Menu
in , ,

WAKATI TUKIONA GIZA KWA RONALDO, YEYE ANAONA MWANGA

Tanzania Sports

Macho yetu yanatamani kuliona giza la Cristiano Ronaldo. Akili zetu tayari zimeshaamini kwa asilimia kubwa jua limebakiza hatua chache kuzama katika maisha ya soka ya Cristiano Ronaldo.

Miaka 33 ndiyo anayoimiliki. Miaka ambayo haimpi nafasi ya kumfanya awe Cristiano Ronaldo wa miaka 5 iliyopita.

Kasi iliyokuwepo kwenye miguu yake imeshapungua, hata nguvu za miguu yake inaanza kupotea na uzee wa mpira unamkaribia.

Hapa ndipo imani yetu inapojaa, wengi tunaamini maisha yake ya ushindani katika mpira yameshaanza kuingia na giza zito ambalo ni ngumu kulitoa kwa kibatari anachomiliki Cristiano Ronaldo.

Uso wake una majibu tofauti na kitu ambacho sisi tunakifikiria. Nafsi zetu zinaamini Cristiano Ronaldo yuko katika siku za mwisho katika mpira lakini uso wake unaonesha unatamani changamoto mpya.

Hataki kuishi sehemu ambayo haitompa changamoto, anaamini katika changamoto kama mhimiri wa kumwimarisha zaidi.

Ulifikiri Cristiano Ronaldo ameshatosheka na Ballon 5 alizo nazo mkononi mwake? Kuna kitu gani kingine anakita ilihali ana Medali tano za klabu bingwa barani ulaya?.

Kwake yeye maisha ya ushindani hajaisha ndiyo yanaanza ndiyo maana kwa umri wake hakufikiria kwenda kutafuna pesa za China.

Pesa za China hazikuwa na thamani kubwa kwake kama ushindani mkubwa uliopo ndani ya uwanja.

Akili yake inawaza kushinda makombe makubwa, matamanio yake yanampelekea kupata ballon d’or ya 6. Hatamani kuziona siku za mwisho za ushindani wake katika mpira.

Maisha yaliletwa kwa ajili ya maisha. Cristiano Ronaldo analifahamu vyema hili tena kwa kiwango kikubwa ndiyo maana maisha yake yameandikwa katika maisha ya ligi kubwa ulaya.

Hakutosheka na maisha ya Ureno, akaamini England ndiyo sehemu kubwa kwake yeye kuandika maisha mapya kutokana na miguu yake.

Miguu ambayo aliipeleka Hispania. Sehemu iliyobeba ligi bora duniani. Sehemu ambayo alikutana na mpinzani wake mkubwa ndani ya miaka 10 iliyopita katika mpira “Lionel Messi”.

Miaka 9 miguu yake ilitumikishwa katika ardhi ya Hispania kwenye jiji la Madrid. Jiji ambalo limebeba klabu kubwa duniani.

Leo hii maisha yake yanaendwa kuandikwa katika jiji la Turin. Sehemu ambayo ina timu imara na timu yenye historia kubwa duniani ” Juventus”.

Yote haya yanaonesha kwake yeye haamini kama tayari kashafika mwisho kama ambavyo sisi tunavyotamani iwe.

Hajawahi kukata tamaaa, kwake yeye kila uchwao anatamani mafanikio mapya, mafaniko makubwa.

Leo hii tunaweza tukawa tunambeza kwa maneno anayosema kuwa bado yupo kwenye mstari wa ushindani lakini miguu yake inaweza kutuumbua kwa sababu akili yake haijawahi kuamini katika namba za umri wa mtu. Akili zake zinaamini kwenye changamoto kama ndiyo njia ya mafanikio makubwa na yeye anapenda changamoto kuliko kitu chochote duniani, na hii ni ishara tosha kuwa Cristiano Ronaldo bado anasiku za kutufanya tumuimbe kila leo.

Macho yetu yanatakiwa kujiandaa kwa ajili ya kutazama maajabu ya uzee wa miguu ya Cristiano Ronaldo.

Masikio yetu yanatakiwa yajiandae kusikia rekodi nyingi zikivunjwa na kuwekwa na miguu ya kizee ya Cristiano Ronaldo.

Bado tuna dakika nyingi sana za kumwangalia Cristiano Ronaldo, dakika ambazo zitatufanya sisi kuanza kuifuatilia tena ligi kuu ya Italy “Seria A”.

Ligi ambayo ilikuwa imeshaanza kupoteza mvuto ndani na nje ya uwanja lakini kwa miguu ya kizee ya Cristiano Ronaldo kuna uwezekano mkubwa kwa ligi ya Italy “Seria A” kuwa na sura ya kijana kupitia miguu ya kizee ya Cristiano Ronaldo.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version