Menu
in , , ,

Vita kuu tano Yanga na Simba leo

Tanzania Sports

HATIMAYE muda wa vigogo vya soka nchini kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu umewahidia, na leo Oktoba 19 kivumbi na jasho kitatimka katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam. Yanga na Simba zinakutana katika mchezo wa kwanza kwenye mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania bara. Ikumbukwe katika mchezo uliopita wa kufungua msimu, Ngao ya Jamii, Yanga waliibuka na ushindi wa bao moja kwa nunge. Hata hivyo siku zote mchezo wa vigogo huwa hautabiriki hata kama upande mmoja unaweza kudhaniwa ni dhaifu. Kwenye mchezo uliopita ushindani ulikuwa mkubwa kuanzia mbinu za makocha na wachezaji wenyewe pamoja na mashabiki ambao walishindana kushangilia kwa nguvu. Pambano hili linaingia katika vita kuu tatu ambazo mashabiki wanapaswa kuzingatia.

VITA KALI YA MAKIPA LANGONI

Hakuna ubishi makipa waliosajiliwa na timu hizo mbili ni mahiri na wameonesha uwezo mkubwa. Makipa hapo ni Moussa Camara raia wa Guinea na ndiye mlinda mlango namba moja wa Simba kwa sasa, huku Yanga wanalinda lango lao wakiwa na Djigui Diara raia wa Mali ambaye uwezo wake wa kusakata kandanda si wa kutilia shaka. Simba na Yanga wanavijuvunia kuwa na makipa wenye uwezo mkubwa kuzuia michomo na kushiriki mchezo kwa dakika zote 90. 

Umahiri wa Moussa Camara umeonekana mapema zaidi na awapo langoni anajiamini pamoja na kuwa na uwezo wa kusogea yadi 38 kutoka eneo lake. Ni golikipa ambaye ameleta ladha ya aina yake si katika klabu ya Simba pekee bali hata Ligi Kuu. Hali kadhalika Djigui Diara amekuwa kipa mahiri aliyetinga fainali ya Kombe la shirikisho, na alifanya vizuri kwenye mashindano ya AFCON nchini Ivory Coast. Diara pia amefanya vema akiwa na Yanga msimu uliopita licha ya kuondoshwa mashindanoni na Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini.  Umahiri wa makipa wa timu zote mbili uneifanya Kariakoo Derby iwe ya moto mno. Mashabiki wa pande zote mbili wanajivunia makipa hao, na hivyo kuwa mojawapo ya eneo ambalo litawaletea burudani na ushindani mkali, nani anaweza kulinda lango na nyavu zake kutotikiswa.

PRESHA YA MABEKI WA KATI

Kule Simba kuna Chermalone na Ibrahim Hamza, wakati Yanga kuna Ibrahim Bacca na Dickson Job au Bakari Nondo. Mabeki hawa wanasifika kuwa mahiri katika kulinda lango lao. Kombinenga ya Bacca na Job imehamia hadi timu ya Taifa Stars na kuwa moto wa kuotea mbali. Simba msimu uliopita ilikuwa na Inonga nas Chermalone katika safu ya ulinzi wa kati, lakini msimu huu wameingiza kitasa kingine Ibrahim Hamza ambaye ameziba vema pengo la Mkongomani huyo aliyehama Msimbazi. 

Hamza amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya ulinzi ya Simba, ingawaje kuelekea Derby kulikuwa na taarifa za kuumia na kuwa sababu ya kutocheza katika mechi za Taifa Stars. Hata hivyo safu ya ulinzi ya Simba imeimarika na inacheza kwa kasi muda wote, pamoja na kupandisha mashambulizi. Malone ni beki mzuri kuelekea kulia au katikati na si mcheza rafu lakini ni kitasa cha aina yake. Kwenye safu hii vita itakuwa kuzima mashambulizi ya washambuliaji wenye uchu. Yanga watakuwa na kibarua cha kumdhibiti Leonel Ateba, Edwin Balua, Joshua Mutale, Ahoua na Kibu Dennis, wakati Simba nao watakuwa na kazi ya kuwadhibiti Prince Dube, Clement Mzize, Kennedy Musonda, Jean Baleke pamoja na Stephane Aziz Ki. Je nani atalia na nani atacheka, matokeo yatajibu.

