GUMZO kubwa nyumbani Tanzania kwa sasa ni hatua ya Bodi ya Ithibati ya Uandishi wa Habari kuendeleza kampeni ya kuhamasisha waandishi wa fani hiyo kujisajili ili wapate vitambulisho rasmi. Vitambulisho hivi vinamtaka mwandishi wa habari kuwasilisha baraua ya mwajiri / ajira yake kwenye chombo husika ili kuruhusiwa kufanya kazi hiyo.
Baadhi ya watangazaji maarufu nchini Tanzania wamelazimika kujiondoa au kuondolewa na Bodi ya Ithibati au vyombo husika vya habari kwa kile kinachoitwa kukosa vigezo husika vya kufanya kazi ya uandishi wa habari. Zaidi ya hayo, wengi wao ambao wamedumu kwenye fani hiyo kwa kipindi zaidi ya miaka 20 nao wametakiwa kurudi chuoni kusoma ili wawe na vigezo.
Utaratibu huo unaelezwa kuwa kwenye Sheria ya Uandishi wa Habari ya mwaka 2016, ambapo iliweka kigezo ili kufanya kazi ya uandishi wa habari, mwandishi anatakiwa kuwa na elimu si chini ya Stashahada / Diploma. Hatua hiyo imesababisha mjadala wa pande mbili wanaopinga na kukubaliana nao.
Hata hivyo kupitia makala haya napenda kueleza mambo machache ambayo yanahitimisha kuwa vyeti sio kila kitu katika fani ya uandishi wa habari na utangazaji mbele ya talanta au kipaji. Unakutana na vyeti, lakini hakuna kipaji chochote na ufanisi ni hafifu.
Ingawa sote tunatambua kuwa sifa rasmi za uandishi wa habari zinaweza kusaidia kwenye fani husika. Hata hivyo inawezekana kuwa mtu yeyote kuwa mtangazaji bila sifa rasmi za kielimu. Watu wengi wamejenga majina na heshima kubwa katika utangazaji wakiwa wamechota uzoefu na ujuzi uliooboreshwa kupitia njia mbadala. Hawa ni wale ambao wamepata mafunzo wakiwa kazini (indoor training) na kwingineko kazini. Kabla ya kuendelea nitatoa mifano michache kuthibitisha hoja yangu kwa watangazaji ambao wamefanikiwa kupitia njia mbadala.
Uzoefu ni kitu muhimu
Upo uwezekano kwa watu wengi kuupata uzoefu wa vitendo kupitia kujitolea, mafunzo kazini au majukumu ya ngazi za awali kama vile msaidizi wa uzalishaji au mwendeshaji wa kipindi kunaweza kutoa mchango muhimu wa kazini, hadi kufikia umahiri. Hawa ni baadhi ya watu ambao walipenda utangazaji lakini walipitia njia mbadala si rasmi ya vyeti inayopigiwa kampeni kwa sasa.
Freelance:-
Huu ni aina ya Uandishi wa habari wa kujitegemea ambao unaweza kuwa njia nzuri ya kujenga na kupata kutambuliwa kwa kazi yako. Vyombo vya habari mbalimbali duniani vinafanya kazi na watu wenye utaalamu na uandishi kwa sababu ya ufanisi na talanta zao walizonazo. Baadhi ya waandishi kutoka barani Afrika wanafanya kazi na vyombo vya habari vya hapa Ulaya wakiwa na sifa mbadala kwa umahiri, japokuwa wapo wengine wenye sifa rasmi zinazohitajika na Bodi ya Ithibati. Kwahiyo uandishi wa habari wa kujitegemea hauhitaji barua ya mwajiri kwa sababu mwandishi huyu hajaajiriwa na chombo chochote lakini kwa heshima, weledi, na uwezo mkubwa wa kazi yake anafanya kazi vizuri inayovutia wamiliki wa vyombo vya nje. Bodi Ithibati Tanzania huenda haijazingatia kukua na kupanuka kwa uandishi wa kujitegemea ndio maana wanapigania barua za waajiri kana kwamba kila kitu kinatokana na kuajiriwa.
Mipango ya mafunzo na mafunzo yenyewe;
Kampuni nyingi za vyombo vya habari hutoa mafunzo au mipango ya wafunzaji, ambayo inaunganisha mafunzo ya kazini na sifa nyinginezo. Sifa hizo ni pale ambapo mwandishi anakuwa na uwezo wa uandishi lakini hana sifa rasmi, hivyo vyombo vya habari huweka mipango ya mafunzo na kutoa mafunzo kwa wahusika hadi kuwa wabobezi.
Kozi za mitandaoni na kujisomea;-
Mabadiliko ya Dunia kupitia teknolojia hayajaiacha salama fani ya uandishi wa habari. Uandishi wa habari ni miongoni mwa fani ambazo zinakumbana na wimbi hilo hivyo mifumo ya utendaji wa kazi hii imetanuka zaidi kuliko awali. Mathalani mifumo kama vile ‘Future Learn’ hutoa kozi mbalimbali za uandishi wa habari, na kujifunza kwa kujielekeza kunaweza kusaidia kukuza ujuzi wa mtu unaohitajika bila kutegemea sifa rasmi kama za Bodi ya Ithibati. Hivyo basi kozi hizo zimejenga fursa za ndani;- Uandishi wa habari kupitia kuunda blogu, tovuti au uwepo wa mitandao ya kijamii umechangia kuonesha ujuzi wa kuandika na kuripoti masuala muhimu kwa weledi.
Vyombo vya habari vya Jamii;
Teknolojia imeleta wimbi la uandishi wa habari wa raia au jamii (Citizen Journalism) ambapo zimeibuka redio za mitandaoni, blogu, tovuti na YouTube ambako watu mbalimbali hutoa ujuzi wao wa habari kwa watu wanaopenda kuwa wanahabari.
Mifumo ya kujitolea katika vituo vya redio vya jamii au Televisheni kunaweza kutoa uzoefu muhimu na fursa za nafasi mbalimbali kwa watu. Mabadiliko haya yanaumba mafunzo mbadala yanayomwivisha mtu kuwa mfano mtangazaji.
Mitandao;
Hii ni nyenzo nyingine ambayo inampa mtu fursa ya kuhudhuria hafla za tasnia husika na kuungana na wataalamu kisha ikawa njia ya kufungua milango kwa fursa.
Ujuzi muhimu na utafiti katika kukagua ukweli;
Ujuzi thabiti wa uandishi na mawasiliano ni muhimu kwa uandishi wa habari kama utangazaji na uchapishaji. Utafiti na uwezo wa kukagua ukweli ni vitu muhimu sana katika kuwasilisha habari sahihi na kwa weledi. Hii maana yake inamfanya mwandishi wa habari yeyote (bila kujali vigezo rasmi au mbadala) anaweza kuzingatia kwa undani kama njia muhimu ya kuhakikisha maudhui yanakuwa sahihi na yenye ubora wa hali ya juu kwenda kwa watazamaji,wasomaji au walaji na wadau husika.
Kubadilika na uthabiti;
Kwa vile suala la teknolojia limeleta mapinduzi makubwa basi, hali ya kubadilika kwa uandishi wa habari na utangazaji nako ni miongoni mwa mambo yaliyokutana na nayo.
Kwa maana hiyo mwandishi wa habari au mtu anayetaka kufanya kazi ya uandishi wa habari anatakiwa kuwa tayari kubadilika. Hii ni muhimu kwa uandishi wa habari unapowajibika kutoka zama moja kwenda nyingine.
Sifa ya elimu na mifano sahihi
Kimsingi, ingawa shahada ya uandishi wa habari inaweza kuwa yenye manufaa, lakini si njia pekee ya taaluma ya utangazaji. Kujenga msingi thabiti wa uzoefu wa vitendo, kukuza ujuzi unaofaa, na kujielekeza kwingineko kunakofaa kunaweza kusababisha mwandishi kuzalisha kazi yenye mafanikio katika utangazaji, bila kuwa na sifa rasmi zinazotajwa na Bodi ya Ithibati.
Huku Uingereza, ingawa sifa rasmi za uandishi wa habari ni za kawaida na mara nyingi hupendelewa na mwajiri, hakuna masharti makubwa wala magumu kwa mtangazaji. Sheria inaeleza kuwa mtu yeyote anayefanya kazi ya uandishi wa habari-iwe kama mwandishi, mtangazaji, mtayarishaji vipindi, mpigapicha au mhariri wa maudhui-awe na angalau Stashahada ya Uandishi wa Habari (Journalism) au mawasiliano ya Umma (Mass Communications) ili kustahili kupata ithibati.
Wanahabari kadhaa mashuhuri duniani wametokea kupata mafanikio bila hata ya kuwa na sifa za juu za kisomi kwenye kada ya uandishi na utangazaji habari. Mifano ni Larry King pamoja na Oprah Wifrey, ambaye alijenga himaya yake ya vyombo vya habari kutoka kuwa mtangazaji wa habari wa ndani ya nchi (local) hadi nguli wa vyombo vya habari duniani.
