*Scolari hana wasiwasi na Samba Boys
*Daraja lavunjika na kuzua hofu Brazil
Homa ya robo fainali inazidi kupanda, huku wachezaji saba wa Ujerumani wakikumbwa na mafua kabla ya mechi yao dhidi ya Ufaransa.
Kocha Joachim Low amekiri kwamba wachezaji wake wana matatizo lakini amekataa kutaja majina yao.
Low alisema, hata hivyo, kwamba wachezaji hao waliweza kufanya mazoezi japokuwa wana homa na tezi za makoo yao zilikuwa zinawauma.
Inatambulika kwamba Mats Hummels na Christoph Kramer waliugua mapema wiki hii, ambapo Hummels alikosa mechi dhidi ya Algeria.
Kocha huyu anasema kwamba anaamini safari ya maeneo tofauti Brazil na mabadiliko ya hali ya hewa katika mechi zao nne imechangia. Mazingira ni ya kitropiki, palikuwa na mvua kubwa kisha baridi kali Porto Alegre.
Hata hivyo, Low alisema anaamini hali haitazidi kuwa mbaya hivyo wataweza kuwakabili Wafaransa barabara.
Upande wa pili, kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps alieleza kwamba lazima wachezaji wake waliocheza vyema mechi zilizopita wakaze misuli zaidi.
Deschamps ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, alisema kwamba anahofia Waherumani kutokana na uzoefu wao katika mashindano hayo.
SCOLARI HANA WASIWASI NA BRAZIL
Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari amesema hana wasiwasi na kikosi chake na kwamba kina uwezekano wa kutwaa ubingwa.
Alikuwa akiwajibu wapinzani wake ambao wamekuwa wakidai wachezaji walishindwa kujituma ipasavyo kwenye mechi zilizopita, wakimtegemea mno Neymar na kwamba itakuwa ngumu kuwakabili Colombia Ijumaa hii.
“Washabiki wetu wanataka tuwaambie kile tunachotaka, jinsi tunavyotaka kushinda na jinsi tutakavyofanikisha.
“Sisi tunaendelea na hotuba ile ile; je, tunaelekea kutwaa kombe? Ndio. Tunaingia hatua ya tano sasa,” akasema Scolari.
Kocha huyo ameshambuliwa na wachezaji wa Brazil wa zamani, ikiwa ni pamoja na nahodha wa kikosi cha 1970 kilichotwaa ubingwa, Carlos Alberto.
DARAJA LAVUNJIKA BELO HORIZONTE
Daraja linalounganisha mji wa soka wa Belo Horizonte limevunjika, na katika hali ya hofu kuangukia gari na kuua watu wawili.
Daraja hilo la chumba na zege lililokuwa katika matengenezo lilianguka na kusababisha wasiwasi miongoni mwa watumia vyombo vya moto.
Jiji hili limekuwa mwenyeji wa mechi kadhaa na pia mechi ya nusu fainali wiki ijayo itafanyika hapo.
Idara ya Afya ya Jimbo la Minas Gerais lilipo Jiji la Belo Horizonte ilisema kwamba watu 22 wengine walijeruhiwa na dereva wa basi na mtu mwingine walipoteza maisha.