*Vilijengwa na nguvu ya watanzania wote bila kujali itikadi
SIJUI kama Jaji Joseph Warioba na Tume yake wamemaliza kukusanya maoni ya kutuwezesha Watanzania kuandika Katiba ya kwanza ya wananchi. Sijui pia kama haya yatakayoandikwa hapa hawakuyakusanya kwenye maoni waliyokusanya hadi sasa.
Ninapendekeza kwamba Katiba yetu iwe na kifungu kinachozuia, mtu yeyote, kikundi chochote cha watu kikiwemo chama cha siasa kudai rasmi au kwa maneno tu kumiliki mali yoyote inayohamishika (movable property) na isiyohamishika (immovable property) kama mali hiyo imetokana na fedha ya umma na si fedha pekee ya mtu huyo au kikundi hicho au imekuwepo kiasilia.
Kwa sababu Katiba ya nchi si kitu cha kulenga vitu vidogo vya kibinafsi vya leo na kesho tu, kifungu hiki siyo tu kitaizuia leo CCM kudai viwanja vya michezo vya umma kuwa mali yake wakati vilijengwa na umma wote bali pia utaizuia CHADEMA ikikamata dola kudai njia zote za mawasiliano ikiwemo viwanja vya ndege, reli, bandari, barabara na simu kuwa mali yake ambapo CUF nayo ikiingia madarakani isiseme kwamba vyuo vyote vya umma vya elimu ya juu ni vyake.
Kifungu hicho kitawazuia NCCR Mageuzi wakikamata dola kuja kudai vivutio vya utalii vyote kuwa mali yake. Leo tuna uwanja wa CCM Kirumba, hatutaki CHADEMA wakiwa ulingoni wakaja na Uwanja wa ndege wa CHADEMA wa Julius Nyerere au reli ya CHADEMA ya kati ya nchi. Hatutaki kuja kuwa na Chuo Kikuu cha CUF cha Kilimo cha Sokoine na wala hatutaki kuwa na Hifadhi ya NCCR Mageuzi ya Mlima Kilimanjaro au Mbuga ya Wanyama ya NCCR Mageuzi ya Serengeti.
Nani atawalaumu watakaofanya hivyo wakati huo, ikiwa leo hii CCM inaachiwa itambe na viwanja vya michezo vya umma kuanzia CCM Kirumba Mwanza mpaka CCM Gombani, Pemba. Kuanzia CCM Majimaji Songea mpaka uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga. Kwa sababu za msingi sana Katiba mpya isaidie kuinyang’anya CCM viwanja vya michezo vya umma inavyovimiliki kwa nguvu kutokana na kuwa chama tawala. Sababu ya muda mrefu ni hiyo iliyoelezwa ikizingatiwa kwamba si rahisi chama cha siasa kuongoza nchi milele.
Sababu ya muda mfupi ya hoja hii inazingatia zaidi uboreshwaji wa viwanja hivyo ili vilete tija nyingi ambazo baadhi yake zitaainishwa hapa chini. Kwa bahati mbaya sana CCM katika kujimilikisha viwanja vya michezo vya umma imezingatia sababu za kitanzania za ufahari tu na kutotafakari sababu za kiuchumi na za kijamii. Ukimuuliza Mtanzania umuhimu wa Shirikisho la Afrika Mashariki atakwambia kwamba sisi watu wa ukanda huu ni ndugu na ni vizuri tukishirikiana lakini ukimuuliza Mkenya kuhusu umuhimu wa Shirikisho hilo atakumbia ni kupanua wigo wa kufanya shughuli za kiuchumi.
Hivyo hivyo CCM inaona ufahari kumiliki viwanja vya michezo bila kujua kwamba kiuchumi viwanja hivyo ni miradi mikubwa ya kipato na ndiyo maana Arsenal ya Uingereza iliachana na uwanja mdogo wa Highbury na kujenga uwanja mkubwa wa Emirates hapo Ashburton Groove, London. Ndiyo maana Liverpool wako mbioni kuachana na Anfield na kuwa na uwanja mkubwa zaidi.
Hata ukitafakari kuhusu kiasi cha pesa ambacho uwanja wa Benjamin William Mkapa, unaoitwa uwanja wa Taifa, kimeingiza tangu uzinduliwe mpaka sasa, utaona kuwa viwanja vya michezo ni vitega uchumi zaidi ya vitu vya kifahari kama CCM inavyofanya.
Katiba mpya irudishe viwanja vya michezo kwa umma ambao ndiyo mmiliki halali kwa sababu CCM haiwezi na haitaki kufanya hivyo kwa manufaa ya umma.
