Menu
in

Watanzania soka yao na kocha wao!

KAMA ilivyo kwa watu wa mataifa yote duniani,Watanzania wanaipenda sana nchi yao.Wanapenda kuona nchi yao hii inapata mafanikio katika nyanja mbalimbali ikiwemo michezo na hasa mchezo wa soka.Ni upendo huo wa nchi yao,ndiyo unaofanya wote waipende timu yao ya Taifa ya soka na hivyo kufurahia mafanikio yake,yaani mafanikio ya timu hiyo.Lakini kwa bahati mbaya sana, Watanzania wengi walio mashabiki wa Yanga wanaipenda Yanga kuliko hata nchi ya Tanzania yenyewe! Vile vile, mashabiki wengi wa Simba wanaipenda Simba kuliko nchi ya Tanzania yenyewe! Furaha au karaha za wengi wa Watanzania juu ya timu yao ya Taifa,mara nyingi inatokana na jambo jema au baya kwa timu hiyo linalohusiana moja kwa moja na Yanga na/au Simba.

Kocha wa Taifa Stars

Kwa bahati mbaya sana, mashabiki wa Yanga na Simba wapo kila mahali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Wamo ndani ya vilabu hivyo vya soka,wamo kwenye vilabu vyote vya soka nchini,wamo ndani ya vyama vya michezo yote nchini vinavyojumuisha Shirikisho la Soka la Tanzania,yaani Tanzania Football Federation(TFF),wamo serikalini na popote pale patakapokujia kichwani,pawe sehemu ya kijamii,ya utawala,ya kisiasa na kadhalika.Kote huko kuna “Yanga damu” na “Simba damu”.Matokeo ya kuwepo kwa hali hii ni kufanya kila jambo linalohusu soka kujadiliwa,kutathminiwa au kuamuliwa kwa kuzingatia ama kuibeba au kuiumiza Yanga au Simba,kutegemeana na mhusika katika mjadala huo,tathmini hiyo au uamuzi huo ni shabiki wa timu gani kati ya timu hizi mbili.

Kitu cha kushangaza kuhusu Watanzania ni kwamba wanazipenda Yanga na Simba tu wakati kuna timu nyingi nzuri na zinazocheza soka la hali ya juu kama Mtibwa Sugar,JKT Ruvu,Kagera Sugar,Prisons,Miembeni,KMKM,Mundu,Malindi na nyinginezo.Hawana ushabiki wa moja kwa moja wa timu hizi kama baadhi yao walivyowahi kuwa na ushabiki wa asilimia mia moja kwa Cosmopolitan,Pan African,Nyota Nyekundu na kwa miaka hii ya karibuni Ashanti United.Siku hizi,kwa mfano, mashabiki wa Yanga huwa wa Mtibwa Sugar inapocheza na Simba ambapo wa Simba nao huwa mashabiki wa timu hiyo kali ya mkoani Morogoro inapocheza na Yanga.Viongozi wote wa vilabu vyote vya soka nchini ni mashabiki au hata wanachama wa Yanga au Simba na wako tayari kuzisaliti timu zao kwa manufaa ya Yanga au Simba.Migogoro yao mingi huhusiana na hawa wanataka kuisaliti timu yao ili Yanga au Simba inufaike wakati wenzao wenye ushabiki wa timu tofauti  kati ya hizo wanapinga! Kibaya zaidi,hata wachezaji wa timu hizo nyingine wana Uyanga na Usimba ndani yao!

Kinachoshangaza,wakati hapa nyumbani Tanzania,Watanzania wanazishabikia Yanga na Simba tu licha ya kuwepo timu nzuri nyingi,kwa Ulaya wanazishabikia timu nyingi mno.Tanzania kuna mashabiki wengi wa Arsenal,Manchester United,Liverpool,Chelsea,Real Madrid,Barcelona,AC Milan,Inter Milan,Juventus,Bayern Munich na Newcastle United.Pamoja na hizo, kuna nyingine nyingi zenye mashabiki wachache wachache hapa nchini. Sasa swali la kujiuliza,inakuwaje kwa soka la kimataifa ushabiki wa Watanzania unahusisha timu nyingi lakini hapa kwetu unahusisha timu mbili tu? Hawa ndiyo Watanzania katika soka.

