By Idda Mushi, PST, Morogoro
Michezo mingi ambayo imekufa ama kusahaulika ni rahisi kufufuliwa upya kupitia mpango wa mafunzo ya michezo kwa walimu mashuleni ambao wataweza kumudu kufundisha wanafunzi na hatimaye kusambaa katika maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi ya walimu wa shule za msingi na Sekondari walisema hayo wakati wakiongea na PST mjini hapa wakati wa mafunzo ya mchezo wa kuruka upondo ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya riadha yanayotolewa na mtaalamu kutoka nchini Ujerumani.
Walimu hao walisema kuwa mchezo kama upondo uliokuwa umekufa itakuwa ni rahisi kujulikana na kuanza kuchezwa upya baada ya wao kupata elimu ambayo wanakusudia kuitoa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na baadaye uweze kuenea katika sehemu mbalimbali nchini.
Naye mkufunzi wa maswala ya michezo kutoka Ujerumani, Peter Thumm alisema kuwa Tanzania ni nchi yenye vipaji vingi, ambapo kama vikitumiwa vyema nchi inaweza kupata medali nyingi katika fani ya michezo ya aina mbalimbali.
Alisisitiza kuwa iwapo vijana watafundishwa michezo mbadala wanaweza kuwa miongoni mwa wanamichezo wazuri watakaoweza kuiletea sifa nchi kwa kukusanya medali nyingi kwenye michezo hiyo hususani katika michuano ya Jumuiya ya Madola na michuano mingine.
Mafunzo hayo yameshirikisha walimu 10 kutoka mkoa wa Morogoro na yanahusisha walimu waliofaulu kwenye kozi ya kwanza iliyohusu maswala ya riadha ambayo ilimalizika hivi karibuni.
Mafunzo hayo yanalenga walimu hao kujenga uwezo wa kufundisha wanafunzi mashuleni juu ya maswala ya michezo ya aina mbalimbali ambayo kama wakimudu vyema inaweza kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa.