TIMU za soka za Simba na Yanga za Dar es Salaam zimeuanza vibaya mwaka 2012 kwa kupata vipigo kwenye mechi za kuwania Kombe la Mapinduzi Zanzibar mwaka huu jambo ambalo limezitonesha kidonda timu hizo cha kufungwa kwenye mechi tofauti za kirafiki zilizofanyika wakati wa kumaliza mwaka 2011.
Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza ambapo Jumatatu usiku wa kuamkia Jumanne wiki hii ilicharazwa goli 1-0 na timu changa ya Mafunzo ya Zanzibar ukilinganisha na ukongwe wa Yanga.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi inashirikisha timu tatu kutoka Tanzania Bara na zingine tatu za Tanzania Zanzibar.
Kipigo hicho kwa Yanga kilitokea wakati ikikumbuka kufungwa mwishoni mwa mwaka jana magoli 2-0 na timu ya Azam FC inayojiandaa kutawala Tanzania kisoka na kiuendeshaji kutokana na kuwa ya kwanza nchini kuwa na uwanja wa kisasa na maeneo mbalimbali ya kufanyia mazoezi.
Kwa upande wa Simba SC ambayo mwishoni mwa mwaka jana ilichabangwa magoli 3-2 na timy ya watengeneza Sukari Mtibwa ya Morogoro, usiku wa kuamkia leo Jumatano imekiona cha moto baada ya kuchapwa magoli 2-1 na timu ya Jamhuri kutoka Pemba.
Pigo hilo limekuja baada ya kushuhudia mkongwe mwenzake alipoburuzwa kwenye uwanja huohuo wa Amani Zanzibar kuwani kombe la Mapinduzi ambalo kwa sasa linashikiliwa na Simba.
Kufungwa kwa timu hizo kumewachefua mashabiki wake hususan walioko Tanzania bara ambao kwa jana walishindwa kutambiana kutokana na timu zao kugaragazwa kwenye mashindano hayo wakati zikiwa kwenye maandalizi makubwa ya Ligi Kuu ya VODACOM na pia zinajiandaa na michuano ya Afrika.
Yanga ambayo ni bingwa Tanzania, kwa sasa inajiandaa kumenyana na Zamalek ya Misri katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika wakati nayo Simba inajiandaa kucheza na Kinyovu ya Rwanda katika mechi za Kombe la Shirikisho zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Lakini pia vipigo hivyo kwa klabu kongwe za Bara, vinaashiria wazi kwamba soka la Zanzibar linazidi kukua kwani mpaka sasa ni timu ya Azam FC kutoka Bara ambayo imepata ushindi kwa kuifunga magoli 3-1 timu ya Kikwajuni Zanzibar.
Mechi zinazotarajiwa kufanyika baadaye kuanzia leo jioni ni za Yanga kwa kucheza na Kikwajuni, Azam na Mafunzo wakati Simba nayo imebakiza mechi dhidi ya Miembeni na KMKM.