Katika mchezo wowote ule duniani ili ukue ni lazima uwe na mashindano ambayo yapo katika mifumo ya ligi. Ligi yoyote lazima iwe na mchanganyiko wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani. Mchezo wa mpira wa kikapu nchini Marekani una ligi maarufu iitwayo NBA katika kujikuza ligi hiyo imekuwa na mbinu ya kutafuta hadhira ya kimataifa hususani katika nchi za bara la Asia waliamua kutengeneza mazingira ya kusajiliwa wachezaji wa kutoka katika bara hilo na hapo ndipo alisajiliwa mchezaji kutoka nchini China aitwaye Yao Ming. Yao Ming alisaidia kwa kiwango kikubwa kuutangaza mchezo huo katika bara hilo na hatimaye kuhamasisha vijana wengi sana kuupenda mchezo huo na hivyo ikapelekea NBA ikapenya kiurahisi katika bara hilo na kupata mashabiki wengi. Hata pale ambapo alisajiliwa mtanzania Hashim Thabeet kucheza katika ligi ya NBA nako kulipelekea watanzania wengi sana kufuatilia NBA.
England katika mbinu ya kutangaza ligi yake ya soka iliruhusu kusajiliwa wachezaji wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali ili wacheze katika ligi hiyo. Ilitumia mbinu za ushawishi za mikataba mizuri ya kipesa kuwashawishi wachezaji wazuri wa mataifa ya nje kucheza katika ligi hiyo. Walipofanikiwa katika hilo walijitanua katika masuala ya haki za kurusha matangazo ya runinga (Broadcasting Rights) ili kuhakikisha ligi yao inaonekana katika ligi mbalimbali duniani hususani nchi za dunia ya tatu za bara la Afrika na Asia. Kusajiliwa kwa wachezaji wengi wa kiafrika hususani kutoka nchi za Afrika magharibi kulisaidia ligi hiyo kupata mashabiki wengi katika nchi hizo. Mwanzoni mwa miaka ya 2000 kulikuwa na timu kama Portsmouth ambazo zilikuwa zina wachezaji wengi sana ambao walitoka afrika magharibi na hii ilisaidia kuongeza mashabiki wa timu hiyo na wafuatiliaji wa ligi hiyo katika nchi hiyo. Klabu ya Aston Villa ilipata wafuatliaji wengi na mashabiki wengi pale iliposajili mchezaji wa kimataifa kutoka Tanzania Mbwana Samatta na hata wengi wa mashabiki wao walianza kutoa maoni yao katika kurasa za kijamii za klabu hiyo zilizopo katika mitandao ya kijamii.
Ligi ya England katika kutengeneza mashabiki katika bara la Asia ilinufaika sana na usajili wa wachezaji kutoka katika nchi ya Uchina Lie Tie Na Sun Jihai waliposajiliwa kucheza katika ligi kuu ya soka ya nchini England mnamo mwaka 2002 inakadiriwa Zaidi ya watu milioni 700 kupitia kuangalia mubashara walifuatilia kwa ukaribu mechi zao za awali ambazo timu zao zilikuwa zinacheza. Lie Tie alisajiliwa Everton na Sun Jihai alisajiliwa Manchester City. Uangaliaji na ufuatiliaji wa ligi ya England katika bara la Asia uliongezeka sana katika kipindi hicho.
Ligi ya Italia halikadhalika nayo ilinufaika sana na ufuatiliaji wa watazamaji na mashabiki wa soka kutoka katika bara la Asia pale mnamo mwaka 1997 pale kiungo machachari wa kutoka japan Hidetoshi Nakata aliposajiliwa kwenda kucheza katika timu ya Peruggia ya nchini humo hakika ulikuwa ni usajili ambao ulitikisa kwa kipindi hicho kwani Nakata alikuwa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na kuna mda ilifiki mpaka akapachikwa jina la utani la “David Beckham wa Asia”. Hakika Nakata alitangaza sana ligi ya italia. Ligi hiyo ilizidi kupata mashabiki lakini iliboronga pale baada ya mashindano ya kombe la Dunia la mwaka 2002 yaliyofanyika nchini Korea na Japan ambapo timu ya soka ya taifa la Italia ilitolewa na korea ambapo mchezaji An Jung Hwan aliitoa timu ya Italia katika hatua ya mtoano ambapo wakati huo naye alikuwa anacheza katika ligi ya Italia.
Ligi ya Italia halikadhalika katika miaka ya 1990 ilikuwa na wafuatiliaji wengi sana kutoka bara la Amerika kwani mastaa wengi wa soka wa wakati huo walikuwa wanatokea katika bara hilo kama vile Gabriel Batistuta, Alvaro Recoba, Juan Sebastian Veron, Marcelo Salas, Ronaldo de Lima, Ivan Zamorano na wengineo wengi kuliifanya ligi hii iwe na mashabiki wengi sana katika bara hilo.
Tukirudi katika ligi ya soka ya Tanzania tokea ipate udhamini wa kurushwa matangazo yake mubashara na kampuni ya Azam imejikuta ina wafuatiliaji wengi sana katika nchi jirani za afrika mashariki na uwekezaji huu umesaidia kuvuta wachezaji wengi kutoka maeneo mbalimbali ya bara la afrika kuja kucheza nchini Tanzania. Tumeona kwa sasa kuna wachezaji kama vile Djigui Diarra, Clatous Chama Aziz Ki, Henock Inonga, ambao walicheza vizuri katika mashindano ya soka ya AFCON na walitangaza ligi ya soka ya Tanzania kwani walitangazika kwamba wanacheza ligi hii. Kuwepo kwa wachezaji wengi wa kimataifa kunakuza ligi ya Tanzania kwani kunaleta ushindani ambao huko nyuma haukuwepo. Changamoto ambayo baadhi ya wachambuzi huileta kwamba wachezaji wengi wan je wakiwepo hufanya wachezaji wa ndani wasionekane si sahihi kwani ushindani unaoletwa na wagenu huwafanya wenyeji wajitume Zaidi na Zaidi. Nchi za Italia na Ujerumani ambazo tokea ianze miaka ya 2000 zimekuwa zinaweka mazingira mazuri Zaidi kwa wachezaji wazawa kuliko kuwa na wageni kumezifanya ligi hiyo idorore na kutotanuka vizuri kibiashara katika mabara nje ya Ulaya.
Uwepo wa wachezaji wengi wa nje uzifanye klabu zianze kutengeneza akademi zake za soka kwa ajili ya kuibua vipaji vya wachezaji ambao ni wachanga kwani ligi yetu sasa inafuatiliwa na wafuatliaji wengi kutoka nje ya nchi na hivyo kutengeneza mazingira mazuri ya fursa ya wachezaji hao kuja kusajiliwa katika vilabu vikubwa barani afrika. Pili vilabu vianze kujtanua kibiashara katika nchi ambazo nje ya Tanzania kwani nembo zao za biashara zimeanza kufahamika na kutengeneza mashabiki na wafuasi katika mataifa hayo. Waanze kupelekea biadhaa zenye nembo zao kwani zitaanza kuuzika kwa mashabiki wao ambao wako nje ya nchi.