Wikiendi hii pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara linafunguliwa kwa mchezo wa ngao ya hisani kati ya Simba na Yanga utakaochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. Ni mechi inayosubiriwa kwa hamu. Septemba 27 mechi tatu zitachezwa katika viwanja tofauti.
Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa wageni wa Ligi Kuu Mbeya Kwanza FC saa nane mchana, wakati Namungo FC watawakaribisha wageni wengine Geita Gold saa kumi jioni. Wakongwe Coastal Union watakuwa wenyeji wa mabwanyenye wa Chamazi, Azam fc.
Wakati macho na masikio yanaelekezwa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, kampuni ya Azam Media inafanya kazi ya kuweka taa katika baadhi ya viwanja vitakavyotumika kwa michezo ya Ligi Kuu. Baadhi ya viwanja vitavyowekwa taa ili kuruhusu mechi kuchezwa usiku ni Jamhuri (Dodoma), Kaitaba (Kagera) Mkwakwani (Tanga) na Majaliwa (Lindi).
Duru za michezo na burudani zinabainisha kuwa viwanja vinavyowekwa taa vimefanywa hivyo kimkakati, kwa sababu Lindi (anatoka waziri mkuu na uwanja unaitwa jina lake), Mkwakwani (anatoka rais wa TFF Wallace Karia), Jamhuri (Dodoma ndiko yaliko makao makuu ya serikali) na Kaitaba (Kagera kwa sababu ya eneo la kanda ya ziwa).
TANZANIASPORTS inakuletea uchambuzi juu ya hali mbaya ya viwanja vinavyotarajiwa kutumika Ligi Kuu Tanzania bara kwa sababu matatizo ya enreo la kuchezea (pitch),miundombinu ya ndani na mengineyo muhimu kuhusu michezo ya soka.
Tunafahamu kuwa mara kadhaa TFF na Bodi ya Ligi wamelazimika kuvifungia baadhi ya viwanja kutokana na kasoro mbalimbali. Aidha, serikali imeondoa kodi ya nyasi bandia hatua ambayo ilitarajiwa kufanyiwa haraka kutengenezwa viwanja hivyo kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu kuanza.
UWANJA WA SOKOINE (Mbeya)
Dimba hilo limekuwa likitumiwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara hususani za mkoa huo. Tanzania Prisons waliamua kubadili uwanja na kutumia wa Nelson Mandela uliopo mjini Sumbawanga.
Kiujumla uwanja huu ni mbaya kuanzia eneo la kuchezea,muundo wa ujenzi,miundombinu ya ndani na usalama wa mashabiki na watu wengine unatia shaka kwa namna ulivyo.
Mbeya ni jiji kubwa na linastahili kuwa na uwanja wenye hadhi kubwa, lakini hali ya uwanja wa Sokoine sio nzuri wala haiwafanyi Azam Media kuipa kipaumbele kufunga taa. Si kosa la Azam Media bali wamiliki wa uwanja wenyewe.
LAKE TANGANYIKA (Kigoma)
Kama si kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la FA basi hakukuwa na mpango wa kuupa thamani uwanja huo. Kigoma imekuwa uhaba wa timu zianzoshiriki au kuchagua uwanja wa Lake Tanganyika kuwa wa nyumbani katika mechi za Ligi Kuu. Fainali ya hiyo ilionesha wazi kuwa eneo la kuchezea liliandaliwa kwa ajili ya mchezo huo tu, na zaidi ya hapo ni kama vile unatelekezwa.
MKWAKWANI (Tanga)
Jiji la Tanga lina hadhi kubwa nchini Tanzania. tanga kuna bandari kubwa na yenye kuelekea kupitisha mizigo mingi kwenda nchi kama Uganda. vile vile ni jiji lililopo mwambao wa Bahari ya Hindi, lakini hlaina uwanja mzuri wa soka.
Eneo la kuchezea mpira la uwanja wa Mkwakwani ni baya, na nyasi zake hazionekani kuhudumiwa wala kutengewa bajeti ya kuimarishwa. Mkwakwani unatajwa kuwa moja ya viwanja vibovu vilivyoshindikana, na wachezaji na makocha wanakerwa na huduma ya uwanja huo hivyo kuharibu mifumo ya uchezaji na ufanisi wa timu.
MAJALIWA (Lindi)
Huu ni uwanja ambao umebeba jina la mheshimiwa waziri mkuu wa Tanzania wa sasa, Kassim Majaliwa. Uwanja huo unatumiwa na timu ya Namungo FC kama wa nyumbani.
Namungo ni timu iliyowakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa msimu uliopita 2020/2021. Kama ungekuwa uwanja mzuri basi Namungo wangeruhusiwa kutumia uwanja huo kwenye mashindano ya kimataifa. Ukweli ni kwamba uwanja huo una eneo baya la kuchezea na hakujaonekana kama kuna mpango wowote wa marekabisho.
CCM KIRUMBA (Mwanza)
Wakati klabu ya Biashara United ilipochagua kutumia uwanja wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza kama wa nyumbani katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho la CAF iliamini unafaa kutumika mashindanoni.