Soka ya Watanzania hawa ni soka iliyo zaidi ya soka ya ridhaa.Kwa sababu ingekuwa ni soka ya ridhaa,ingeanza kuwa hivyo baada ya kuandaliwa kwa kuwepo kwa shule za soka na watoto kuanza kuishi ndani ya mchezo huo tangu wakiwa wadogo,kungekuwa na wataalam wa kutosha wa kufundisha mchezo huo nchi nzima, kungekuwa na walimu bora wa kutosha wa kufundisha vilabu vyetu vya soka na kungekuwa na mashindano mengi tofauti ya makundi tofauti ya kiumri na kiviwango vya soka.Karibu hayo yote hatuna lakini hata viwanja vya watoto kucheza soka wao wenyewe kivyao hatuna! Hayo yangefanyika na soka yetu kubaki ya ridhaa,tungesema kweli soka yetu ni ya ridhaa.Kinyume chake,soka yetu inaweza kufananishwa na kuku wa kienyeji,walio maarufu sana barani Afrika, kwa maana ya kwamba,kuku hao wakishafunguliwa toka ndani asubuhi,mwenye kuku hajui wanakula nini na wapi,maji ya kunywa wanapata wapi,wanakabiliana vipi na adui zao kama vipanga,mwewe na vicheche na wanaumwa nini na kutibiwaje! Pamoja na kuwaacha waishi kivyao,mwenye kuku anategemea kupata nyama na mayai toka kwa kuku hawa anaowafungulia asubuhi watoke nje na anaowafungia jioni wakishaingia ndani toka kokote nje wanakoishi kivyao!

Hivi ndivyo wanasoka wetu wa Tanzania walivyo.Leo tunafurahia vitu vya akina Mrisho Ngassa,Juma Jabu,Nadir Haroub,Shadrack Nsajigwa,Salum Swedi,Juma Kaseja,Mussa Hassan Mgosi na wengine wengi bila kutafakari wachezaji hao walipata malezi gani ya awali ya mchezo huo na sasa hivi wanaishi vipi, kwa maana ya kupata nasaha za kuwajenga kisaikolojia  na baadaye wataishi vipi soka yao ikifikia tamati.Watatumikaje kwa manufaa ya wanasoka wa miaka ijayo.Hatuna mpango rasmi wa kitaifa wa kuhakikisha soka yetu hii ya ridhaa inakuwa na mipango ya kisayansi ya kuibua,kuimarisha na kuinua vipaji vya wanasoka wetu lakini tunategemea kupata mafanikio ya mchezo huo kimataifa kama mfugaji wa kuku wa kienyeji anavyotegemea kupata mayai mengi na nyama tamu toka kwa kuku wanaoishi kivyao! Mingi ya mipango hiyo iko juu ya uwezo wa TFF na hivyo serikali yenyewe ndiyo inapaswa ipange na kusimamia mipango hiyo.Kwa mfano,uwezo wa TFF unaishia kuvilazimisha vilabu vyetu vya ligi kuu kuwa na timu za vijana,jambo ambalo kisayansi haliwezekani.

Hili haliwezekani kwa sababu umri wa vijana hao wa kuwemo ndani ya timu hizo, wa miaka 21 kurudi chini, ni umri wa kuwa shuleni.Hapo serikali yenyewe ndiyo inaweza kutengeneza timu za uhakika za vijana kwa kuanzisha,katika kanda zote za kijiografia za nchi yetu,shule maalum za sekondari za watoto wenye vipaji vya michezo.Hizo shule ndizo zitakuwa timu za uhakika na za kudumu za vijana.Lakini kijana wa umri wa miaka 17 hawezi kuchezea timu ya vijana ya klabu yoyote kwani hataweza kuishi maisha ya kitimu ya soka muda wote wakati muda huo anapaswa kuutumia shuleni.Hii ina ukweli mzito kwa maisha yetu ya sasa,ikizingatiwa kuwa elimu ya msingi ya Tanzania kwa sasa ni ya kidato cha nne (Form Four).Kwa wakati tulio nao, huwezi kuwapata vijana wa umri huo wasio shuleni.

