Menu
in , ,

WANAMICHEZO NA KUJIENDELEZA KIELIMU

Wanamichezo wengi huwa wanapata tabu sana kupata shughuli ya kufanya pindi wanapostaafu kucheza michezo. Na jambo hili huwapelekea watu wengi kwenye hali ngumu sana za kimaisha. Ugumu huo wa kimaisha umewapelekea wengi wao kupata ugonjwa wa sonono(stress) na hii inatokana na wengi wao kushindwa kukubaliana na hali za kimaisha ambazo huwa wanajikuta wamo ndani yake. Sonono imewapelekea hata baadhi yao kujaribu kufanya maamuzi magumu na ya hatari ambayo baadhi yao yalihatarisha maisha yao. Wachezaji wengi kwa kukosa ujuzi wa ziada(professions) huwa wanajikuta kwenye hali ngumu na wengi wao hukosa shughuli za kufanya za kuwaingizia vipato na hili huwapelekea kuwa kwenye hali ngumu kwani wanakuwa wanakosa vipato vya uhakika vya kuendeleza maisha yao.

Hivi karibuni zilizagaa picha kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilikuwa zinamwonyesha mchezaji wa kimataifa wa Tanzania ambaye anachezea klabu ya JKT Tanzania bwana Shiza Kichuya akiwa amevaa gwanda za jeshi la kujenga taifa huku maelezo yakiwa yanaeleza kwamba mchezaji huyo amefuzu mafunzo ya awali ya kulitumikia jeshi la kujenga taifa na kwamba kuanzia kwa sasa anaajiriwa kwenye jeshi hilo kama askari. Wadau wengi wanaofuatilia michezo mitandaoni walitoa maoni yao huku wakiwa kama wanasononeka kwamba mchezaji huyo amepoteza njia na huku wakiwa wanamuonea huruma. Wachache walimsifu mchezaji huyo kwa kitendo chake hicho cha kwenda jeshi na wakamuona kama ni mwanamichezo ambaye amezisoma alama za nyakati na ameona kwamba umri wake wa kucheza soka umeshafika ukingoni na anahitajika apate shughuli ya ziada ambayo itamwezesha kuwa na kipato cha uhakika katika nyakati ambapo atakuwa amestaafu kucheza soka la kulipwa. Kichuya kama ilivyo kwa wachezaji wengi waliopo kwenye mchezo wa soka ameng’ara kwa misimu michache sana na akabahatika kucheza vilabu mbalimbali vikubwa nchini Tanzania na nje ya nchi.

Wanamichezo wengi tumezoea kuwaona kwamba pindi wanapostaafu kucheza michezo ya kulipwa huhamia kwenye ukocha wa michezo hiyo. Ni jambo jema lakini changamoto ni kwamba sio kila mchezo huwa na kipato kizuri pindi wachezaji hao wanapoamua kuingia kwenye ukocha. Kwa Tanzania tunaona mwanamichezo kama Japhet Kaseba ameibukia kwenye ukocha wa mchezo wa Kickboxer baada ya kustaafu mwanamasumbwi Rashid Matumla naye ameibukia kwenye ukocha wa masumbwi, wachezaji wa mpira wa kikapu nao kuibukia kwenye ukocha wa mchezo huo katika maeneo mbalimbali halikadhalika tumeona wanariadha wengi nao halikadhalika wakaibukia kwenye ukocha wa riadha katika maeneo mbalimbalia nchini Tanzania.

Nchini Nigeria wanamichezo wengi wamekuwa wanajiendeleza kielimu kwa namna tofauti ili waweze kuwa na kipato cha uhakika pindi wanapomaliza kucheza michezo ya kulipwa. Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia mwanamichezo kama mwanasoka maarufu wa nchi hiyo bwana Obafemi Martins kuamua kujiunga na chuo kikuu cha Havard nchini Marekani ili ajiendeleze kielimu kwa kuamua kusomea shahada ya biashara. Rais mstaafu wa Liberia bwana George Weah pindi alipostaafu kusakata kabumbu aliamua kurudi darasani na kusoma na hatua hiyo ilimsaidi kuweza kusoma mpaka kufikia kiwango cha kuwa na elimu ya juu ya shahada na hatua hiyo ilimsaidia kuweza kuwania kiti cha uraisi wa nchi hiyo na kushinda.

