KATIKA sehemu ya kwanza ya makala hii tuliona jinsi Simba ilivyokusanya vijana mwaka 1971 na kutengeneza timu iliyokuja kuleta matunda mazuri mwaka 1974. Kikosi hicho hakikuwa moja ya vikosi vinne vya Yanga na Simba vilivyoanzishwa kisayansi kwa sababu hicho kilitokana na vijana wenye vipaji waliokusanywa toka timu tofauti Tanzania.
Miongoni mwa vile vilivyotengenezwa na Yanga na Simba wenyewe, tulianza na kikosi cha Yanga Kids cha mwaka 1972 kilichokuja ibeba Pan African na timu ya taifa. Leo tunaendelea na vikosi vitatu vilivyobaki.
Vijana wa Simba 1977
Simba ilikuwa inatisha mwaka 1977 ambapo kikosi chake cha kwanza kilikuwa cha kipa Omar Mahadhi, mabeki wa kulia Daud Salum na kushoto Mohammed Kajole. Mabeki wa kati Athumani Juma, Aloo Mwitu na Mohammed “Tall” Bakari. Viungo wa nyuma Aluu Ally na Iddi Kibonye na mbele ni Ezekiel Grayson “Jujuman”, Ismail Mwarabu na Abdallah Mwinyimkuu. Kulia ni Willy Mwaijibe na Abbas Dilunga na kushoto ni Martin Kikwa.
Wafunga mabao walikuwa Abdallah “King” Kibaden, Adam Sabu na Jumanne Hassan Masmenti “Tarzan”. Mbele ya kikosi hiki mtu ukitoka ilikuwa bahati. Ndicho kikosi kilichoifunga Yanga 6-0 mwaka huo.
Baada ya Pan African kuanzishwa, kufikia mwaka wa tukio tutakalolikumbushia, Simba hii ilicheza nao mara tatu. Jijini Arusha walitoka sare ya 3-3. Wakacheza mechi “ya kirafiki” Dar es Salaam na mechi hiyo kuvunjika kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika baada ya wachezaji wa timu hizo mbili kupigana ovyo ovyo huku Kibaden akichaniwa jezi vipande vipande! Wakati huo matokeo yalikuwa bado 0-0.
Mechi ya tatu ilikuwa ya kugombea kombe la Biashara ambayo lilimalizika kwa suluhu huku ikiwa limejaa msisimko mkubwa kama kona za hatari za Kajole, vichwa vya Jumanne, Kikwa na Sabu. Kasi ya Kassim Manara kushoto kwa safu ya ushambuliaji ya Pan African na makwanja ya Daud Salum kwa Manara aliyekuwa hazuiliki kiuana michezo. Nyingine ilikuwa burudani iliyojitegemea ya Martin Kikwa kushoto kwa Simba kwenye ushambuliaji na mikiki ya Juma Shaaban
kumdhibiti. Baada ya suluhu hiyo, ilipangwa tarehe ya mbali ya marudiano.
Wakati Simba ikijiandaa na pambano hilo kubwa chini ya kocha Samsarov kutoka Bulgaria, kukatokea tatizo miongoni mwa wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza lililowafanya wasishiriki mazoezi. Viongozi wa Simba wakichanganyikiwa, kocha Samsarov akawaandaa vijana wadogo wa Simba kwa pambano hilo kubwa.
Watu walishangaa siku ya mechi hiyo kuuona muziki kamili wa Pan African dhidi ya vitoto vya Simba vilivyoongezewa nguvu na kipa Mahadhi na beki Kajole tu! Watu wakaona kuwa siku hiyo kwa uchache sana Pan ingeshinda kwa mabao 10-0!
Mechi ilipoanza, Pan kamili walipata bao la mapema na watoto wa Simba wakiwemo mabeki Abbas Kuka, Filbert Rubibira, winga wa kulia Rahim Lumelezi na wa kushoto George “Best” Kulagwa, kiungo Nicodemus Njohole na wengine walisawazisha bao kipindi cha pili na kuweka kambi kwenye eneo la Pan African kamili. Wakati wowote ule wangeweza kufunga bao la ushindi au mabao ya ushindi lakini haikuwa hivyo na mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 1-1 ikiwaacha watu na mshangao mkubwa.
Tangu siku hiyo baadhi ya vijana hao kama Nico Njohole, Kulagwa, Lumelezi na Kuka walikamata namba kikosi cha kwanza lakini Lumelezi alikatizwa soka yake kwa kuvunjika mguu. Hilo lilikuwa tatizo kubwa mno miaka hiyo. Vijana hawa walichangia kuipa Simba ubingwa wa mfululizo wa nchi hii ulioanza mwaka 1976 na kudumu mpaka mwaka 1980.
Black Stars ya Yanga 1995
Mwaka 1994 wachezaji wakubwa wa Yanga wa kitanzania waliingia kwenye mgogoro wa Yanga asili na Yanga kampuni na kuamua kuukomoa uongozi. Walifungwa na Simba 4-1 kwa kinachosadikiwa kutekeleza mgomo huo. Yanga hii ilikuwa ya kina makipa Steven Nemes na Rifat Said,mabeki Ngandou Ramadhan, Joseph Lazaro, Kenneth Mkapa, Willy Mtendamema, Costantine Kimanda na Willy Martin.