Kwa hiyo, mipango isiyo ya kisayansi ya soka yetu inasababisha kujikwamua kwetu kutoka kwenye soka duni kuwe kwa kulazimisha lazimisha na wala si kule kunakofanyika kisayansi ambako kunafuata hatua moja hadi nyingine za maendeleo zinazohusisha zaidi mwanasoka kuishi kisoka halisi tangu utotoni.Kinyume chake, wachezaji wetu wengi wanaibuka kivyao vyao tu toka mitaani. Katika kulazimisha huko, tukajikuta tukimtafuta kocha Marcio Maximo wa Brazil.Tangu aliopokuja mwaka 2006,kocha huyo amefanya aliyoyaweza na ameshindwa yaliyoshindikana.Hivi karibuni ameongezewa mkataba wa mwaka mmoja.Kwa hiyo kuna mjadala mkubwa sana wa endapo kuongezwa huko kwa mkataba kuna faida au hasara kwa Taifa letu kisoka.Mjadala huu ni mkali sana kwani una pande mbili zinazoonekana kulingana kwa idadi ya watu waliopo kila upande.Hii inathibitishwa na ukweli kwamba popote pale mjadala huu unapoanzishwa kunakuwa na idadi inayolingana ya wanaosema ni faida na wale wanaosema ni hasara kuendelea kwa kocha huyo kuifundisha timu hiyo. Mfano mmojawapo wa hali hiyo ni ule uliojitokeza kwenye kipindi cha Ulimwengu wa Michezo cha Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) cha Jumamosi,Machi 28,2009.Watanzania wachache waliochangia hoja ya mkataba mpya wa kocha huyo waligawanyika sawa kwa pande mbili za faida na hasara.Hivi ndivyo ilivyo kila mahali nchini kuhusu mjadala huo.

Hoja nyingi za kusema kuna faida au kuna hasara ya kuendelea na Maximo,zinatokana na jinsi alivyowapa raha au alivyowakera Simba au Yanga lakini hilo halijulikani kwa sababu haliwekwi wazi na watoa hoja hao.Ukitaka kugundua ukweli huo,sikiliza kwa makini hoja zao.Nyingi haziendi mbali zaidi ya “apewe nafasi nyingine”,”asisakamwe aachwe afanye kazi”,”ametutoa chini,mwacheni aendelee kutuinua” na kadhalika toka kwa wanaosema kuna faida kwa kocha huyo kuendelea kuifundisha timu yetu ya Taifa. Watanzania hao hawaelezi kuna faida gani ya kuanzia sasa na kuendelea kwa kocha huyo kubaki kuifundisha timu yetu ya Taifa.Kwa wale wanaopinga kwa hoja za kishabiki kubaki kwa kocha huyo, utawasikia wakisema “aondoke kwani amefika mwisho wa uwezo wake”,”sasa tujaribu kocha toka Ulaya”,”Maximo hafai”,”hakuleta kombe hata moja” na mengine mepesi yasiyoangalia tulikuwa na soka ya maandalizi yapi ya utotoni,kocha huyo katutoa wapi na katufikisha wapi.Hakuna hoja toka kwa Watanzania hao zinazoonyesha hasara tutakayopata kuanzia sasa kocha huyo akiendelea kufundisha timu yetu.

Pamoja na Maximo kuonekana wazi kuwa kocha aliyejulishwa kuhusu siasa za Yanga na Simba mara tu alipofika,lakini ameshindwa kuwaridhisha mashabiki wa vilabu hivyo kwa asilimia zote licha ya kujitahidi sana kufanya hivyo.Uthibitisho wa darasa alilopewa kuhusu nguvu za Yanga na Simba kwa soka letu unaonekana kwa jinsi anavyowianisha siku zote idadi ya wachezaji toka Yanga na Simba kwenye timu hiyo.Inasadikiwa hata hatua kali za hivi karibuni za utovu wa nidhamu kwa wachezaji wawili wa timu hiyo Haruna Moshi “Boban” wa Simba na Athumani Idd “Chuji” wa Yanga zimechukuliwa kwa mmojawao katika misingi hiyo hiyo ya kukwepa kuudhiana na watu wa Yanga au wa Simba pekee.Inasemekana mmoja wa wachezaji hao (haijulikani ni yupi) ametolewa kafara ya Uyanga na Usimba!