Yupo pia Arianna Huffington aliyeanzisha Huffington Post bila ya kuwa na hata shahada ya uandishi wa habari. Zaidi ya hayo, watu binafsi kama Tyler Perry, gwiji wa vyombo vya habari aliyejitengeneza mwenyewe na Ryan Seacrest, mhusika maarufu wa matangazo ya Televisheni, pia wamepata mafanikio bila sifa rasmi zinazoonekana kuelezwa nyumbani Tanzania na Bodi ya Ithibati ili waandishi husika waweze kufanya kazi kwenye vyombo vya habari.
A freelance journalist is a self-employed writer who works on a contract or assignment basis for various media outlets
Mimi;-
Ni kweli sijasomea uandishi wa habari, lakini kwenye fani yangu ya michezo nina sifa za kiwango cha MSc katika fani ya michezo, je unataka kunizuia kuandika au kutangaza hadi niwe na sifa za uandishi wa habari? Sidhani kama nitakubaliana na hilo.

Je unataka tuache kumsoma au kumsiliza Dr Hildebrand Shayo, msomi na mbobezi wa masuala ya fedha na uchumi kwa kuwa tu, si muandishi wa habari?
Ninatoa mifano mingine hapa ambapo kuna watu mashuhuri walitoa mchango mkubwa kwa tasnia ya habari bila hizo sifa rasmi kwa vyombo vya habari.
Opray Winfrey;- alianza kama mtangazaji wa habari nchini na akajenga himaya ya vyombo vyahabari ikijumuisha mtandao wa Televisheni, jarida na kampuni ya utayarishaji wa maudhui.
Arianna Huffington;- alianzisha Huffington Post, tovuti kuu ya habari na maoni.
Tyler Perry;- bingwa wa vyombo vya habari aliyejitengeneza ambaye alianza na michezo ya kuigiza ya jukwaani na kubadilika hadi kubobea katika utayarishaji wa filamu na Televisheni.
Ryan Seacrest: Mtangazaji na mtayarishaji maarufu wa televisheni.
Cona O’Brien: Mcheshi na mtangazaji wa Televisheni aliyefanikiwa ambaye alianza kazi yake ya uandishi wa vichekesho (kama Masoud Kipanya aliyekuwa Clouds Media).
Watu hawa wanaonesha kwamba ingawa sifa zinawasaidia, sifa hizo sio njia pekee ya mafanikio katika tasnia ya habari. Mafanikio yanaweza kupatikana kupitia talanta au kipaji, bidii na uelewa mzuri wa masuala mazima ya Tasnia ya Habari.
Je, Daktari bingwa utamzuia kutoa elimu ya bure kupitia TikTok au YouTube? Wakati ana sifa za taalama yake? Ukweli ni kwamba wapo waandishi na watangazaji wazuri wa redio na Televisheni na baadhi ambao hadi sasa wanafanya vyema kwenye vyombo vya husika.
Baadhi ya vyombo hivyo ni vya Kiingereza ambao walianza uandishi mara baada ya kuhitimu sekondari, wakaanza kazi kabla hata ya kuingia vyuo vya uandishi. Walikuja kujiendeleza baadaye kimasomo wakiwa kazini moja kwa moja au njia ya vyuo huria vilivyo ndani na nje ya nchi.
Ni maoni yangu kwamba kuwa mwandishi au mtangazaji bora si lazima kuwa na wasomi wakubwa; wapo wasomi wenye vyeti vikubwa, lakini kazini hakuna ufanisi, na ushahidi wa hayo yote upo wazi kabisa. Je ni wachambuzi au watangazaji wangapi kwenye vyombo vya habari mbalimbali hapa Uingereza wenye cheti cha uandishi? Lakini wana wafuasi mamilioni kwenye social media zao? Ni kwa sababu weledi wao umejionesha dhahiri na wamejenga heshima ya uandishi wa habari na utangazaji pasipo kupitia mifumo rasmi au sifa rasmi kama inavyoelezwa nyumbani Tanzania.
Ni wajibu wa Bodi ya Ithibati kuvuka mipaka ya kikanuni na sheria kutambua kuwa si kila mtangazaji anahitaji sifa rasmi au mwandishi wa kujitegemea atawasilisha barua za waajiri. Tujifunze kuwa vyeti si kila kitu katika uandishi wa habari badala yake ni talanta ya mtu huyo ndiyo inayompa nafasi ya kuheshimika na kujenga jina bora la kitaaluma huku akipewa mafunzo yatokanayo.