Menu
in , , ,

Vigogo wapigwa


*Arsenal, Man City, Spurs kichapo
*Manchester United wanacheka tu

Ligi Kuu ya England imemaliza mzunguko wa 11 kwa matokeo ambayo hayakutarajiwa, ambapo vigogo wengi wamelizwa katika siku iliyokuwa zaidi ya bao moja bila.

Katika mechi ya mwisho jioni ya Jumapili, Manchester United waliwazamisha Arsenal katika dimba la Old Trafford kwenye mechi ambayo watu walitarajia Arsenal kuendelea kung’ara.

Alikuwa Robin van Persie aliyewaliza Gunners katika kipindi cha kwanza, kwa wao kushindwa kusafisha mpira wa kona ambao aliupiga kwa kichwa na kutinga wavuni.

Hata hivyo, kwenye kipindi cha pili Arsenal walicheza vizuri, wakirejea mchezo wao wa kawaida wa pasi fupi fupi ambao ulitibuliwa katika kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kuliona lango la wapinzani wao.

Ushindi wa Man U umewapandisha hadi nafasi ya tano wakiwa na pointi 20 wakati Arsenal wanabaki kileleni kwa pointi zao 25.

Katika mechi za awali, Tottenham Hotspur walifungwa pia bao 1-0 na Newcastle walioonesha kufufuka upya chini ya kocha wao yule yule Alan Pardew, akimwacha mwenzake Andre Villas-Boas akiwa hana raha nyumbani kwake White Hart Lane.

Spurs wamejikuta katika nafasi ya saba kutokana na matokeo hato, wakati Newcastle wamepanda hadi nafasi ya tisa.

Manchester City nao waliangukia pua, wakipoteza mechi yao ya nne ya Ligi Kuu, na safari hii ikiwa ni mikononi mwa timu iliyochukuliwa kuwa dhaifu sana ya Sunderland.

Hata hivyo, kwa mechi ya Jumapili hii, ingekuwa vigumu kusema ndiyo Sunderland iliyozoeleka kwa jinsi walivyoweza kugangamala kuzuia kufungwa, japokuwa Man City walitawala sana mchezo.

Bao la mapema la Phil Bardsley lilitosha kuwapa ushindi ‘Black Cats’ waliokuwa wakicheza nyumbani kwao chini ya kocha wao mpya Gus Poyet aliyewabadilisha sana wachezaji wake na kuanza kujiamini kwa pasi safi.

Katika mechi nyingine, Swansea na Stoke City walikwenda sare ya mabao 3-3 katika mchezo mkali uliofanyika huko Wales.

Baada ya kukamilika mzunguko wa 11, Arsenal wanabaki kileleni wakifuatiwa na Liverpool walio nyuma yao kwa pointi mbili na Southampton kwa pointi moja.

Chelsea wapo nafasi ya nne wakiwa na pointi 21 wakati Manchester United wameipata nafasi ya tano kwa pointi zao 20 sawa na Everton na Spurs.

Man City wapo nafasi ya nane wakiwa na pointi 19, Newcastle wanafuatia na pointi 17, wakati West Bromwich Albion wana pointi 14 sawa na Aston Villa na Hull.

Swansea wapo nafasi ya 13 wakiwa wameambulia pointi 12 zinazolingana na wenzao wa nchini Wales, Cardiff huku Norwich wakishika nafasi ya 15 kwa pointi zao 11.

West Ham na Stoke wanafungana kwa pointi 10 huku Fulham wenye pointi kama hizo wakiwa wametoswa kwenye timu tatu za mwisho sawa na Sunderland wenye pointi saba na Crystal Palace wenye nne tu.

51.577973-0.130302

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version