‘North London Derby’
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amewataka wachezaji wake wawafundishe soka mahasimu wao wa London Kaskazini – Tottenham Hotspur na kuwaonesha hasa ni nani mtawala hapo.
Akizungumza kuelekea ‘North London Derby’, Wenger (67) amesema lazima vijana wake waoneshe nani mwenye mamlaka jijini hapo, ambapo Spurs walimaliza ligi juu ya Arsenal kwa mara ya kwanza msimu uliopita tangu Mfaransa huyo aingie Arsenal 1996.
Spurs wamekuwa wakali siku za karibuni chini ya kocha Mauricio Pochettino aliyekuwa akitajwa tajwa kwenda Barcelona, ambapo mbali ya kumaliza katika nafasi ya pili msimu uliomalizika, wamefanya vyema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) hadi sasa, wakiwapiga mabingwa watetezi, Real Madrid mabao 3-1 jijini London baada ya kwenda nao sare ya 1-1 jijini Madrid.
Wenger, lakini, hataki kuamini kwamba wapinzani wao hao wamewazidi kabisa, hivyo anataka Arsenal wacheze kwa nguvu na akili ili wapate ushindi dhidi ya Spurs na kuwarejeshea heshima klabu na sifa washabiki wao waliokasirishwa sana msimu uliopita kwa Spurs kuwavuka.
Arsenal walimaliza katika nafasi ya tano na kukosa fursa ya kushiriki UCL kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo miwili, lakini Spurs hawajapata kutwaa tuzo yoyote kubwa. Wakati Spurs wakiwa kwenye UCL, Arsenal wamo kwenye mashindano madogo – Europa League. Spurs wapo juu yao kwenye msimamo wa ligi kuu pia.
Wenger anasema kwamba wachezaji walichukizwa, si kwa sababu ya kumaliza ligi chini ya mahasimu wao hao, bali kumaliza nje ya nne bora. Anasema ni ajabu kwamba mtu ana pointi 75 lakini bado hayumo kwenye nne bora. Waliomaliza humo juu pamoja na Spurs ni Liverpool, Manchester City na Chelsea waliotwaa ubingwa. Manchester United walimaliza wa sita lakini wakapenya UCL kwa sababu walitwaa ubingwa wa Ligi ya Europa.
“Ilikuwa mbaya sana kwetu lakini watu wanasahau kwamba tumetwaa ubingwa wa Kombe la FA tena kwa staili ya aina yake, tukicheza dhidi ya Manchester City kwenye nusu fainali na dhidi ya Chelsea kwenye fainali yenyewe na kwa hakika tulimaliza msimu tukiwa na nguvu sana.
“Uwiano wa mamlaka (baina ya Arsenal na Spurs) ni suala unalotakiwa kujibu na njia pekee ya kufanya hivyo ni kule uwanjani. Hitimisho la watu litatokana na utendaji wa Jumamosi hii, tunayo fursa nzuri ya kuonesha kwamba sie tupo imara zaidi na hebu sasa tuoneshe hivyo,” anasema Wenger.
Mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Lee Dixon, anawachagiza Arsenal akidai kwamba timu yao ni laini. Wenger hakubaliani naye, lakini anasema ni aina ya maneno yanayotolewa licha ya mazuri yote waliyofanya kwa miaka 20.
“Nakumbuka watu wengi waliniuliza mwaka 2002 na 2003 ikiwa (Robert) Pires angekuwa na nguvu na ushupavu wa kutosha kucheza ‘North London Derby’. Hawa ni aina ya watu waliofunga mabao kuliko wengine kwenye derby. Hatimaye kinachoamua ni kiwango cha mchezo.
“Lazima tukubali juu ya kipi ni nguvu na kipi sio. Mwanasoka anatakiwa kuwa na ufanisi na hicho ndicho muhimu zaidi. Ufanisi ukiwa mlinzi si kufanya kosa lolote ili uupate mpira. Ikiwa wewe ni mshambuliaji, kinachotakiwa ni kutia mpira kimiani. Je, hiyo inatosha? Haijalishi sana – inategemeana na jinsi ulivyo na ufanisi mchezoni,” anasema Wenger.
Suala lenyewe, hata hivyo, ni kwamba kwa ujumla Spurs wamekuwa wakionekana siku hizi kuwa na ufanisi zaidi mchezoni wakilinganishwa na Arsenal na kwa hakika wanahesabiwa kuwa washindani wa kweli wa ubingwa msimu huu. Nyongeza ya miaka miwili kwenye mkataba wa ukocha wa Wenger ulizingatia kwamba ndiye bora zaidi wa kuweza kuwapeleka kwenye heshima kubwa nyumbani na ng’ambo.
mail to: saria@tanzaniasports.com