Katika ardhi ya Gongo la Mboto jijini Dar es salaam kuna uwekezaji mkubwa wa kielimu umefanyika. Uwekezaji huo ni uwekezaji wa chuo kikuu cha kimataifa cha Kampala tawi la Tanzania. Wawekezaji hao wameweka majengo ya kisasa ambayo ni ya kiwango cha kimataifa na wamewekeza sana katika masomo ya afya za wanadamu (Health Sciences) ambapo kunatolewa kozi za udaktari wa binadamu, upasuaji, ufamasia na utaalamu wa maabara. Wawekezaji hao wamejenga maabara za kisasa kuhakikisha kwamba wanafunzi wa masomo hayo wanakuwa ni wataalamu wa uhakika na wenye uweledi wa hali ya juu kwa kuwafundisha masomo ya vitendo ya hali ya juu.
Chuo hiko kwa sasa hakivumi tu katika medani za elimu peke yake bali kinavuma pia katika medani zinginezo zikiwemo michezo. Katika michezo wawekezaji wa chuo hiko wamejenga viwanja vya kisasa vya kucheza michezo ya Basketball, Volleyball pamoja na Netball. Kwenye mchezo wa Volleyball kuna viwanha viwili vya mchezo huo. Uwekezaji ambao umefanywa na chuo hiko umekifanya chuo hiko kifanye vizuri katika mashindano ya michezo ya vyuo vikuu barani Afrika.
Chama cha mchezo wa volleyball mkoa wa Dar es salaam kwa mwaka huu kimekuwa kinaendesha mashindano ya Volleyball kwa mkoa wa Dar es salaam katika viwanja vya chuo kikuu cha kimataifa cha Kampala. Mashindano hayo yamejumuisha vilabu mbalimbali vya mchezo huo ambavyo vinapatikana katika mkoa wa Dar es salaam. Mashindano hayo yamekuwa ni ya timu za wanaume na wanawake. Timu ambazo zinashiriki mashindano hayo ni kama vile: KIUT, BANDARI, NGOME, MAGEREZA na nyinginezo. Mechi za mashindano hayo zimekuwa zinachezwa kila wikiendi.
Mashindano hayo ya ligi ya DAREVA yamekuwa yanachezwa kwa siku nzima hususani katika siku ya Jumamosi. Vilabu ambavyo hushiriki mashindano hayo vimekuwa vinajitahidi kushiriki huku vikienda na mashabiki wake na hivyo kutengeneza mandhari nzuri ambayo hufanya eneo hilo lionekane limefurika wapenzi wa mchezo huo kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo. Mashindano hayo yameamsha ari Fulani ya ushabiki wa mchezo huo katika ngazi ya juu.
Volleyball ni mojawapo ya michezo kongwe nchini Tanzania. Katika miaka ya nyuma mchezo huo ulikuwa una mashabiki wengi sana na mashindano yake yalikuwa yanakuwa yana hamasa kubwa sana kutokana na wingi wa mashabiki. Mchezo huu unachezwa kuanzia ngazi za shule ya msingi, sekondari mpaka chuo kikuu na unachezwa uraiani, taasisi za umma hadi kwenye majeshi. Kwa kiujumla ni mojawapo ya michezo ambayo ina hazina ya wachezaji wengi sana nchini Tanzania. Ukitembelea shule nyingi za msingi mpaka sekondari utakuta viwanja vya mchezo huo ambavyo vilitengwa kwa miaka mingi sana. Kwa kiwango kikubwa mchezo huu umekuwa unachezwa sana katika taasisi za umma na wala sio binafsi kwa kusema hivyo chuo cha Kampala nchini Tanzania kinaingia katika historia kuwa mojawapo ya taasisi binafsi nchini Tanzania ambao kimeamua kuubeba huu mchezo.
Kuubeba mchezo kama Volleyball ni jambo ambalo lahitaji umakini mkubwa kwani kama taasisi ikiwa haijajipanga vizuri inaweza ikaachana nao kwa kuwa mchezo huu mrejesho wake ndani ya nchi ya Tanzania unaweza usiwe mkubwa sana kama ilivyokwenye Soka ama Ndondi. Mchezo huu ukitaka ushughulike nao inawezekana ukatumia rasilimali zako kwa kiwango kikubwa bila ya kupata udhamini kutoka katika vyanzo vya nje na hili nyakati nyingine huleta mgongano katika taasisi kwani kuna baadhi ya watu ndani ya taasisi wanaweza kuona kwamba zinatumika gharama katika taasisi ambazo hazina tija kubwa kiuchumi hususani katika kukibidhaisha taasisi husika ambapo kwa muktadha huo ni chuo.
Uongozi wa chuo ili ufanye vizuri katika michezo unatakiwa uwe na taasisi imara hususani katika kipengele cha rasilimali watu. Inatakiwa iwe na idara ya michezo ambayo ina watu wenye ueweledi wa hali ya juu sana katika suala la kubidhaisha michezo yaani sio tu wawe na wajumbe wa kamati hiyo ambao wana taaluma ya michezo ila wawe na wafanyakazi katika idara hiyo ambao wanajua masuala ya kubidhaisha michezo na hatimaye kuvutia wadhamini na wawekezaji katika mchezo husika. Wanatakiwa wawe na wafanyakazi katika idara hiyo ambao wanajua suala la diplomasia katika michezo ambao watakuwa hodari katika kujenga mahusiano na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha kwamba program za michezo hapo ni endelevu. Wanatakiwa pia kuwa na watendaji ambao wanajua namna ya kutengeneza hamasa za kimichezo miongoni mwa mashabiki ambazo zitawafanya wanafunzi na wafanyakazi mbalimbali kujumuika kwa wingi kwenda kushangilia vilabu vya chuo chao kushiriki mechi hizo za vilabu vya chuo.
Mafanikio katika michezo ni suala ambalo linahitaji viongozi wenye dhana ya jumuishi yaani kuwaunganisha wadau mbalimbali ili kuleta nguvu katika michezo kwa hiyo viongozi wa michezo katika chuo cha kampala nchini Tanzania wameanza vizuri na mchezo wa Volleyball lakini wanatakiwa washirikiane na viongozi wa michezo mingine iliyopo hapo chuoni na bila y a hivyo yawekana wakaweka hata rehani mafanikio ambayo wameyapata katika mchezo huo kama waking’ang’ania kuubeba mchezo huo peke yake na sio kushirikisha michezo mingine.