Maelfu ya washabiki wa Arsenal walijitokeza mitaani Jumapili hii kushangilia timu yao kutwaa Kombe la FA.
Arsenal wamemaliza ukame wa miaka tisa kwa kuwafunga Hull 3-2 kwenye mechi ngumu iliyochezwa hadi muda wa ziada.
Wachezaji na kocha Arsene Wenger walikaa kwenye mabasi mawili makubwa yaliyo wazi juu katika maandamano yaliyoanzia uwanjani kwao Emirates na kuzunguka mitaa ya Islington kwenye gwaride la mashujaa.
Washabiki walionekana kujawa furaha kuliko hata wachezaji, wakisema kwamba sasa timu yao imepiga abautani na itaweza tena kuwapa raha baada ya kukaa bila kombe tangu 2005.
Wenger amethibitisha atabaki Arsenal kama kocha kwani atasaini mkataba mpya, akasema wachezaji wake walionesha ukomavu, hasa kwa kutoka nyuma walipokuwa wamefungwa mabao 2-0 katika dakika nane za mwanzo hadi kutwaa kombe katika Uwanja wa Wembley.
Ilikuwa siku yenye joto zaidi tangu mwaka huu uanze, ambapo Jua liliwaka huku mbingu zikionekana wazi kuwa za bluu, Nahodha Thomas Vermaelen akasema kombe hilo ni kichocheo kwa timu yake.
Wenger na vijana wake walikuwa wakicheka, wakicheza na kuwapungia washabiki. Mara ya mwisho walitwaa kombe hili hili walipowafunga Manchester United 5-4 kwa penati.
Ushindi huu umekuja baada ya miaka minane, miezi 11, siku 26 na sekunde 38, katika mwaka ambao Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho alimkejeli Wenger kwamba amebobea katika kushindwa.
Imetokea kwamba mwaka huu Chelsea hawakupata taji lolote lile na Manchester United kufanya vibaya zaidi kwenye ligi hadi kumfukuza kocha wao, David Moyes aliyekaa madarakani kwa miezi 10 tu.
Aaron Ramsey aliyefunga bao la ushindi alisema kwamba kombe hilo ni zawadi kwa Wenger kutokana na jinsi anavyokaa nao, kuwaunga mkono katika shida na raha, akiwapa mbinu nzuri za kucheza.
Jumamosi hiyo ya ushindi Wenger alionekana tena mwenye raha badala ya kukunja ndita, ambapo aliloweshwa kwa shampeni, akiwa katika ‘sare’ yake anayoipenda ya shati jeupe na suruali nyeusi.
“Wakati mwingine furaha huunganishwa na mateso na muda mwingi ambao lazima ukubali kusubiri, mafanikio yanapokuja huwa ni wakati wa kipekee sana,” akasema Wenger ambaye ameizolea klabu hiyo makombe matano ya FA.
Wachezaji walichukua kipaza sauti na kwa pamoja wakaimba wimbo wa kuisifu klabu yao, huku beki mrefu Mjerumani, Per Mertesacker akiweka kionjo ‘Ni Arsenal hadi nife’ na kuwapa washabiki matumaini mapya.