Tanzania Sports

Kwa barani ulaya suala la kujiendeleza kielimu sio suala lenye ugeni sana kwani wanasoka na wanamichezo wengi tu ambao wana viwango vikubwa vya elimu ambavyo huwa vinawasaidia kimaisha pindi wanapostaafu kucheza soka la kulipwa. Elimu hizo huwafungulia njia nyingine za kimaisha ambazo baadhi yao huzitumia hata wakati wanapokuwa wanacheza kutengeneza vipato vya ziada. Mwanasoka wa zamani wa Chelsea bwana Frank Lampard ana shahada ya lugha ya kilatini kutoka Brentwood school, beki wa italia Giorgio Chiellini ana shahada ya kwanza ya uchumi na shahada ya uzamili ya biashara, beki wa zamani wa Manchester City Vincent Kompany ana shahada ya biashara kutoka Alliance Manchester Business school, kiungo wa zamani wa Chelsea Juan Mata ana shahada ya sayansi ya michezo kutoka Camilo Jose Cela University, kipa wa zamani wa Liverpool ana shahada ya sayansi ya siasa, kiungo wa zamani wa Barcelona Andres Iniesta ana shahada ya kwanza baiolojia na shahada ya uzamili ya sayansi ya michezo, mchezaji wa zamani wa Brazil Socrates ana shahada ya juu ya uzamivu(PHD) katika falsafa, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa urusi Andrey Arshavin ana shahada ya uzamili ya ubunifu wa mitindo, beki wa zamani wa Chelsea Glen Johnson ana shahada ya hisabati.

Kujiendeleza kielimu hakupo tu katika mchezo wa soka peke yake bali ni suala ambalo liko katika michezo yote. Mchezaji maarufu wangumi duniani kutoka taifa la ufilipino bwana Many Pacquiao ana shahada ya uzamili katika masuala ya utawala wa umma na hili limemsaidia hata katika harakati zake za kisiasa ambazo zilistawi Zaidi baada ya kustaafu ngumi za kulipwa, mwanamichezo maarufu wa mieleka wa Marekani bwana Drew Mclutyre ana shahada ya uzamili katika masuala ya kuzuia uhalifu. Mwanariadha Christine Oluruogu ambaye amewahi kuwa mshindi wa Marathon kwa mara kadhaa ana kiwango cha elimu cha shahada ya kwanza katika fani za lugha (linguistics). Mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu(basketball) Shaquile Oneal ana shahada ya uzamili katika biashara kutoka chuo kikuu cha Philadelphia na shahada ya uzamivu katika masuala ya elimu kutoka chuo kikuu cha Barry University.

Mafaniko ya wanamichezo kupitia elimu sio suala ambalo lipo katika nchi ambazo zilizoendelea tu peke yake bali ni suala ambalo hata nchini kwetu Tanzania lipo piaila tofauti ni kiwango cha mafanikio. Aliyewahi kuwa raisi wa shirikisho la soka Tanzania bwana Leodgar Chilla Tenga kwa sasa anashikilia nafasi nyingi tu za kiutendaji katika bodi za mashirika ya umma pamoja na binafsi na kabla ya kushika nafasi hizo aliwahi kuwa mchezaji mahiri wa soka nchini Tanzania. Katibu mkuu wa wizara ya utamaduni, Sanaa na michezo bwana Ally Mayay aliwahi kuwa mwanasoka mahiri nchini Tanzania ambapo aliwika katika vilabu kadhaa. Mkurugenzi mstaafu wa shirika la NSSF na balozi mstaafu wa Tanzania nchini Malaysia bwana Dokta Ramadhan Dau aliwahi kuwa mcheza soka mzuri ambapo alicheza vilabu kadhaa ikiwemo Pan African.

Ni jukumu la wazazi kuwasimamia watoto wao wenye vipaji vya michezo waweze kufika mbali halikadhalika kuwahimiza kutoachana na suala la kujiendeleza kielimu. Mawakala wa kuwasimamia wachezaji nao wanatakiwa wawasimamie wachezaji wasiache kujiendeleza kielimu.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version