Wajerumani wametimiza ndoto yao ya kuitawala dunia katika soka, baada ya kuwashinda Argentina 1-0 katika mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Maracana nchini Brazil.
Bao la Ujerumani lilitiwa kimiani na Mario Gotze katika dakika ya 113 baada ya timu hizo wkenda suluhu katika dakika 90 za kawaida. Kocha Joachim Low wa Ujerumani alikuwa amemwambia Gotze wa Bayern Munich kwamba amfunike Lionel Messi wa Argentina.
Gotze alitokea benchi na bado anashikilia rekodi ya kuwa mchezai mdogo zaidi kuanza kuchezea timu hiyo ya taifa. Kocha wa Argentina, Allejandro Sabella hakutulia, akiona jinsi vijana wake walivyokuwa wametoa nuru ya kuweza kutwaa ubingwa huo.
Tofauti na nusu fainali mchekea dhidi ya Brazil ambapo Ujerumani walishinda kwa 7-1, nusura Argentina wawaadhiri Wajerumani hao, ambapo walikosa karibu mabao matatu ya wazi kupitia kwa Lionel Messi, Gonzalo Higuain na Rodrigo Palacio wakiwa na nafasi wazi kabisa za kufunga.
Timu zote zilicheza vyema, na kwa nyakati tofauti zikitawala na kushambulia kwa kasi, japokuwa tangu mwanzo Argentina walijipanga kukaba zaidi na kufanya mashambulizi ya kushitukiza. Messi alicheza chini ya kiwango na Argentina hawakupiga shuti hata moja golini.
Huu ni ukamilisho wa mpango wa miaka 10 wa Chama cha Soka Ujerumani kuijenga upya soka yao kwa kuanzisha kampeni za akademia na kambi nyingine maalumu kuibua na kusuka vipaji, iliyoanza 2004 baada ya kufanya vibaya kwenye michuano ya Euro.
Wakati huo kocha Rudi Voller alijiuzulu kukinoa kikosi hicho, akachukua shujaa wa soka wa Bavaria, Jurgen Klinsmann ambaye sasa anafundisha Timu ya Taifa ya Marekani. Ujerumani waliandaa Kombe la Dunia 2006 lakini wakaishia nafasi ya tatu baada ya kutolewa na Italia kwenye nusu fainali.
Kwenye Euro 2008 bado walipoteza kwa Hispania katika fainali, kutokana na bao pekee Torres. Mipango yao bado haikuwa imekamilika kwani Kombe la Dunia 2010 walipigwa na Hispania na kushika nafasi ya tatu na 2012 wakatunguliwa na Italia kwenye nusu fainali ya Euro wakaishia nafasi ya tatu.
Mwaka huu, chini ya Low, mambo yaliyonekana kutimia, ambapo walicheza vyema tangu mwanzo, japokuwa walihenyeshwa na timu za Afrika, Ghana kwenye makundi walikwenda sare na Algeria wakawapelekesha hadi dakika 120 na kushinda 2-1 hatua ya 16 bora.
Nahodha wa Argentina, Messi aliibuka mchezaji bora wa mashindano huku mchezaji wa Ujerumani, Manuel Neur akiibuka kuwa kipa bora, akakiri kwamba timu imekuwa nzuri sasa lakini pia benchi la ufundi na viongozi wa soka wamechangia kikubwa.
Ilikuwa furaha na vifijo Nahodha Philip Lahm aliponyanyua kombe hilo, huku wachezaji wa Argentina wakilia kwa masikitiko lakini watajilaumu wenyewe kwa jinsi walivyoshindwa kutumia nafasi nyingi walizopata.
Hii ni mara ya kwanza kwa taifa la Ulaya kutwaa kombe hilo katika ardhi ya Amerika, ambapo Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alihudhuria na kushangilia sana bao na pia baada ya mechi kumalizika.
Ni mwanamama anayependa michezo, kwani alifuatilia pia kutoka Marekani wakati Bayern Munich wakicheza na Chelsea kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kwa bahati mbaya Bayern wakapigwa kwa penati.
Ujerumani wamechukua kombe hilo kwa Hispania waliotolewa kwa aibu katika awamu ya kwanza na watatakiwa kwenda kulitetea nchini Urusi, ambako hali ya hewa ya kisiasa ni tofauti baina ya mataifa ya Mashariki na Magharibi, kutokana na utawala wa Vladimir Putin kukinzana kimaslahi na nchi kama Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Italia na nyinginezo.