KUCHEKA NA NYAVU

Yanga wanaweza kumpanga mshambuliaji yeyote kulingana na mahitaji ya kocha wao Miguel Gamondi. Kwa upande wao Simba wapo wazi kabisa Fadlu David ataanza na Leonel Ateba ambaye amekuwa kivutio miongoni mwa mashabiki wa soka nchini. Kwa msingi huo Gamondi anaweza kuingia dimbani akiwa na Prince Dube, Clement Mzize,Kenned Musonda, Aziz Ki, na Maxi Nzengeli. 

Simba nao wanaweza kuwaongeza Balua, Ahoua, Kibu na Mutale au Valentino Mashaka kadiri mwalimu atakavyaoamua. Lakini swali kubwa linaloibua vita ni nani atakuwa wa kwanza kucheka na vyavu? Si hilo tu swali lingine nani atacheka nyavu katika mchezo wa Derby ya leo? Ni Aziz Ki au Leonel Ateba? Kama utazungumzia wachezaji chipukizi basi Yanga wanaye Clement Mzize na Simba wanacho kipaji cha Edwin Balua. Sifa ya wachezaji wa kundi hili ni kasi, wote kwa pamoja na wanayo sifa ya kucheza kwa kasi na kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.

VICHWA VYA MAKOCHA

Nilitazama video ya makocha Fadlu David na Miguel Gamondi wakati wakisalimiana kwenye mkutano na vyombo vya habari. Salamu ya makocha hao ilikuwa fupi sana, walipeana mikono ya heri na kusalimiana maneno machache kisha kila mmoja akaendelea na ratiba yake. Hii ilikuwa salamu fupi na kudhihirishwa vichwa vyao vinasomana na kubeba presha kubwa ya mchezo huo. Kiufundi makocha hawa wote wanaweza kupanga kikosi cha kucheza kwa kasi muda wote wa mchezo. 

Fadlu David ameonesha kuwa anapenda kuona mabeki wake wa pembeni wanapanda mbele zaidi kuliko kawaida. Mara nyingi ameonekana akiwafokea wachezaji wa maeneo hayo na kuwaonesha ishara ya kupanda mbele zaidi. Mohammed Hussein na Shomari Kapombe wamekuwa wakipandisha mashambulizi kuliko kawaida. Mchezo wa kasi anaofundisha Fadlu umekuwa tishio hasa unapocheza na timu kubwa na yenye hadhi kubwa ya kimbinu kama Yanga. Lakini wanapokutana na timu nyingine kasi yao inakuwa imepoa na hata uwajibikaji huwa  wa kiwango cha kawaida. 

Kichwa cha Fadlu David kinasifiwa kwa uwezo wa kufanya mabadiliko yanayotishia zaidi wapinzani na kusababisha timu yake kuibuka mshindi. Hakuna anayweza kubeza ushindi wake kimataifa. Upande wa Miguel Gamondi anayo machaguo mengi kichwnai mwake katika mchezo huo. Safu ya ushambuliaji bila shaka itakuwa na washambuliaji watatu kwa wakati mmoja huku Clement Mzize akipelekwa winga wa kulia ili kumpa nafasi Prince Dube kutawala eneo la mshambuliaji wa kati. Hata hivyo Gamondi anaelewa mchezo huo ni mgumu hivyo hawezi kwenda kichwa kichwa bila akili ya Maxi Nzengeli katika kuweka uwiano kati ya ulinzi na usambuliaji. Kimsingi vichwa vya makocha hawa navyo ni vita nyingine kwenye Kariakoo Derby.

SHANGWE ZA MASHABIKI

Hii ni vita ya wazi kabisa katika mchezo wa kandanda. Simba na Yanga wanapokutana vita nyingine inakuwa nje ya uwanja yaani mashabiki wake. Hawa ndiyo wachezaji namba 12 ambao wanatia hamasa na kuzifanya timu zicheze kwa ari na nguvu pamoja na maarifa makubwa. Mashabiki wanatoa hamasa na mchango wa aina yake kwa wachezaji wa timu zote mbili. Ushangilia, vituko vya hapa na pale, utani na kutambiana ndivyo vitu vinavyoufanya mchezo huo kuwa mkali zaidi na wao wanachochea zaidi nje ya uwanja hadi ndani ya uwanja. Hakuna ubishi mashabiki ni wachezaji namba 12.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version