Inasemekana pia hali hiyo ndiyo iliyomtia kitanzi kocha huyo cha kutomrudisha kwenye timu hiyo hadi sasa kipa namba moja wa nchi hii Juma Kaseja “Juma K. Juma” licha ya kipa huyo kuwa juu sana ya makipa wote nchini na nchi yetu kuwa na uhaba wa makipa wazuri kwa sasa.Alimuondoa kwenye timu ya Taifa kwa sababu inayofahamika kibinafsi alipokuwa Simba.Sasa yuko Yanga,inasemekana, anaogopa kumrudisha kwenye timu hiyo asije kuonekana kuwa kumnunia kwake kulikuwa kwa sababu alikuwa mchezaji wa Simba! Kwa hiyo,kocha huyo anatekeleza mkakati wa kuwaridhisha wote Yanga na Simba katika kiwango cha kutupa hasara wakati fulani kama ilivyo kwenye suala la Kaseja na kwenye suala la kumpoteza mchezaji mmoja mahiri kati ya Haruna Moshi na Athumani Idd kwenye timu ya Taifa kwa matatizo ya mmojawao,kama maelezo kuhusu mambo hayo mawili ni ya kweli.Licha ya hayo,kama ni ya kweli,hakufanikiwa kuwaridhisha pande zote kwani wanaosema kocha huyo aondoke kwa misingi ya kishabiki ni mashabiki wa timu zote mbili za Yanga na Simba.

Ukiacha hoja hizo za kishabiki,naomba niongelee hoja za kimantiki nilizokusanya toka kwa Watanzania wenye misimamo tofauti kuhusu kubaki kwa kocha Marcio Maximo.Kwa wale wasio na hoja za kishabiki wanaoona kwamba ni faida kwa Taifa kwa kocha huyo kubaki, wana hoja ambazo ukizikusanya zinatengeneza hoja kuu kwamba kocha huyo ameshajifunza kuhusu jinsi soka yetu inavyotengenezwa na yeye tayari anapanga mipango ya ufundishaji wa timu yetu kwa kuzingatia hali hiyo.Hii inathibitishwa na jinsi anavyowaibua wachezaji wachanga na kuwakuza wakiwa ndani ya timu ya Taifa.Mfano ni jinsi alivyowajumuisha wachezaji wadogo kama Jerry Tegete,Kigi Makasi na wengine kwenye timu hiyo nao kukomaa wakiwa humo ndani mpaka kuwa wachezaji wa kutegemewa sana sasa wa timu ya Taifa.Sasa hivi anawainua vijana wengine wadogo zaidi kama Mwinyi Kazimoto,Zahor Pazi,Razak Khalfan na wengine.Kwa kufanya hivyo,kocha huyo anaonekana kuwa na mkakati wa wazi wa kuziba pengo lililopo katika mipango yetu ya soka.Pengo hilo ni kukosekana kwa soka la vijana.Kwa hiyo,vijana hao wadogo wakijengwa na kujengeka vizuri,watakuwa wa faida kubwa kwa soka yetu miaka ijayo na wataweza kufanya makubwa sana kwa Taifa lao miaka hiyo.

Watanzania wenye hoja hizo,wanaona kuwa kumuondoa kocha huyo sasa ni kukata ghafla mikakati hiyo kwani atakapokuja kocha mwingine ataingia moja kwa moja kwenye juhudi za kuleta furaha ya leo,baada ya kujua nini kimemfanya mtangulizi wake asikubalike.Akifanya hivyo,kocha huyo mwingine atajielekeza zaidi kwa wakongwe wa kuleta mafanikio ya sasa tu na matokeo yake tutarudi  kulekule.Hoja hizi zina mantiki na zinajadilika.Kwa upande mwingine,wanaoona kuna faida kwa Maximo kuondoka,wasio na hoja za kishabiki, wanakuja na hoja ya msingi ya jumla kwamba kocha huyo haipeleki mbele soka yetu kutokana na kujielekeza kwenye mipango ya kuinua vipaji kila siku.Watanzania wa msimamo huo wanatoa hoja kwamba alipoanza kutengenezan timu mwaka 2006 angekuwa akiwaacha wakongwe wakiwa wanafutika polepole toka ndani ya timu hiyo huku vijana wakichukua nafasi zao kidogo kidogo badala ya kuanzisha timu mpya kila baada ya muda kama anavyofanya sasa hivi.Watoa hoja hizo wanaona kuwa Maximo anaogopa kukamilisha timu ya ushindani ili kila ikishindwa kufanikiwa kwenye mashindano mbalimbali, jibu liwe anatengeneza timu.Watanzania hao wanaamini kuwa Maximo ameajiriwa si kwa kutengeneza timu tu miaka yote na hapo ndipo wanapokuja na hoja kwamba ameshakamilisha lengo la kutengeneza timu na hivyo sasa achukue mwingine na malengo ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika ya wachezaji wote (CAN) ambapo naye akifikia au kukaribia lengo hilo, aondoke kumwachia mwingine wa kutekeleza malengo ya kutupeleka kwenye fainali za kombe la Dunia.Hoja hizi nazo ni za msingi na zinajadilika.

