Tangu kuanzishwa kwa mfumo mpya wa Mwamuzi Msaidizi kupitia Video (VAR), maswali na changamoto yamekuwa mengi kuliko majibu na suluhisho.
Pamekuwapo migongano mingi juu ya matumizi ya VAR, kwa sababu utata umekuwa mwingi juu ya uamuzi husika, ambapo pia mtiririko wa mechi hukosekana pamwe na ladha yake pale mwamuzi wa kati anapokwenda kuwasiliana na VAR.
Pamoja na makosa yaliyokuwapo uwanjani kwa waamuzi, iwe wa kati au wasaidizi wake washika vibendera sasa wachezaji, makocha, washabiki na wadau wengine wanaonekana kukerwa zaidi na VAR.
Mabao yamekataliwa ambayo kwa mitazamo ya wengi yalionekana ni halali na mmoja wa walalamikaji ni Kocha wa Chelsea, Frank Lampard pamoja na wengine na sasa kocha wa zamani ambaye ni ofisa wa Shirikisho la Soka la KImataifa (Fifa), Arsene Wenger, naye ameona kuna walakini.
Anasema kwamba hakuna sababu pale mshambuliaji wa mwisho anapofanya kazi yake, kisha akamzidi beki kwa kiungo kwa kiasi kidogo tu, basi anachukuliwa ameotea. Nakumbuka mchezaji wa Liverpool, Roberto Firmino alipatwa na VAR kuwa ameotea kwa sababu tu bega lake kimahesabu lilizidi lile la mlinzi wa Aston Villa.
Kwenye mechi baina ya Manchester City na Sheffield United kwenye Uwanja wa Etihad nako kulikuwa na mambo; malalamiko yakawa makubwa dhidi ya VAR lakini hayakusikilizwa; yaliangukia kwenye uziwi.
Sheffield United au Blades kama wanavyojulikana, walishatia mpira kimiani kupitia kwa Lys Mousset lakini VAR ikakataa kwa maelezo kwamba mfungaji alikuwa ameotea.
Lakini pia jamaa hao walilalamikia bao la kuongoza la Aguero, kwa sababu mwamuzi Chris Kavanagh alionekana kumzinga na kumzuia John Fleck wakati wa majenzi ya bao hilo. Chris Wilder akaondoka akiwa ameshaungana na waamuzi wanaolia dhidi ya VAR kwenye wikiendi nyingine ambayo VAR imezidi kulalamikiwa.
Wilder alikataa kueleza ni kipi alichokuwa akijadiliana na Kavanagh kwenye chumba cha waamuzi baada ya mechi hiyo, lakini kwa ujumla alionekana kusikitishwa sana na waamuzi hao. Alisema alikuwa anajivunia wachezaji wake na timu kwa jinsi walivyojitahidi.
“Ikiwa unapoteza mechi, kuna njia ya kuipoteza. Lakini nimeiona timu yangu na hali ambayo tumekuwa nayo. Je, tulidhani kwamba tungesonga nayo hadi mwisho wa Desemba? Sidhani. Tumeongezeka katika kujiamini na ujasiri. Ni upinde mkubwa wa kujifunza. Hawa jamaa (Manchester City) wana wachezaji mahiri sana. Klabu mbili hizi ni sawa na tofauti ya miaka miwili ya mwanga kwa umbali; hawakuwa hivyo miaka miaka kadhaa iliyopita.
“Klabu moja haikusonga mbele kwa kasi ambayo City walikuwa nayo, lakini sidhani kwamba pale uwanjani pengo lilionekana kubwa kivile kwa mujibu wa ukali wa mchezo. Timu yangu iliamua kujaribu na ndicho kitu cha msingi tulicho nacho,” anasema