Mambo ya virusi vya corona na ugonjwa uuletao wa Covid-19 yanazidi kupamba moto, athari zikiendelea kuonekana huku vita ikizuka kati ya wanasoka na klabu zao.
Hadi sasa wanasoka, wakiwamo wa ligi kubwa duniani, wapo majumbani mwao, kila mmoja akiendelea na mazoezi kivyake na wengine wakijiuguza baada ya kupata maambukizi ya Covid-19.
Lakini sasa kadiri muda unavyokwenda na klabu kutokuwa na mapato ya kueleweka, hasa kutokana na viingilio na kwingineko kwa sababu ya udhamini kusimama, menejimenti za klabu zimeamua kukata waajiriwa mishahara.
Wakati wale wanaofanya kama vibarua, hasa siku za mechi wamepumzishwa kwa lazima kwa vile hakuna mechi wala matukio na hivyo kukosa fedha ambazo hulipwa kwa wakati husika, shoka linaelekezwa kwa wanasoka wenyewe.
Tayari Barcelona, kwa mfano, wamewaita nyota kwa maana ya wachezaji waandamizi na kujadiliana nao juu ya athari za kiuchumi kwa hali hiyo mbaya na kwamba watalazimika kukatwa mishahara, klabu nyingine zinaonekana kuanza kuchukua hatua huku baadhi ya wachezaji wakiwa hawataki kusikia kukatwa mishahara.
Kwa ujumla, hadi sasa hakuna suluhu iliyopatikana Ulaya juu ya masuala haya ya virusi vya corona na athari zake, kukiwa na giza juu ya hatma ya wachezaji, hasa ikizingatiwa kwamba kwa kawaida mkataba kwa msimu humalizika Mei mwishoni na kuanzia Juni ni mikataba mipya.
Ugonjwa unazidi kung’ata na haijulikani lini msimu wa ligi za Ulaya utamalizika, kama ilivyo pia kwa Amerika, Asia na Afrika, watu wakiwa wamebaki majumbani.
Kuanzia klabu kama FC Sion hadi Dinamo Zagreb zinakabiliwa na hali ngumu na wachezaji hawataki kukubali makato. Kimsingi soka ndiyo sekta inayolipa zaidi, ikiwa ni asilimia 64 ya mapato yake yote kwenye mishahara, sasa imesimama na haijulikani kipi kinaendelea na lini itarejea.
Klabu katika ngazi zote zinajaribu kutazama upya mwenendo ili kupunguza matumizi kwa sababu mapato tayari yameathiriwa kwa njia hasi, huku serikali za mataifa zikiendelea kuchukua hatua kali kama kutaka watu wabaki majumbani, kuzuia ndege kuingia na kutoka, kufunga mipaka na kupiga marufuku mikusanyiko.
Kila ligi ina changamoto za peke yake, lakini moja linalofanana kwa wote ni ukosefu wa mapato wakati huu, na umoja wa wanasoka chini ya Fipro unatazama kuwapigania wachezaji hao wa kulipwa wasiathiriwe mno na mdororo wa uchumi.
Huko klabuni Sion, Uswisi, wachezaji tisa – wakiwamo wachezaji tisa wa zamani wa Arsenal, Alex Song na Johan Djourou – wamefukuzwa kazi baada ya kukataa kukatwa mishahara baada ya klabu kuamua kwamba wanaolipwa zaidi watakatwa hadi asilimia 80 ya mapato yao. Sasa wamepanga kwenda mahakamani kushitaki klabu ili kupata kile wanachoona kwamba ni haki yao inayominywa.
Wachezaji wengi wanataka kama kuna kupunguzwa mishahara au posho, kufanyike baada ya majadiliano mazuri na si uongozi kuamua tu na kutekeleza. Ama kwa Dinamo Zagreb, wachezaji wamekataa uamuzi wa kuwakata kima cha theluthi ya mishahara yao kwa miezi sita. Chama cha wanasoka wa Croatia kinasema kwamba hata kama wachezaji wanataka mazungumzo, ni mapema mno kuamua sasa kwamba wataweka makato kwa miezi sita.
Kwa nchi za Skandinavia, klabu zimewaambia wachezaji wa kigeni kwamba wakatwe asilimia kati ya 25 hadi 50 na waondoke kwenda kukaa majumbani mwao katika nchi watokazo kwa ajili ya Covid-19 ili klabu ziweze kuleta uwiano wa daftari zao za hesabu na ukaguzi wake.
Katibu Mkuu wa Fipro, Jonas Baer-Hoffmann anasema kwamba wanasononeshwa na kwamba klabu zinachukua hatua binafsi kwa ajili ya kupunguza mishahara ya wachezaji wakatihuu, hata kufikia theluthi mbili, kitu wanachosema hakiukubaliki. Anasema wanajua hali ya uchumi ilivyoathirika, lakini ni muhimu kukafanyika mazungumzo na wachezaji au vyama vyao mbalimbali.
Wakala mmoja anasema hali kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) ni mbaya, na kwamba kuna aina mbili za klabu – zenye uwezo ambazo wala hazijatikisika na zinaendelea kulipa mishahara na posho kama kawaida, lakini kuna nyingine zinazotazama hali kwa hadhari na lazima zitaweka makato.
Nchini Ujerumani, wachezai wa klabu za Bayern Munich, Borussia Dortmund na Borussia Mönchengladbach wamekubali makato lakini wamekwenda mbali zaidi kuchangia klabu ndogo. Wamekubali makato hadi asilimia 70 wakati huu mgumu wa Covid-19.