Menu
in , , ,

Wachezaji wa kigeni kupunguzwa

*FA waja na mfumo mpya kuibeba England

*Washabiki kumwondoa Pardew Newcastle

*Everton matata Europa, Spurs dorodoro

Chama cha Soka cha England (FA) kimepanga kubadili mpango wa usajili ili kupunguza idadi ya wachezaji wasiotoka Umoja wa Ulaya (EU) hadi asilimia 50 katika soka ya England.

Mwenyekiti wa FA, Greg Dyke amesema kwamba hatua hiyo inachukuliwa kwa ajili ya kujaribu kuponya soka ya Timu ya Taifa ya England (Three Lions).

Dyke anadai kwamba mfumo wa usajili unaoruhusu wachezaji kumiminika kwenye klabu za England kutoka ng’ambo ni vurugu tupu na kwamba mipango ikienda vizuri mwisho itakuwa tayari msimu wa 2015/16.

Hatua hii inakuja baada ya klabu nyingi za Ligi Kuu ya England (EPL) kusajili wachezaji wengi kutoka nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kutoka Amerika, Afrika na pia nchi zilizo nje ya EU. Hata hivyo, haijulikani kama hatua hiyo itasaidia sana soka ya Three Lions.

Mwenyekiti huyo alidai kwamba asilimia nane ya wachezaji wanaoingia England kutoka nje ya EU huomba wenyewe kuja, ambapo hutuma video za jinsi wanavyocheza huko, halafu kocha anaipeleka kwa kamati ya ufundi kisha wanaridhika na kumwita kuingia England.

FA wanataka kuondokana na mambo kama hayo, ambapo timu ndizo zinatakiwa kuchukua wachezaji kwa kuzingatia vigezo. Hadi mwisho wa msimu uliopita kulikuwa na wachezaji 122 wanaotoka nje ya EU walioingia nchini England tangu 2009.

ALAN PARDEW KUTIMULIWA NEWCASTLE?

Washabiki wa Newcastle wamemchoka kocha wao, Alan Pardew na sasa wamedhamiria kumtimua kwa kutia shinikizo kwa uongozi wa klabu na mmiliki, Mike Ashley.

Washabiki hao wamechapisha stika 30,000 zenye picha yake na zimeandikwa ‘SACKPARDEW’ ambazo zitasambazwa na kutumiwa wakati wa mechi yao ijayo kama hatakuwa ameshafukuzwa.

Newcastle wameanza vibaya EPL lakini Pardew anasema kwamba anaungwa mkono na uongozi na kuwa kitendo cha washabiki hao ni kuchochea vurugu na kitawaathiri wachezaji. Pardew (53) ndiye kocha wa pili kwa kuwa kwa muda mrefu zaidi kwenye klabu moja, akiwa amedumu hapo St James’ Park kwa miaka mitatu na ushee, kwani alianza kazi Desemba 2010.

Arsene Wenger ndiye anaongoza kukaa kwa muda mrefu kwenye klabu moja, kwani yupo Arsenal tangu 1996, ikiwa ni miaka 18.

“Hali hii inawaathiri sana wachezaji,” anasema Pardew ambaye pigo lake lililopita lilikuwa kufungwa na Southampton 4-0 wakati inajulikana wazi kwamba Saints wamechukuliwa wachezaji wake nyota kiangazi hiki, huku Newcastle wakiwa na wachezaji waliogharimu fedha nyingi.

Hata hivyo, Pardew alisaini mkataba mpya wa muda mrefu hivi karibuni, hivyo akifukuzwa kazi itabidi alipwe fidia kubwa. Katika mechi iliyopita washabiki walibeba mabango ya kutaka Pardew afukuzwe.

EVERTON WANG’ARA EUROPA

Everton wameingia kwenye ramani ya Ulaya kwa kishindo, kwa kuwafunga Wolfsburg ya Ujerumani 4-1 katika michuano ya Ligi ya Europa katika dimba la Goodison Park.

Toffees wameingia kwenye mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu 2010 na walidhibiti mechi hiyo vilivyo chini ya kocha Roberto Martinez.

Toffees walifunga mabao yao kupitia kwa Ricardo Rodriguez aliyejifunga na Seamus Coleman kupiga la pili kabla ya Leighton Baines kufunga penati kipindi cha pili, Kevin Mirallas akatupia la nne kabla ya Rodriguez kufuta kosa lake kwa kufunga kwa mpira wa adhabu ndogo

Timu nyingine katika kundi hilo ni Lille ya Ufaransa na FK Krasnodar ya Urusi. Katika mechi nyingine ya Kombe la Europa, Tottenham Hotspur walikwenda suluhu na Partizan Belgrade jijini Belgrade, Serbia.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version