Menu
in , ,

Wenger anabaki Arsenal

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger anatarajiwa kubaki klabuni hapo kwa walau miaka miwili zaidi, baada ya kufanya mazungumzo na mmiliki, Stan Kroenke.

Taarifa zinadai kwamba Wenger ambaye hadi sasa amekuwa kimya juu ya iwapo ataendelea kuwafundisha Washika Bunduki wa London msimu ujao au la, amekuwa na mazungumzo ya muda mrefu na Mmarekani huyo ambaye hataki kusikia habari za kuondoka kwake.

Gazeti la The Mirror linaeleza kwamba pamoja na Kroenke anayemiliki zaidi ya asilimia 70 ya hisa za klabu hiyo, walikuwapo pia vigogo wengine wa Arsenal kwenye mazungumzo ya karibuni kabisa.

Baadhi ya washabiki wa Arsenal wamekuwa wakipiga kelele kutaka kocha huyo aliyedumu kwa miaka 20 sasa asipewe mkataba mpya, pale alio nao sasa utakapoisha kiangazi hiki. Hata hivyo, kumekuwapo ushauri kutoka ndani na nje ya Arsenal dhidi ya kumwacha aondoke.

Haondoki, angalau kwa sasa…

Baadhi ya walioeleza umuhimu wa Wenger kubaki ni wachezaji wa zamani wa Arsenal, Jens Lehman na Robert Pires pamoja na beki wa kati wa zamani wa Manchester United ambaye ni mchambuzi wa soka, Rio Ferdinand.

Wakuu wa Arsenal wanaelezwa kwamba kitambo sasa walishaweka mezani mkataba mpya lakini Wenger amekuwa akisita kuusaini, akitaka kwanza amalize kazi ya msimu huu au afanye hivyo Aprili hii. Inaelezwa kwamba ametakiwa na wakuu awajulishe uamuzi kabla ya mwisho wa mwezi huu ili waweze kujiandaa iwapo anaondoka.

Katika kuashiria kutoondoka kwake, majuzi aliwaeleza washabiki wa klabu hiyo kwamba amefanya mengi tangu afike hapo na amejitolea kwa hali na mali kuijenga klabu na kwamba hata akiondoka wasitarajie kushinda kila mchezo.

Washabiki wamekerwa na kuanguka kwa Arsenal hadi nafasi ya sita, baada ya kuchapwa na Everton, Chelsea, Watford, Liverpool na West Bromwich Albion na pia kutupwa kwa aibu nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa jumla ya mabao 10-2 kwenye mechi mbili dhidi ya Bayern Munich.

-=-

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version