MCHEZO wa watani wa jadi uliomalizika kwa ushindi wa Yanga wa 1-0 dhidi ya Simba umetuonesha umahiri na akili nzuri za wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania. Kikubwa zaidi wachezaji wazawa na wageni kwa pamoja wameonesha mchezo ambao unathamnisha Ligi Kuu na kuzidisha mvuto kwa majirani zetu Kenya,Uganda,Zambia, DRC, Msumbiji, Malawi na kwingineko barani Afrika.
Thamani ya Ligi Kuu ilionekana hata pale Televisheni kubwa kutoka Afrika kusini ilipoomba haki ya kuonesha Wiki ya Mwananchi wakati Yanga walipopepetana na Kaizer Chiefs. Katika mchezo uliomalizika Oktoba 19 mwaka huu ndani ya dimba la Benjamin Mkapa wapo wachezaji ambao wanastahili kupewa maua yao ya pongezi. Ni wachezaji ambao wameonesha kwanini wanastahili kuanza kikosi cha kwanza za Simba na Yanga. Na huu ni mzunguko wa sita (mechi ya sita) ya Ligi Kuu Tanzania bara.
Miguel Gamondi ana raha zake
Kocha wa Yanga ameongoza kikosi chake kuibuka na ushindi muhimu katika Ligi Kuu dhidi ya wenyeji wa mchezo Simba. Upangaji wa kikosi cha Yanga unaweza kumpa sifa kocha huyo. Uamuzi wa kuwaweka pamoja Pacome Zouzoua na Aziz Ki kisha mbele yao akampanga Prince Dube, maana yake alikuwa na wabunifu wawili ambao walikuwa na kazi ya kuipangua safu ya ulinzi ya Simba. Katika mfumo wa 4-3-3 tena kwenye derby ilidhaniwa angeweka mshambuliaji mmoja na kiungo mshambuliaji mmoja huku wengine wakiwa na jukumu la kuilinda timu. Kuwapanga Aziz Ki na Pacome ina maana kocha alimtegemea Pacome kurudi kusaidia ulinzi wakati Aziz akiwa na jukumu la kucheza nyuma ya mabeki kumsaidia Dube. Kwa hakika mpangilio wake unapasw akupongezwa.
Nani angekuwa mchezaji bora?
Huu ni mtihani mzito kwani, mchezo ulivyokuwa umeonesha umahiri wa wachezaji wa vikosi vyote vya Yanga na Simba. Lakini Charles Ahoua, Pacome Zouzoua,Che Malone, Augustine Okejepha na Aziz Ki bila shaka yoyote hawa wangeweza kugawana tuzo moja ya mchezaji bora wa mchezo. Umahiri na ubunifu walioonesha kwa muda waliocheza unaonesha kuwa usajili wao ni wenye thamani kubwa sana. sasa katika orodha hiyo huwezi kumweka kando Djigui Diara ambaye aliokoa mchomo ambao ungezua habari nyingine ya kusikitisha kwa Yanga. Ni orodha ambayo inakufanya uwape maua yao kwa umahiri walioonesha.
Yusuf Kagoma karibu kwenye ‘Show za Kibabe’
Huyu kipaji anacho. Uwezo anao mkubwa. Uhodari wa kupambana kwa muda mrefu yaani dakika 90 za mchezo anao mkubwa na kwamba Simba wamefanya usajili makini sana katika eneo la kiungo. Hii ni mechi yake ya kwanza kubwa dhidi ya Yanga. Ni mchezaji ambaye alikuwa kwenye mzozo baina ya Yanga na Simba, lakini kanuni za Ligi Kuu zilikuwa zinaipa Simba nafasi na haki ya kumtumia kijana wa Kitanzania.
Yusuf Kagoma hawezi kuwa kama Christopher Alex Massawe ambaye alikuwa anatamba katika eneo la kiungo mkabaji. Ni eneo ambalo hata Suleiman Matola alitamba nalo. Kagoma hawezi kuwa Fabrice Ngoma au Hussein Amani Masha lakini anakuwa kiungo aliyelata uhai na ushindani mkubwa kikosini. Aliyependekeza usajili wake lazima apewe maua yake.
Simba walikuwa wanamtegemea Fabrice Ngoma na Mzamiru Yassin katika misimu kadhaa, lakini ujio wa Yusuf Kagoma kutoka Tabora United umeongeza maarifa na kufanya eneo la kiungo kuwa imara. Lakini katika mchezo dhidi ya Yanga hakuwa na utayari wa kukabiliana na presha ya mechi kubwa. Katika mchezo huu wa sita, jambo ambalo anapaswa kuambiwa ni ‘karibu kwenye show za kibabe’. Kuumia kwake katika mchezo huo haina maana ni mwisho wa kipaji chake lakini angalau anatakiwa kuimarika na kutambua kuwa hizi ni show za kibabe za Kariakoo Derby.
Mousa Camara ametemea ndani lakini anajua kazi
Ingawa timu yake imefungwa 1-0 lakini ni kipa ambaye ameonesha uwezo na thamani yake. Simba wana kila sababu za kumlinda golikipa wao, licha ya kupangua mpira vibaya ambao ulimkuta Maxi Nzengeli alipiga shuti kali lililomgonga Kevin Kijiri na kutinga wavuni. Katika mazingira yale golikipa hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kutua chini tofauti na mweleko wa mpira. Huenda mpira ule ungekwenda kwenye kona ya lango, naye kama binamu hesabu zake zilikuwa kuzuia hatari ambayo ingetokea, lakini akaishia kutema mpira. Kimsingi uwezo wake wa kunusa hatari langoni na kuokoa michomo ndiyo ulilochangia aumie bega lakini aliendelea na mchezo. Huyu ni aina ya golikipa wa kisasa na hakika Aishi Manula na Ali Salim wamepata mpinzani mahiri langoni.