Mshambuliaji mpya wa Arsenal, Danny Welbeck amesema hangeweza kuwa na furaha zaidi ya kutimiza ndoto yake ya kuchezea Arsenal.
Welbeck (23) aliyedumu Manchester United kwa miaka 15 tangu akiwa mtoto, amesema ana furaha isiyo kifani kufanikiwa kujiunga na Gunners, kwani alikuwa akiifuatilia na kutazama mechi zake za Ligi Kuu, kisha akajifikiria ingekuwaje akicheza Emirates.
Anasema kwamba anaamini sana katika mfumo wa uchezaji anaopendelea kocha Arsene Wenger na jinsi wachezaji wenyewe wanavyojituma uwanjani, hasa wale wa kiungo ambao ni wa hali ya juu, akisema ni rahisi kwake kupatiwa mipira yao na kuipachika wavuni.
“Nadhani huu ni wakati tunaoweza kuutumia kusukuma gurudumu mbele na kujaribu kutwaa hata kombe la Ligi Kuu. Suala langu lilienda hadi ukingoni mwa siku ya usajili. Ni vigumu kueleza nilivyojihisi nyakati tofauti za siku hiyo kwa sababu dili lilikuwapo, kisha likazimika lakini hatimaye mie ni mchezaji wa Arsenal na nisingeweza kuwa na furaha kubwa zaidi ya hii,” anasema Welbeck.
Anaongeza kwamba Arsenal ni klabu inayokua na kwamba katika miaka ya karibuni wamefanya vizuri ambapo mwaka jana walitwaa Kombe la FA, akisema kwamba yeye mwenyewe ana medali moja na anapenda kuongeza nyingine.
Mchezaji huyo mrefu anasema kwamba kipya atakachoingiza Arsenal ni kasi na nguvu na kwamba akiungana na wachezaji wengine, muziki utakuwa mzuri wakiwazunguka watakavyo mabeki na kucheka na nyavu.
“Nataka kufunga mabao na kusaidia timu kupanda juu zaidi kwa kushinda mechi nyingi. Hii ni hatua yangu nyingine katika maendeleo kisoka baada ya kuwa United tangu nikiwa mtoto, hakika kwa kuwaonesha watu nini ninachoweza kufanya kama mwanasoka na kufika pale nitakapo,” anasema kwa furaha Welbeck.
Alipoulizwa iwapo ilikuwa vigumu kuhama Manchester United alikokaa kwa muda mrefu zaidi wa maisha yake, Welbeck anasema kwamba maisha ni kusonga mbele na si kukaa sehemu moja.
“Kwa hakika unatakiwa kufanya uamuzi sahihi kwa hali uliyomo na kwa wakati sahihi. Naamini kabisa kwamba kuja Arsenal ni uamuzi sahihi,” anamalizia.