Wakati Pep Guardiola na Manchester City wakiweka rekodi za maana na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu, Arsene Wenger na Arsenal pia wanaweka rekodi zao. Tofauti iliyopo ni kwamba Manchester City wanaweka rekodi nzuri na za fahari wakati hawa wengine wakiandika rekodi mbaya za kufedhehesha kupita kiasi.
Baada ya kipigo cha 1-0 walichopata Manchester United kutoka kwa West Bromwich Jumapili, City walitwaa rasmi ubingwa wa EPL wakiwa na michezo mitano mkononi iliyosalia. Wamejiunga na Manchester United ya 2000/01 na kufanya timu mbili pekee zilizotwaa ubingwa wa EPL mapema zaidi kwenye historia ya michuano hiyo.
Arsenal nao waliandika rekodi yao kufuatia kupoteza ugenini kwa 2-1 dhidi ya Newcastle United. Washika Bunduki hao wa London ni timu pekee kwenye Ligi nne za juu za nchini England ambayo haijavuna alama hata moja ugenini kwa mwaka huu 2018. Hata Bury ambao ndiyo timu ya kwanza kushuka daraja kwenye ligi nne za juu wamevuna alama nne mwaka huu kwenye viwanja vya ugenini.
Mchezo wa ugenini unaofuata utawapeleka Washika Bunduki hawa Old Trafford. Tunatarajia nini hapa? Chochote wanachoweza kufanya Newcastle United, basi Manchester United wanaweza kukifanya vyema zaidi. Mbaya zaidi mchezo huo utachezwa katikati ya michezo miwili migumu ya nusu fainali ya Europa League dhidi ya Atletico Madrid.
Arsenal wako nyuma ya mabingwa Manchester City kwa alama 33. Pia nyuma ya Tottenham Hotspur walio kwenye nafasi ya nne kwa alama 13. Na ni alama 2 tu zinazowatenganisha vijana hao wa Wenger na Burnley walio kwenye nafasi ya saba. Pengine mabaya zaidi yako njiani kwa kuwa Wenger atahitaji kuipuuza EPL ili kuelekeza nguvu kwenye Europa League.
Tukirudi nyuma kwa takribani misimu 15, Arsenal ndio waliokuwa wakitengeneza rekodi za kutukuta chini ya Arsene Wenger kama wafanyavyo sasa Manchester City. Walionesha mtindo safi wa soka na kuwa timu tishio. Sifa nyingi zilienda kwa Wenger na alistahili sifa hizo zaidi ya Thiery Henry ama Patrick Vieira. Sasa mambo yanakwenda kombo. Nani alaumiwe na kuwajibishwa?
Inaonekana Wenger bado ni mwalimu wa Arsenal kwa sababu aliitengeneza Arsenal tishio iliyoshinda taji la Ligi Kuu ya England bila kupoteza mchezo wowote kwenye msimu wa 2003/04. Kuna watu ndani ya Arsenal wanadhani kwamba Mfaransa huyo anaweza kuirejesha Arsenal kuwa timu tishio kama ilivyokuwa awali. Watu hawa akiwemo Wenger mwenyewe wanajidanganya.
Ikiwa Mfaransa huyo atashinda taji la Ligi ya Europa atajiongezea kuungwa mkono zaidi na wanaomuunga mkono sasa ndani ya bodi ya Arsenal. Yeye mwenyewe pia anaweza kudhani hayo ni mafanikio makubwa yanayotosha kufanya apewe mkataba wa miaka 10 zaidi. Kiuhalisia hata kama watashinda taji hilo, Wenger aende mwishoni mwa msimu huu ukiwa umesalia mwaka mmoja kwenye mkataba wake.
Bado hakuna uhakika wa kuondoka kwa Wenger mbaka sasa. Huu ni utani kwa klabu yenye historia kubwa na inayostahili kuwa na malengo makubwa mno. Arsenal wanapaswa kujifunza jambo kutoka kwa Chelsea ambao wana mataji matano ya Ligi Kuu ya England na moja la Ligi ya Mabingwa tangu taji la mwisho la Arsenal la Ligi Kuu ya England.
Kama watashinda taji la Ligi ya Europa na kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao, hilo linaweza kutosha kumuokoa Arsene Wenger. Lakini kwa upande mwingine huo utakuwa wakati sahihi zaidi wa kuiacha timu kwa mtu mwingine kuanza kutengeneza kikosi kitakachoweza kutoa upinzani wa kweli kwenye Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa.
Kikosi cha sasa cha Arsenal kimesheheni nyota waliojaa vipaji. Lakini wanahitaji changamoto mpya chini ya mwalimu mpya atakayeweza kuamsha ari za wachezaji hao. Mtazame Oxlaide-Chamberlain aliye chini ya Jurgen Klopp kwa sasa. Ozil na wenzie pia wanahitaji kuwa chini ya mwalimu mpya ili wapate matumaini ya kweli na hatimaye kuonesha viwango walivyo navyo. Wenger ni lazima aende, ili Arsenal wawe washindani wa kweli.