Menu
in

Wachezaji wana ‘hasira’ na corona

Mabingwa

LIGI mbalimbali zinafikia tamati ya msimu wa 2019/2020. Ni msimu ambao umewapa changamoto viongozi wa soka, mashabiki na wachezaji wenyewe. Sababu kubwa ikiwa ni mlipuko wa ugonjwa wa corona ambao ulianzia katika jimbo la Wuhan nchini China na kusambaa kote duniani. Ugonjwa huo umesababisha hasira miongoni mwa wachezaji. Makala haya naelezea matukio muhimu ambayo bila shaka yamewaudhi wachezaji na hawakuwa na namna zaidi ya kukubali matokeo …

UBINGWA WA KIMYA KIMYA

Tanzania Sports
Mabingwa wa EPL 2019/20

Bayern Munich ni mabingwa wa Bundesliga, Ujerumani. Liverpool ni mabingwa wa Premier League, England. Real Madrid ni mabingwa wa La Liga, Hispania. PSG ni wababe wa Ligue 1, Ufaransa. Juventus wanaelekea kuwa watemi wa Serie kule Italia. Simba ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania.

Baadhi ya mabingwa hawajafanya sherehe. Wamepewe makombe katika mazingira ya ukimya. Hakuna shamra shamra za mashabiki. Wachezaji wamejitahidi kurekodiwa picha za video au matangazo kurushwa moja moja kwa moja kutoka viwanjani, lakini wakiwa na ukiwa sana. Ni ukiwa wa viwanja vitupu bila mashakabiki. Ubingwa wa kimya kimya umewaudhi wachezaji lakini hawana namna nyingine.

KUKATWA MISHAHARA

Utajiri wa baadhi ya wamiliki wa Vilabu vya EPL

Malumbano kati ya wachezaji wa Barcelona na viongozi wao ni mfano halisi. Wachezaji walikuwa na hasira ya kukatwa mishahara yao. Arturo Vidal ni miongoni mwa wachezaji walioweka wazi misimamo ya kutokatwa mishara.

Real Madrid nayo ilikata mishahara ya wachezaji wake kwa asilimia 30. Hivyo wachezaji wakaambulia asilimia 70 ya mishahara yao. hata kama hawawezi kusema hadharani lakini katika mazingira ya kawaida kabisa hilo linawaudhi.

Mbaya zaidi Rais wa Real Madrid, Florentino Perez alibainisha kuwa upo uwezekano wa kutosajili wachezaji wengine au wakilazimika kusajili wanatakiwa kuuza wachezaji ili kupata fedha kiasi cha pauni milioni 300 na ushee. Liverpool ilitangaza kuyumba kimapato kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Korona. Wachezaji wamekatwa mishahara.

SOKO LA WACHEZAJI KUDODA

Thamani ya baadhi ya wachezaji, imeshuka kufuatia CORONA

Ukweli ni kwamba dili za mauzo ya wachezaji haziwezi kuwa kama ilivyozoeleka. Uchumi wa vilabu umeyumba. Mawakala hawafanya biashara nzuri msimu wa 2020/2021. Dili za biashara zimepungua. Wataalamu wa uchumi wanasema inawezekana miaka miwili ikasumbua soko la uuzaji na ununuzi wa wachezjai. Bei ya wachezaji sokoni zimebadilika.

Hakuna timu iliyo tayari kumwaga fedha sokoni. Kwahiyo hakuna wachezaji watakaolipwa fedha nyingi katika mikataba mipya katika usajili au kwa wanaoendelea.

Kipindi hiki wachumi wanafafanua madhara ya Korona, huku timu zikibana matumizi na matanuzi sokoni, hilo linawaathiri wachezaji moja kwa moja. Hapo lazima wauchukie ugonjwa wa Korona. Uginjwa ambao unapeperusha dili za kuchota fedha.

TUZO ZIMEYEYUKA

Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa tuzo mwaka 1956, sasa Korona imesababisha kufutwa kwa sherehe za Ballon d’Or mwaka huu. Waandaaji wa tuzo hizo wa jarida la France Football wametangaza wiki hii kuwa itakuwa vigumu kuandaa tuzo hizo zenye heshima kubwa ulimwenguni kwa sababu msimu huu umeathiriwa na mlipuko wa ugonjwa Korona.

Ballon d’Or

Tuzo hiyo ambayo inashikiliwa na Lionel Messi kwa sasa, bila shaka imeua dili nyingi za wachezaji. Kwanza biashara zimeharibika kwa waandaaji, kisha wachezaji wanalikosa jumuiko lao la kila mwaka ambalo wanakutanishwa na shere za tuzo hizo.

Hii ina maana mastaa waliofanya vizuri msimu huu hawana chao kwenye tuzo hizo. Mastaa kama Robert Lewandowski, Sergio Ramos, Lionel Messi, Kevin De Bruyne, Cristiano Ronaldo, Virgil Van Dijk, Karim Benzema, Sadio Mane, Erling Haaland na Bruno Fernandes walitegemewa kutwa kama miongoni mwa wanaowania tuzo hizo. Lakini Korona imefuta matamanio yao.

LIKIZO YA KULENGA NA MANATI

Wachezaji maarufu wakiwa mapumzikoni

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amegoma kuwapa likizo wachezaji wake. Pep ameamua kuchukua hatua hiyo kama njia ya kuwaandaa wachezaji wake dhidi ya Real Madrid katika mchezo wa raundi ya 16 mtoano wa UEFA. Mechi za UEFA zitachezwa mwanzoni mwa mwezi Agosti, ikiwa na maana pia watakuwa na muda mfupi wa kuajindaa kwa msimu mpya 2020/2021.

Ligi Kuu England inatarajiwa kuanza Spetemba 12 mwaka huu. Hivyo timu zinazoshiriki UEFA zitakuwa na muda mfupi mno wa kuandaa wachezaji wao. Kwa maana hiyo likizo zao zitakuwa zimeyeushwa na ugonjwa wa Korona.

KUTEMWA

Ligi ziliposimamishwa sababu ya ugonjwa corona kuna timu ziliamua kuwatema baadhi ya wachezaji. Timu hizo ziliwatema wachezaji hao kwa lengo la kuweka mizani ya vitabu vya fedha. Ikiwa na maana korona ilileta balaa kwenye mapato ya timu. Jambo hilo linawaweka katika wakayti mgumu wachezaji na bila shaka watakuwa wanaudhika sana kila wanapokumbuka ugonjwa wa Korona.

MAGOLI MATAMU

Zipo timu zimefunga mabao matamu sana. Chukulia namna Arsenal walivyoandaa moja ya bao lao dhidi ya Manchester City. Zilipigwa pasi kuanzia langoni mwao, kimahesabu taratibu kwenda kulia, kisha kushoto na katikati, halafu zikaenda winga wa kulia na baadaye kushoto kisha likapachikwa bao maridadi kabisa.

Lilikuwa bao linalostahili yowe kubwa la mashabiki. Lakini uwanja ulikuwa mtupu. Mashabiki wamezuiwa sababu ya Korona. Kimsingi mabao matamu kama hayo yananoga zaidi pale mchezaji anaposhuhudia shangwe kutoka kwa mashabiki wakiimba na kulitaja jina lake.

Hakika ni suala la burudani kubwa sana, lakini limeishia kuwaudhi wachezaji. Wanapachika mabao matamu lakini mashabiki hamna uwanjani. Inaudhi mno, lakini korona ndiyo imetubana kila kona ya dunia. Shangwe zinaishia kwenye makochi nyumbani.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version