Kwa mtazamo wangu,awe Maximo au kocha mwingine,jambo la msingi ambalo Watanzania tunapaswa tufanye ni kumpa kocha wetu masharti ya kimkataba kwamba tunataka atufanyie nini.Tumueleze wazi kuwa wengi wa wachezaji wetu wamechipuka kutoka timu za mitaani.Hawakutoka kwenye shule rasmi za soka.Hivyo tunataka awatengeneze wawe wachezaji kamili wenye vitu vya kutosha vya uchezaji soka.Tumweleze tunataka atufanikishie mambo yapi ya soka ya kimataifa kwa muda upi.Sisi ndiyo waajiri wa kocha na tunamlipa kwa kutufikisha kwenye lengo letu.Kama kumueleza mahitaji yetu kutachukuliwa kama kumuingilia katika kazi,basi hakuna haja ya kujishughulisha na soka kabisa.Tunamtetemekeaje mtu tuliyemuajiri na kumlipa? Yeye ndiye alipaswa kututetemekea sisi waajiri wake.

Hata kumtaka (siyo kumuomba) atupatie taarifa za kina za kuwanunia wachezaji Juma Kaseja”Juma K.Juma”,Athumani Idd “Chuji” na Haruna Moshi “Boban” ni jambo ambalo TFF ilipaswa ilifanye kwa usahihi kabisa na kumshauri nini afanye kufuatia atakayoeleza kwenye taarifa hiyo.Hatua kama hii ni ya usimamizi wa utawala wa soka na si ya kuingilia utaalam wa kocha.Kosa lingekuwepo kama swali lingekuwa kwa nini hamchagui mchezaji fulani kwenye timu ya Taifa wakati ana kipaji.Hapo ingekuwa ni kuingilia mipango ya kocha lakini kumuuliza kuhusu nini kimetokea baina yake na wachezaji aliokwishawachagua kwenye timu ya Taifa si suala la kitaalam bali la kiutawala.Vinginevyo,kamati ya Ufundi ya TFF ina kazi gani?

Tuanze upya kupangilia mipango yetu ya maendeleo ya soka kwa kuwatazama Watanzania na hulka zao za soka lakini tusiwadekeze kwa Uyanga na Usimba kana kwamba shughuli ya uendeshaji wa soka yetu ya kimataifa ni ya kijiweni kwenye ubishi wa kijinga wa Yanga na Simba.Uchaguzi wa wachezaji wa timu ya taifa usizingatie kutowaudhi watu wa Yanga na Simba bali uzingatie ubora wa wachezaji.Hatua za kinidhamu kwa wachezaji nazo zihusiane na makosa yao tu na si kuangalia kama mchezaji huyu ni wa Yanga au wa Simba. Inafaa tutazame mfumo wa soka letu kwa ujumla wake na kuangalia nini cha kufanya na kocha wetu wa timu ya Taifa.Ni muhimu kina Maximo wasiwe juu yetu na kufanya chochote kile hata cha matashi  binafsi.Mbona ameshauriwa asiwaudhi Yanga wala Simba na anatekeleza,kwa nini tunaogopa kumshauri na mengine ya msingi? Tunataka maendeleo ya kweli ya soka yetu na si siasa wala kufurahisha watu.

ibramka2002@yahoo.com

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version