Kuna njia mbili kubwa za kufanya viwanja hivyo viwe bora kwa kuinua michezo yetu na kutuinua kiuchumi mara vikiachwa na CCM ambayo ushauri kwake ni kujenga kiwanja chake kimoja tu. Njia ya kwanza ni kwa serikali kuunda Mamlaka ya Uendelezaji na Usimamizi wa viwanja vya michezo.
Kazi kubwa ya mamlaka hiyo itakayofanya kazi yake kwa kutumia ushauri wa kitaalam (consultancy) licha ya yenyewe kuundwa na watu waliobobea katika mipango ya ujenzi na uongozi wa viwanja vya michezo itakuwa kwanza, kuchambua nini vinahitajika kuboreshwa kwenye viwanja tofauti kuanzia sehemu za kuchezea (pitches) na sehemu za kufanyia michezo ya riadha mpaka majukwa ya watazamaji na vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na yote ya msingi kama taa za uwanjani ili viwanja vyote viwe na uwezo wa kuchezewa usiku.
Viwanja vikiboreshwa hivyo, tutakuwa na jeuri hata ya kuomba kuandaa mashindano ya fainali ya mataifa ya Afrika au hata yale ya wachezaji wanaocheza nyumbani tu. Mara nyingi mashindano yetu huwa na makundi manne nasi tutakuwa na jeuri ya kuweka kundi moja kwenye uwanja wa kisasa wa Kirumba Mwanza wenye kila kitu kinachokubalika kwa uwanja kuendeshea mashindano ya kimataifa.
Kundi jingine litakuwa Sheikh Amri Abeid Arusha kwenye uwanja wa hadhi hiyo hiyo. Jingine litakuwa uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wenye hadhi hiyo hiyo na la nne litakuwa kwenye uwanja wa Aman, Zanzibar.
Kwenye mechi za mwisho za makundi zinazochezwa pamoja, mechi za kundi la Mwanza zitachezwa Kirumba na Kambarage Shinyanga au Ali Hassan Mwinyi Tabora. Za kundi la Arusha zitachezwa Sheikh Amri Abeid na Mkwakwani Tanga na zile za Dar es Salaam zitachezwa Uhuru na Jamhuri Dodoma huku za Zanzibar zikipigwa Aman na Jamhuri Morogoro kwa nia tu ya kusambaza kipato kwenye miji mingi ingawa si lazima kutumia viwanja vingi hivyo kwa sababu kwenye mechi za mwisho kila makundi mawili yatacheza siku moja.
Robo fainali zitapangiwa miongoni mwa viwanja hivyo. Nusu fainali mbili zitapigwa siku moja kwenye uwanja wa Taifa ambamo baadaye zitapigwa mechi za kutafuta mshindi wa tatu na fainali yenyewe.
Mpaka mashindano hayo yakiisha tutakuwa tumetengeneza pesa nyingi mno kwa utalii wa aina yake kupitia misafara ya timu hizo zote 15 ikijumuisha wachezaji, viongozi na wahudumu wengine. Pamoja nao kila timu itakuja na mashabiki wengi. Kipato kikubwa hivyo kitatokana na uwezo wa kuandaa mashindano makubwa ya bara letu utakaotokana na kuwa na viwanja bora vya michezo.
Njia ya pili ni kwa serikali kubinafsisha baadhi ya viwanja inavyoshindwa kuviboresha yenyewe. Kwa njia hizo, tutakuwa na viwanja bora vya michezo kwa kuinua michezo na kuinuka kiuchumi lakini hali ni mbaya kwa sasa kwa sababu viwanja karibu vyote vya soka nchini, ukiondoa wa Chamazi wa Azam F.C, Kaunda wa Yanga, Manungu wa Mtibwa na vingine vichache visivyo na majina makubwa, vinatajwa kuwa vya CCM, taasisi inayoona ufahari kutajwa kuwa mmiliki wa viwanja hivyo lakini ikiwa haina uwezo wa kuviboresha. Matokeo yake ni kwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kuwa kama gofu kama ulivyo uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Nachelea kupendekeza viwanja hivi kuwa chini ya Halmashauri za miji, manispaa au majiji husika kwani hiyo ndiyo itakuwa kama nyongeza fulani ya chanzo cha kipato cha kifisadi kupitia ubadhilifu uliokithiri kwenye Halmashauri zetu, ubadhilifu unaoshughulikiwa kirafiki mno! Viwanja vyetu vya michezo vikiwekwa huko ndiyo vitakufa kabisa kwa kuliwa.
Katiba yetu iondoe ukiritimba wa CCM kumiliki mali ya umma wasiyoweza kuihudumia. Viwanja vya michezo vya umma ni mali ya umma, hivyo virudishwe kwa umma uamue njia za kuviboresha kwa ajili ya maendeleo yetu ya kimichezo na kiuchumi.
For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....