Menu
in , , , ,

Viwanja vyetu vitakuwa tayari kwa AFCON 2O27?

Tanzania Sports

Benjamini Mkapa Sradium, Dar-Es-Salaa, Tanzania

MWISHONI mwa wiki iliyopita nilikuwa nazungumza na mwandishi na mtayarishaji wa vipindi vya Televisheni ya Taifa ya Kenya (KBC). Katika mazungumzo hayo tulijikita kwenye suala la maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ya mwaka 2027 ambapo Kenya, Tanzania na Uganda zimepewa jukumu la kuwa wenyeji.

Michuano hiyo yenye mvuto barani Afrika inaandaliwa na Mataifa matatu ya Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza ikiwa na maana ni fursa ya kutangaza kandanda,utalii na utamaduni wa ukanda huu pamoja na kuonesha ulimwengu jinsi mchezo wa soka unavyopendwa na wingi wa vipaji vilivyomo eneo hili. Kabla ya mashindano ya AFCON 2027 kuna yale yanayohusisha wachezaji wa ndani wa Afrika yaani CHAN. Mashindano ya CHAN pia yatafanyika kwenye nchi hizo tatu na kuwa fursa muhimu ya kujinadai katika ulimwengu wa kandanda.

Uchunguzi wa TANZANIASPORTS katika maandalizi ya mashindano makubwa barani Afrika na ya tatu duniani unaonesha kuwa changamoto ya Tanzania,Uganda na Kenya ni viwanja vitakavyotumika. Katika viwanja vya kandanda vinavyofaa kutumika katika mashindano hayo vipo vile ambavyo vinahitaji ukarabati mdogo na vingine ukarabati mkubwa.

Mathalani michezo mbalimbali ya Ligi Kuu nchini Kenya inaonesha viwanja vingi vina hali duni ya utunzaji. “Kenya hali ya viwanja bado si nzuri, juhudi zinahitajika kabla mashabiki hawajakata tamaa. Matumaini makubwa yapo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huko Tanzania, japo kuna uwanja mpya unaojengwa unaitwa Talanta Stadium, ila  sina uhakika kama utakuwa tayari kwa Afcon. Pia upo ukarabati wa uwanja wa Moi Kasarani na Nyayo Stadium, lakini hofu haijatuacha” alisema mwanahabari huyo.

Maoni ya mwanahabari huyo si pekee kwani idadi ya watu wenye kulitazama suala hilo kwa hofu ya utayari wa viwanja inazidi kuongezeka. Uwezekano wa kuwa tayari na viwanja wa mashindano hayo ni Benjamin Mkapa (Dar Es Salaam, kisha unaofuatia ni New Amaan Comlpex (Zanzibar), pamoja na viwanja vingine vidogo kama vile Azam Complex na KMC Stadium.

Kwa upande wa Uganda bado wanayo changamoto kwani hata baadhi za mechi za kufuzu mashindano ya Kimataifa walilazimika kucheza nje ya nchi mfano Misri. Hilo lina maana kuwa licha ya kuwa kwenye ukarabati bado Uganda haikuwa na kiwanja ambacho kinakidhi vigezo vya Shirikisho la soka CAF pamoja na lile la kimataifa, FIFA.

Mashindano ya AFCON ni sehemu ya kutangaza umahiri wan chi zinazoandaa kwa kuonesha namna miundombinu yake ilivyopangika na uwezo wa kuhudumia wageni. Taarifa za ujenzi wa uwanja mpya wa soka Jijini Arusha bado si zile zinazofurahisha kwani imesalia miaka miwili pekee kabla ya kuanza mashindano ya Afcon mwaka 2027. Katika shughuli za ujenzi ni wazi muda uliosalia ni mdogo ama unapaswa kujengwa kwa kasi mno ili kuwa tayari kwa mashindano.

TANZANIASPORTS inafahamu kuwa ipo Kamati ya ushirikiano kupitia Wizara za mambo ya nje kati ya Kenya, Uganda na Tanzania inayotakiwa kushughulia masuala ya maandalizi ya miundombinu ya mashindano ya Afcon mwaka 2027. ni wakati ambao viongozi wa kandanda na serikali kuona kuwa muda uliosalia ni mdogo na hakuna namna yoyote ya kulala usingizi au kulegalega kabla ya kupokonywa uenyeji wa fainali hizo.

Ni fainali ambazo zinatarajiwa kuacha urithi mkubwa kwenye kandanda ikiwa zitaandaliwa na nchi za Afrika Mashariki na zitaonesha mshikamano wa Mataifa yetu. Shime kwa viongozi wote wanapaswa kuchukua jukumu hili na kulitekeleza kwa nguvu na maarifa makubwa ili kuacha alama nzuri ya urithi katika mashindano. Ikumbukwe Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana mwaka 2019 lakini hayakupewa uzito mkubwa kiasi kwamba ikaonekana kama jambo la kawaida. Nchi zote zinapaswa kuamka na kuona mchezo wa soka ni mahali pa biashara na kukuza uchumi wan chi zao.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version