachezaji wote hao hawajacheza tangu Desemba, klabu wakisema walikuwa
wanaumwa – Sakho goti na Ayew nyama za paja lakini wote wamefuzu
vipimo vya afya huko walikokwenda. Inasubiriwa kuona hatua zaidi
zitakazochukuliwa kwenye sakata hili lililonyanyua kope za macho ya
wengi.