Menu
in , , ,

Wenger atamlipua Mourinho?

*Wenger atamaliza ubishi wa Mourinho?

Mawazo ya wadau wengi wa soka yanaelekezwa kwenye mechi kubwa ya Jumapili hii baina ya Arsenal na Chelsea katika Ligi Kuu ya England.

Licha ya kwamba zipo mechi nyingine Jumamosi, wengi wanaangalia ya Jumapili kwa sababu inakutanisha mahasimu wawili – Arsene Wenger na Jose Mourinho.

 

Timu hizi zinakutana zikiwa na hali tofauti. Chelsea wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 10 wakifuatiwa na Arsenal.

 

Hata hivyo Arsenal wanaingia wakiwa na wachezaji walio katika utimamu wa mwili na kiwango cha juu.

 

Wameshinda mfululizo wa mechi nane zilizopita za Ligi Kuu, mserereko mzuri zaidi tangu enzi za Invicibles 2004 waliposhinda mechi tisa mfululizo.

 

Kadhalika Wenger anaingia akijiamini kwamba ataweza kumfunga mdomo Mourinho katika jaribio lake la 13, ambapo hajapata kufanikiwa kumshinda hata mara moja.

 

Wenger mwenyewe na wachezaji wake kadhalika wanajiamini, wako kwenye kiwango kizuri, amewapa mtindo mzuri wa kucheza lakini zaidi sana kwenye ulinzi wako vizuri, mambo yanayoweza kuwapa faida dhidi ya Chelsea.

 

Hata hivyo, ili kushinda lazima Arsenal wafanye kazi ya ziada kwa sababu Mourinho ni mjanja na huwa anakwepa kufungwa kwenye mechi kubwa kama hii.

 

Mahasimu hawa wawili walikutana kwa mara ya kwanza Desemba 2004 katika Uwanja wa Highbury na kwenda sare ya 2-2.

 

Tangu Mourinho atue Chelsea awamu ile ya kwanza amecheza mechi 39 za ligi dhidi ya mahasimu wake wakubwa, The Gunners, Liverpool, Manchester United na Manchester City – na kati ya hizo amepoteza tat utu.

 

Ni juzi tu The Blues wametoka kuwafunga Man United 1-0. Matokeo ya ‘The Special One’ dhidi ya Arsenal yamekuwa ya kumpendeaz zaidi, kwani katika mechi 12 kwenye mashindano yote Arsenal hawajapata kumshinda.

 

Hata hivyo, aina ya soka The Gunners waliyokuwa wakicheza wakati huo ilikuwa nzuri kwa Mourinho kumudu kwani Arsenal walikuwa wakishambulia na kujisahau nyuma, hivyo yeye akatumia mwanya huo kuwaadhibu.

 

Inadhaniwa kwamba Mourinho hatabadili mtazamo wikiendi hii, hivyo suala litakaloamua mshindi ni jinsi Wenger atakavyowapanga vijana wake kuweza kushambulia na kujilinda vyema.

 

Mechi ya Jumapili bila shaka itakuwa karibu sawa na ya Chelsea dhidi ya Man United, angalau kwa mwelekeo wa uchezaji. Arsenal watapenda kumiliki zaidi mpira na kushambulia wakati Chelsea watakuwa wakijihami kama ilivyokuwa kwa United.

 

Tatizo ni kwamba Mashetani Wekundu walishindwa kuwamudu Chelsea kwa kuvunja ukuta wao, hivyo wakaishia kufumua mashuti marefu.

Chelsea walikuwa na watu 10 nyuma ya mpira kwenye hiyo mechi, lakini kwa Arsenal mambo yanaweza kuwa tofauti, kutokana na aina ya wachezaji wa mbele walio nao.

 

Wakishafungua vyumba na kumiliki mpira kati ya viungo na mabeki wa Chelsea, Arsenal wataendelea kupeana pasi hadi wawahadae Chelsea badala ya kupiga mashuti ya mbali kama United.

 

Siku hizi Arsenal wana utulivu, kujituma na humiliki sana mpira na wengine wanadai kwamba hutoa pasi hadi nyavuni. Uvumilivu wa jinsi hiyo unawafaa dhidi ya Chelsea kwa sababu watawachosha.

Sanchez

 

Kama ilivyokuwa dimbani Emirates msimu uliopita, Mourinho atajaribu kujaza watu kwenye kiungo lakini Arsenal ni wakali zaidi siku hizi wanaposonga mbele na kwa matokeo ya karibuni lazima watakuwa na kujiamini zaidi, hata dhidi ya ngome imara kama ya Chelsea.

 

Arsenal wamefika fainali ya Kombe la FA na wanaingia kwenye mechi hii wakiwa timu yenye rekodi nzuri zaidi kwa timu za madaraja ya juu Ulaya, kwa kukusanya wakiwa na uwiano mwingi zaidi wa pointi kwa mechi kwa England, Hispania, Ujerumani, Ufaransa na Italia.

 

Wameshajifunza na kumaizi jinsi ya kuwashinda wapinzani wao wakubwa pia, maana zamani walikuwa wakipata shida kuwafunga Manchester City, Liverpool na Chelsea.

 

Januari walikwenda Etihad na kuwapiga City, wakawafyatua Liverpool nyumbani kwao mapema mwezi huu na pia waliwapiga Man United na kuwatupa nje ya Kombe la FA.

 

Wakiwafunga Chelsea Jumapili hii na tena dhidi ya Man U Mei 17 itamaanisha wanakuwa vyema na hata wasipofanya hivyo, bado kuna maendeleo makubwa sana wamefanya msimu huu.

 

Kama alivyosema Wenger, suala si historia bali hali za timu na kujituma kwa wahusika katika mchezo. Wakiwa na Francis Coquelin kwenye timu yenye nidhamu kubwa kwenye kiungo watamudu kuwadhibiti Chelsea kwenye mashambulizi ya kushitukiza, maana hawatasukuma wachezaji wengi mno mbele.

 

Chelsea hujipanga vizuri sana nyuma lakini hutulia kusubiri fursa ya kumwingilia adui kama alivyofanya Eden Hazard alipowapatia The Blues ushindi dhidi ya United.

 

Kwa muda mrefu Arsenal wamekuwa wakimaliza ligi kwa nguvu na washabiki kujisemea; ‘mwaka ujao ni wetu’, lakini wakianza huwa hovyo. Safari hii, hata hivyo, mambo ni tofauti.

 

Ningekuwa Wenger ningemsajili kiungo wa Southampton, Morgan Schneiderlin ili acheze sambamba na Coquelin na kununua beki mmoja mahiri wa kati pia.

 

Ushindi kwa Arsenal Jumapili litakuwa dili kubwa kwa Wenger wala si tu kwa sababu ya uhasimu binafsi wa muda mrefu dhidi ya Mourinho

Yawezekana ushindi wa Arsenal, ukipatikana, hautaathiri mbio za Chelsea kutwaa ubingwa, maana kuna kila dalili Chelsea watauchukua bila kujali matokeo ya mechi hii.

 

Hata hivyo, ushindi utakuwa salamu tosha kwa mahasimu na utawaweka Washika Bunduki wa London pazuri kwa kuuendea ubingwa siku zijazo. Ushindi, bila kujali jinsi wanavyoupata dhidi ya mabingwa wateule utaonesha kwamba wanamaanisha mambo mazuri kwa msimu ujao.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version