Menu
in , ,

VITU MUHIMU KWENYE MECHI ZA KUFUZU KOMBE LA DUNIA NCHINI RUSSIA 2018

Kuna vitu ambavyo unaweza ukafanya na ukaonekana bora na kila mtu
akafurahia ubora wako kwa sababu umedhibitisha kuwa wewe ni bora.

Ubora mara nyingi hukamirika pale unapokuwa shujaa, shujaa hukumbukwa
na vizazi vyote, shujaa historia yake siku zote haifutiki.

Kitu kizuri ni pale ubora wako unapokufanya uwe shujaa wa nchi yako,
jana Messi alitakiwa kudhibitisha kuwa yeye ni moja ya wachezaji bora
duniani.

Ubora wake ulikuwa ukitizamwa na kila mtu , kila jicho lilitamani
kuona ni kipi ambacho angefanya ili kuiokoa timu yake ambayo ilikuwa
na hatihati ya kufuzu kombe la dunia.

Kitu ambacho wengi walikitamani kitokee ndicho hicho ambacho Messi
alikifanya, ambapo alijitwishwa timu yake mgongoni mwake na kukimbia
kuipeleka Russia.

Inawezekana ukawa umeumia kwa kiasi kikubwa na Chile kukosekana katika
kombe la dunia huko nchini Russia la mwaka 2018.

Timu ambayo ilikuwa na kila aina ya kipaji ambacho kingewahikikishia
kufuzu kombe la dunia kwa mara ya tatu mfululizo,yani mwaka 2010, 2014
na mwaka 2018 ambao wameshindwa kufuzu.

Mabingwa wa kombe la Amerika ya kusini mara mbili mfululizo, na
wanafainali wa kombe la Mabara mwaka huu.

Kikosi cha Chile kimetumika kile kile kwa muda mrefu, kikosi chao ni
kidogo na hawakuwa na mpango mzuri kwa wao kutengeneza watu ambao
wataingia taratibu kwenye kikosi ili wawasaidie hawa ambao wametumika
muda mrefu.

Hiki kitu ndicho ambacho kimewagharimu kwa kiasi kikubwa Uholanzi,
wamekuwa na kikosi kile kile kwa muda mrefu , kikosi ambacho
hakikutafutiwa watu wa kuja kuwasaidia waliopo.

Hivo imepelekea hawa waliopo kuteendana na kasi kitu ambacho
kiliwafanya wawe wanahangaika sana , ikizingatia kwa sasa mataifa
mengi yamewekeza kwa kiasi kikubwa katika mpira kitu ambacho kimeleta
mapinduzi makubwa katika mpira.

Leo hii nchi kama Iceland na Panama wanafuzu kwa mara ya kwanza kombe
la dunia kwa sababu ya mipango ambayo waliwekeza katika maendeleo ya
soka katika nchi zao.

Ndiyo maana unaona kuna baadhi ya nchi zinasubiri mpaka mechi za
mwisho ilikujihakikishia kufuzu kombe la dunia.

Wales wanaweza wakawa wanajilaumu wenyewe, kushindwa kupata ushindi
katika mechi yao ya mwisho katika ardhi yao ya nyumbani tena wakiwa na
kumbukumbu nzuri ya wao kufanya vzuri katika kombe la Euro 2016 kwa
kushika nafasi ya tatu.

Wamewaachia Ireland ya Kaskazini ambayo itaungana na Jamhuri ya
Ireland katika mechi za mtoano kutafuta timu nne ambazo zitakamilisha
timu 16 za ulaya kwenda Russia 2018.

wachezaji wa Brazil wakifurahia kufuzu kwenye kombe la Dunia 2018, Urusi.

Baba yao amefuzu , lakini kufuzu kwao kunaonesha kuwa wanaenda Russia
lakini wakiwa na kikosi ambacho siyo imara, kikosi ambacho hakina
uzito mkubwa wa kushindana kuchukua kombe.

Ni kitu cha kushangaza Uganda kusimama katikati ya miamba miwili ya
soka barani Afrika yani Misri na Ghana.

Ingawa hawajafuzu lakini Uganda imeonesha ukomavu wa kutosha, ukomavu
ambao wanatakiwa kuutumia kwa ajili ya michuano ijayo. Waendelee
kwenye mwamvuli huo huo wa mafanikio yao ili waweze kupata nafasi ya
kufuzu kombe la dunia ijayo.

Kuna vizazi vingi vikubwa vilipita pale Misri, vizazi ambavyo vilikuwa
vimebarikiwa kwa kiasi kikubwa uwezo wa kucheza mpira lakini
havikuweza kuipeleka Misri kombe la dunia.

Walisubiri miaka 28 ili waende kombe la dunia kupitia miguu ya Mohamed
Salah, shujaa mpya ambaye vitabu vya historia vya soka nchini Misri
vitamkumbuka milele.

Kuwepo kwa wachezaji wa kulipwa katika timu za Afrika inatoa mchango
mkubwa sana katika maendeleo ya timu za Taifa za Afrika.

Mohamed Salah ameisaidia Misri kuipelekea nchini Russia 2018 katika
kombe la dunia. Pia ilimchukua dakika nne Alex Iwobi baada ya kuingia
kutokea benchi na kufunga goli ambalo liliipeleka Nigeria katika kombe
la dunia nchini Russia.

Hawa wote ni wachezaji wa kulipwa ambao wanacheza katika soka la
kulipwa nchini Uingereza .

Hii inamaanisha kuwa na idadi ya wachezaji wa kulipwa katika kikosi cha
timu ya taifa kunaipa nafasi timu ya taifa kufanya vizuri kwa sababu
wachezaji wa kulipwa huwa wanakuwa na uwezo wa kumaliza vizuri kwenye
mechi za kimataifa.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version