Mimi nasema: washapita..
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amewapa Barcelona asilimia 95 ya
kufuzu kwa hatua ya robo fainali, baada ya ushindi wao wa 2-0.
Mabingwa hao wa Hispania walipata ushindi huo katika uwanja wa
nyumbani wa Arsenal – Emirates, mabao yakifungwa na Lionell Messi,
moja kwa penati katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Wenger aliwalaumu wachezaji wake kwa kushindwa kumalizia vyema upande
wa ushambuliaji na pia kuzubaa uwanjani katika hatua hiyo ya 16 bora.
Alex Oxlade-Chamberlain na Olivier Giroud walikosa nafasi za kuwapa
Arsenal mabao kabla ya kuadhibiwa na Messi.
“Kuna tatizo katika jinsi tunavyomalizia mipira kwenye fursa
tunazopata; kuna kitu tunakosa pale mbele. Barcelona wameshapita kwa
asilimia 95 lakini tunataka kwenda (Camp Nou) na kucheza. Hatuendi
tukichukulia kwamba tumetoka, tutapambana,” akasema Mfaransa huyo.
Messi amemfunga kipa wa Arsenal, Petr Cech kwa mara ya kwanza, kwani
akiwa Chelsea hakufaulu kufanya hivyo.
Arsenal walipambana ili kujipa matumaini na fursa ya kwenda Barca kwa
marudiano wiki tatu zijazo wakiwa na ahueni, lakini sasa itabidi
kwanza wafunge mabao matatu zaidi ya Barca ili wavuke.
Arsenal walionekana dhaifu kwa Barcelona, japokuwa walifanikiwa
kuwadhibiti hadi dakika ya 71 Messi alipofunga.
Nyota watatu wa Barca; Messi, Neymar na Luis Suarez walionekana
kuwatesa Arsenal na kuwaathiri kisaikolojia kwenye mechi hiyo. Messi
alifunga bao la kwanza baada ya shambulizi la kushitukiza, na la
penati lilitokana na kuangushwa na Mathieu Flamini.
Messi sasa ameshawafunga Arsenal mabao manane. Katika mechi hiyo,
Suarez aligonga mwamba wakati Cech alifanikiwa kuokoa mpira hatari wa
Neymar.
Wakitolewa katika hatua hii, itakuwa ni mara ya sita mfululizo. Wenger
amefananisha kipigo hicho na kile cha 3-1 kutoka kwa Monaco msimu
uliopita hatua kama hii hii.
“Nasikitika kwamba kuna wakati tulionekana kwamba tunatawala mchezo,
lakini tukaachia na kuwapa bao, kama ilivyokuwa kwa Monaco msimu
uliopita. Utoto, na hili linachanganya,” akasema Wenger.
Katika mechi nyingine ya UCL, Juventus wakiwa nyumbani walilazimishwa
sare ya 2-2 na Bayern Munich.