Menu
in , , ,

Wenger kuongeza mkataba Arsenal


*David Moyes aanza kwa kichapo Man U
*Alcantara amkimbia na kwenda Bayern

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ameanza mazungumzo na klabu hiyo, na anatarajiwa kuongezwa mkataba wa muda mrefu Emirates.
Mfaransa huyo aliyewafundisha Washika Bunduki wa London kwa miaka 17, ametangaza hadharani kwamba yupo tayari kubaki Emirates kwa miaka mingi ijayo.
Amekuwa akihusishwa na kuhamia Paris Saint-Germain majira haya ya kiangazi au mkataba wake wa sasa utakapomalizika mwakani.
Ameanza mazungumzo ya hatima yake na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Arsenal, Ivan Gazidis.
“Mie ni mtu niliye tayari kukaa klabuni hapa kwa muda mrefu na tayari nimeanza mazungumzo na Ivan ambayo yanakwenda vizuri sana, hakuna tatizo,” Wenger amewaambia waandishi wa habari.
Kadhalika, kocha huyo anayeongoza England kwa kukaa katika klabu moja kwa muda mrefu zaidi kwa sasa, amesema nyota waliohusishwa na klabu hiyo si mzaha.
Kwamba wapo tayari kuendeleza mazungumzo na kuwasajili Gozalo Higuain wa Real Madrid, Wayne Rooney wa Manchester United na Luis Suarez wa Liverpool kwa sababu nia, sababu na uwezo wanao.
Wenger (63) amesema klabu sasa inalenga kutumia fedha zaidi kuimarisha kikosi chao msimu huu wa kiangazi wa usajili, lakini akasema anahisi si wachezaji wote wanaowataka watapatikana wakati huu.
Wenger na Arsenal wapo Asia kwa ajili ya ziara za utangulizi wa Ligi Kuu ya England (EPL) 2014, akitamba kwamba wapo vizuri kiuchumi sasa na hiyo ni muhimu kwao.

MOYES APOTEZA MECHI YA KWANZA

Kocha David Moyes ameanza kibarua Manchester United kwa kufungwa bao 1-0 nchini Thailand na kikosi cha Singha All Stars.
Moyes aliyerithi mikoba ya Alex Ferguson, alikuwa akitabiriwa kuanza na wakati mgumu klabuni hapo, na amekiri wangependa kushinda mechi hiyo ili kuweka mtiririko mzuri wa ushindi.
Hata hivyo, Mskochi huyo amesema haikuwa mechi waliyokamia wala kuhitaji sana kushinda, ambapo mchezaji Teeratep Winothai alifunga bao pekee katika dakika ya 50 kwenye Uwanja wa Taifa wa Rajamangala jijini Bangkok.

Hata hivyo, katika kikosi cha United, hawakuwapo nyota Robin van Persie, Nani, David de Gea, Javier Hernandez, Nemanja Vidic wala Wayne Rooney, hivyo anaweza asiwe na wasiwasi.
Badala yao, aliwatumia Adnan Januzaj na Wilfried Zaha aliyekosa bao la wazi la kusawazisha, baada ya kiki yake kugonga mwamba.
Fergie pia alipoteza mechi yake ya kwanza hapo, hivyo Moyes anaona kana kwamba anafuata nyayo na hatimaye wataimarika na kuanza kupata ushindi, kwani Fergie alipoteza 0-2 dimbani kwa Oxford United Novemba 1986.

THIAGO ALCANTARA AENDA BAYERN

Mbio za Moyes na United kumsajili nyota Thiago Alcantara wa Barcelona zimegonga mwamba, baada ya Pep Guardiola wa Bayern Munich kuwazidi dau.
Guardiola aliyekuwa Barca zaidi ya mwaka mmoja uliopita, ameonesha kuwa na ushawishi kwa mchezaji huyo, aliyekubali kuhamia Ujerumani kwa ada ya uhamisho inayofikia pauni milioni 21.6.
Kiungo huyo Mhispania mwenye umri wa miaka 22, anaungana na kocha wake wa zamani katika klabu ambayo ni mabingwa wa Ulaya, ambapo Mwenyekiti wao, Karl-Heinz Rummenigge amekiri Alcantara alikuwa chaguo la Guardiola.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version