Wachezaji wawili kutoka Tanzania wamechaguliwa miongoni mwa 50 waliofanyiwa
majaribio nchini Uganda kwa ajili ya kuingia katika kituo cha kuendeleza
vipaji (centre of excellence) kilichoko Doha nchini Qatar kupitia mpango wa
kukuza vipaji wa Aspire Football Dream.
Abdulrasul Tahir Bitebo (15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja
wa Karume, na Martin Omela Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha
Ukonga ndiyo waliochaguliwa kutoka Tanzania kuingia katika kituo ambapo
watakaa kwa mwezi mmoja kabla ya kusaini mkataba rasmi wa kuendelezwa.
Wachezaji wengine walikuwa wakitoka katika nchi za Uganda na Kenya.
Mchezaji mwingine aliyefuzu katika nafasi tatu zilizokuwepo ni kutoka
nchini Kenya.
Mpango wa Aspire Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar
katika nchi 16 duniani, na kwa hapa nchini uko chini ya Idara ya Ufundi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
TFF ina jumla ya vituo 14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa
Aspire Football Dream. Vituo hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe,
Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Makongo, na Tabata vilivyo katika Mkoa
wa Dar es Salaam. Vingine ni Bagamoyo kilichopo mkoani Pwani, Morogoro,
Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kituo kingine cha kuendeleza vipaji (centre of excellence) cha Aspire kipo
Dakar nchini Senegal.
* *
*TFF KUENDESHA KOZI SITA KATI YA JULAI- SEPTEMBA*
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaendesha kozi sita tofauti
za mpira wa miguu kati ya Julai na Septemba mwaka huu.
* *
Kozi hizo ni FIFA 11 For Health itakayofanyika Hombolo mkoani Dodoma
kuanzia Julai 8 hadi 19 mwaka huu. Julai 6 hadi 15 mwaka huu kutakuwa na
kozi ya mpira wa miguu wa ufukweni (Beach Soccer) itakayofanyika jijini Dar
es Salaam.
Waamuzi wa FIFA nao watakuwa na kozi itakayofanyika kati ya Agosti 22 hadi
26 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati kozi ya ukocha kwa ajili ya Copa
Coca-Cola itafanyika jijini Dar es Salaam kati ya Agosti 12 na 17 mwaka huu.
* *
Vilevile kutakuwa na kozi ya* *mpango wa grassroots unaolenga wachezaji
mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12
itafanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati
tamasha (festival) la grassroots litafanyika Uwanja wa Karume, Septemba 14
mwaka huu.
*RCL KUKAMILISHA HATUA YA NNE JUMAPILI*
Mechi za marudiano za hatua ya nne ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL)
zitachezwa Jumapili (Juni 30 mwaka huu) kwenye viwanja vya Sokoine jijini
Mbeya, na Kambarage mjini Shinyanga.
Friends Rangers ya Dar es Salaam ambayo katika mechi ya kwanza ilifungwa
nyumbani mabao 3-0 itakuwa mgeni wa Stand United FC mjini Shinyanga wakati
Kimondo SC itaikaribisha Polisi Jamii ya Mara jijini Mbeya. Katika mechi ya
kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Hatua ya mwisho ya RCL itachezwa Julai 3 mwaka huu kwa mechi za kwanza
wakati zile za marudiano zitafanyika Julai 7 mwaka huu. Timu tatu za kwanza
zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.