Wakaguzi wa CAF walipotembelea uwanja wa CCM Kirumba hawakuridhishwa na miundo mbinu uwanjani hapo. Eneo la kuchezea, huduma muhimu za ndani ya uwanja ni kasoro ambazo zilisababisha uwanja huo ukataliwe.
Biashara United kwa vile hakuna uwanja wenye vigezo katika mkoa wao wa Mara walilazimika kuchagua CCM Kirumba lakini nao wakashindwa hivyo kuangukia uwanja wa Azam Complex wa mabwanyenye wa Chamazi, Dar es salaam.
CCM Kirumba ni uwanja ambao ulipaswa kubeba sifa na hadhi ya jiji kongwe la Mwanza baada ya Dar es salaam. Lakini kwa kipindi cha miaka 20 wamiliki wa uwanja huo CCM wameshindwa kuimarisha na kutoa huduma za msingi hivyo kugeuzwa kuwa uwanja mbaya unaopoteza hadhi kila kukicha.
Miaka ya nyuma Yanga waliwahi kuchagua uwanja huo kama wa nyumbani ambapo waliikaribisha Mamelodi Sundowns kwenye mchezo wa marudiano wa mashindano ya CAF. Leo hii CCM Kirumba haufai hata kuchezewa kombe la shirikisho.
JAMHURI (Dodoma)
Uwanja huu ni wa nyumbani wa timu ya Dodoma Jiji. Ni uwanja ulipo katika makao makuu ya serikali ya Tanzania. ni sawa na kusema Dodoma ni Mji mkuu wa Tanzania ambao una uwanja mbaya zaidi.
Eneo la kuchezea na miundo mbinu mingine ni mambo yanayokarahisha zaidi. pia Dodoma Jiji ni timu ya serikali ambayo ilipaswa kuwekewa mazingira mazuri ya utendaji wa kazi zao kama mfano kwa timu zingine.
Lakini Jmahuri umekuwa uwanja ambao unaharibu sifa za kamera za Televisheni ambazo zinatangaza soka la Tanzania lakini katika eneo baya la kuchezea. Ikumbukwe uchafu au mazigira duni sio sifa ya kujigamba nayo wala kuendekeza. Ni muhimu serikali ione aibu kwa hali ya uwanja huo.
JAMHURI (Morogoro)
Huu ni uwanja uliopo Manispaa ya Morogoro ambao hutumiwa na timu ya Mtibwa Sugar hususani wanapokutana na timu vigogo kama vile Simba na Yanga. Ni uwanja mabo una eneo baya la kuchezea na miundo mbinu yake sio mizuri.
Ndio maana TFF na Bodi ya Ligi waliufungia kwa muda msimu uliopita ili kuwalazimisha wamiliki wafanye marekebisho kabla ya kuruhusiwa kuendelea. Uwanja huo ungeliweza kutumika katika mashindano mengine mfano CECAFA kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
SHEIKH AMRI ABEID(Arusha)
Jiji la Arusha limekuwa maarufu kwa shughuli za utalii, lakini kwenye michezo limedorora mno. Endapo uwanja wake ungekuwa mzuri bila shaka timu zingegombania kuchagua kuwa wa nyumbani.
Eneo la kuchezea mpira,nyasi na miundombinu ya uwanja wenyewe ni hali mbaya na isiyovutia. Ni uwanja ambao huwezi kuchagua hata kuendesha mashindano ya timu za vijana za chini ya iaka 20 za Ligi Kuu wala kwenye mashindano mengine ya soka.
Sheikh Amri Abeid ni uwanja uliotakiwa kubeba heshima na hadhi ya jiji la Arusha, lakini wamiliki wake wapo na hawaonekani kuchungulia fursa hiyo ya kwa kuimarisha na kukaribisha timu za Ligi Kuu kutumia uwanja wao.
CCM MAJIMAJI (Songea)
Uwanja huu ulichaguliwa katumika katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la shirikisho ASFC ambako ulizikutanisha Simba na Azam fc. Ni uwanja ambao una eneo baya la kuchezea na huduma uwanjani hapo ni hafifu.
Ni kama uwanja huo ulitekelezwa na wamiliki wake hali ambayo ilitengeneza vichuguu na mchwa kwa wingi sana. Endapo uwanja huo ungekuwa unatunzwa unafaa kwa mashindano ya Ligi Kuu nap engine ungechaguliwa kuwa mwenyeji wa timu yoyote ya Ligi Kuu.
SAMORA (Iringa)
Iringa ni mkoa ambao umewahi kutoa timu zilizoshiriki Ligi Kuu mara kadhaa, lakini umekosa uwanja wenye hadhi ya kutumika katiika mashindano hayo.
Uwanja wa Samora Machel una eneo baya la kuchezea mpira kiasi kwamba ni vigumu hata timu za Ligi Kuu kuchagua kuwa uwanja wa nyumbani. Wamiliki wa uwanja huo kama vingine bado wamelala usingizi ambao unadhoofisha sketa ya michezo mkoani humo.
Kuhitimisha, wakati zoezi la uwekwaji wa taa katika baadhi viwanja likifanyika, ni muhimu kutoa kipaumbele kwenye eneo la kuchezea mpira kwa sababu hakuna nyasi zenye ubora na viwanja hivi vimekuwa matatizo makubwa kwa wachezaji,makocha na viongozi wa mpira.