KAMPUNI ya vinywaji baridi ya Coca cola itapeleka wachezaji bora 16 kwenye kambi ya kimataifa ya soka iliyopo Rio de Janeiro, Brazil iliyopangwa kuanza Julai 7 mwaka huu.
Afisa Masoko wa kampuni hiyo, Carolyne Mbaga alisema wachezaji hao watachaguliwa na kamati ya ufundi ya vijana ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kutokana na kuonyesha kiwango kizuri katika mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Copa coca cola ngazi ya taifa atakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 8 hadi 28.
“Mwaka jana tulipeleka wachezaji watatu katika kambi hiyo, lakini mwaka huu tumeamua kuwapeleka timu ya wachezaji 16 ili kumvutia kila kijana kushiriki katika kuendeleza vipaji vya soka la vijana Tanzania,” alisema Mbaga.
Alisema kampuni hiyo itawalipia wachezaji, maofisa wawili kutoka Shirikisho la soka Tanzania (TFF) pamoja na mwakilishi mmoja wa Cocacola Tanzania tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi, malazi pamoja na posho muda wote watakaokuwa Brazil.
Mwaka jana kampuni hiyo ilipewaleka wachezaji bora watatu katika kambi hiyo ambao walipatikana katika michuano ya copacocacola ya mwaka jana akiwepo nahodha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Bunu Abdallah.
Mashindano ya Copacocacola huanzia katika ngazi ya wilaya hadi taifa, na kushirikisha mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar.Bingwa wa michuano hiyo mwaka huu atapata Sh. 4.5 Milioni, mshindi wa pili atapata Sh. Milioni 3 wakati mshindi wa tatu atajinyakulia Sh2milioni.