Wadau zaidi wa soka wameingilia kati na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wachezaji wanaodai kuumizwa dimbani ambao hujirusha au kujiangusha.
Kocha Mkuu wa Everton, Roberto Martinez ametaka wachezaji kuacha kabisa tabia ya kujiangusha wakijidai wametegwa na wapinzani wao.
Mhispania huyo aliyeoa Mwingereza anaamini kwamba kila mmoja katika soka ana wajibu na nafasi ya kumaliza tatizo hilo kwenye soka.
Amechukua hatua hiyo baada ya Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Sepp Blatter kupendekeza adhabu ya muda kama zuio.
“Hili ni kosa letu, limetokea na kuendelea kukua kwa misimu kadhaa sasa. Ni juu yetu sote kujaribu kulifuta,” akasema kocha huyo wa zamani wa Wigan walioshuka daraja msimu uliopita.
Orodha ya wachezaji wa Ligi Kuu ya England (EPL) waliopewa kadi kwa madai ya kujiangusha dimbani na idadi ya kadi zao tangu mwaka 2008 ni Gareth Bale (7), Fernando Torres (3), Adnan Januzaj (3), Liam Lawrence (2), David Bentley (2), Ashley Young (2), Luis Suarez (2), Daniel Sturridge (2), Javier Hernandez (2), Oscar (2), Andy Carroll (2) na Emmanuel Eboue mara mbili pia.
Blatter anasema katika safu yake ya maandishi kwa FIFA kwamba kujiangusha, kujirusha au kudanganya kuumia katika soka kunakera na kwamba husababisha mechi kucheleweshwa kwa muda mrefu.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amemchagiza mchezaji wake mwenyewe, Oscar kwa kujirusha Jumatano hii kwenye mechi dhidi ya Southampton.
Bosi huyo kutoka Ureno amesema Ijumaa hii kwamba Blatter anatakiwa kufanya ziara ya dunia kutoa elimu juu ya tabia hiyo mbaya ya wachezaji kujidai wamekwatuliwa na kuumia.
Hata hivyo, Mourinho alisema kwamba England iwe nchi ya mwisho katika ziara hiyo tarajiwa ya Blatter kwa maelezo kwamba ni nchi ambamo soka ni safi zaidi katika masuala hayo.
Nalo jarida maarufu la Manchester United – ‘Red Issue’ limemtaka kocha wao David Moyes kumalizana na wachezaji wanaohusishwa na kujiangusha uwanjani, na limewataka waziwazi akina Januzaj, Young, Danny Welbeck na Wayne Rooney.