Viungo wa kati walikuwa Method Mogella, Mwanamtwa Kihwelo, Said Mwamba, Sekilojo Chambua na wa pembeni (mawinga) David Mjanja, Sanifu Lazaro na Edibily Lunyamila. Wafunga mabao walikuwa Mohammed Hussein Mmachinga, James Tungaraza na Ally Yussuf “Tigana” miongoni mwa wachezaji wengine.
Mgogoro huo ulisababisha kipa Rifat Said kurudi Zanzibar, Edibily Lunyamila kuchukuliwa na Malindi ya Zanzibar kwa msimu mmoja, Steven Nemes na Said Mwamba kujiunga na Simba baada ya mgogoro huo kuwa mkubwa huku kocha Tambwe Leya akikisuka kikosi cha watoto wenye kipaji cha soka aliowakusanya. Alikiita kikosi hicho cha watoto Black Stars.
Miongoni mwa wachezaji wa kikosi hicho walikuwa Anwar Awadh, Mzee Abdallah, Silvatus Ibrahim “Polisi”, Maalim Saleh “Romario”, Nonda Shaaban “Papii” na wengine. Tukumbushane kwamba katika kipindi hicho, tangu kipigo cha 4-1 toka kwa Simba. Yanga ilikuwa ikifungwa mfululizo na Simba na mwiba wao mkali ulikuwa Madaraka Selemani, Mzee wa Kiminyio.
Baada ya vijana wengi wa Black Stars kujumuishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga, likaja pambano la Yanga na Simba na Madaraka akiwemo. Pambano hilo la kwanza msimu wa 1996, lilimalizika kwa suluhu huku Mzee wa Kiminyio akiminywa vilivyo na kijana mdogo Anwar Awadh aliyekuwa beki wa kushoto. Baada ya mechi, mashabiki wa Yanga walimbeba juu juu Anwar kwani hawakuamini kama angeweza kumzuia hivyo Madaraka.
Baadhi ya vijana hawa walikuja kuijenga Yanga imara iliyokuja kucheza ligi ya kwanza ya nane bora ya ubingwa wa Afrika mwaka 1998 na kubeba ubingwa wa Afrika mashariki na ya kati nchini Uganda mwaka 1999 huku ikitoa mchezaji mkubwa wa dunia, Nonda Shaaban.
Kikosi cha watoto wa Simba cha sasa
Kikosi cha sasa hivi cha watoto wa Simba ni wazi kitakuja kuwa Simba kali mno ya baadaye. Ni kikosi kilichoenea idara zote kama kile cha Yanga Kids cha mwaka 1972. Hiki kina wachezaji wazuri zaidi ya mmoja wa kila nafasi wanaopandishwa kwenye kikosi cha kwanza kila wanapoiva. Alianza kupandishwa kiungo Jonas Mkude, wakafuata washambuliaji Edward Christopher na Frank Sekule. Wakafuata tena washambuliaji Abdallah Seseme, Ramadhani Singano “Messi” na Haruna Chononga.
Majuzi wameongezeka beki wa kati Hassan Kondo Khatib na beki wa kushoto Miraji Adam. Watoto hawa wamekuwa wakifanya vizuri kwenye kila mashindano wanayoshiriki peke yao, wakiwa wameshabeba kombe moja la BancABC Super 8, mashindano ambayo ndani yake walipambana na kuvishinda vikosi kamili vya timu kadhaa kubwa za nchi hii kama Mtibwa Sugar na Azam FC za bara pamoja na timu kadhaa kubwa za visiwani.
Simba ikienda vizuri na watoto hawa, itakuwa na kikosi cha kutisha baadaye ili mradi watu wa Simba wasiwe moto kulazimisha mafanikio ya muda mfupi. Jambo la kufurahisha ni kwamba baadhi yao wameshaanza kuitwa kwenye timu ya taifa.
Hitimisho
Ukifuatilia uanzishwaji wa vikosi hivi vinne utaona kwamba cha mwaka 1972 cha Yanga na cha mwaka huu cha Simba, vimeanzishwa kwa maamuzi tu ya kuvianzisha kutafuta maendeleo, wakati kile cha Simba cha 1977 na cha Yanga cha 1995, vilianzishwa kwa kukabili matatizo ya vikosi vya kwanza.
Ni vizuri kuwa na vikosi vya timu za marika tofauti kufanywa kuwa jambo la kimfumo na si la kusubiri tatizo. Hivi ndivyo dunia inavyokwenda na sisi tunapaswa twende hivyo.
Faida kwa Yanga na Simba ya vikosi hivi vya watoto ni kupata timu za mashabiki tupu wa klabu zao kwani kisayansi watoto wakiitwa kwenda Simba kuanza taratibu za kutengenezwa kwa timu ya watoto, watoto watakaoenda huko ni wanaoipenda Simba tu. Hali ni hiyo hiyo kwa watoto watakaoitwa Yanga.
Faida hapa ni kwamba watoto hawa katika maisha yao ya soka ndani ya timu hizo watajituma mno, kwa nguvu na kwa akili, kuhakikisha timu wazipendazo zinapata mafanikio. Wakifanya hivyo wataonekana kufaa kwa timu ya Taifa na mawakala watawaona wanafaa kwa soka ya kulipwa.
Kwa uhakika, kupitia soka ya watoto, kila klabu itajaza kwenye timu zao wachezaji wenye upendo wa wazi na mkubwa wa timu zao kama alivyo Steve Gerrard wa Liverpool kwa Liverpool yake.
…mwisho…