HABARI ya kuvutia kwa mashabiki wa soka nchini ni ile ya matumizi ya tekenolojia ya VAR kwenye mashindano mbalimbali soka. Habari kubwa inasema kuwa Shirikisho la soka Afrika CAF limepanga kuvitembelea viwanja vyote vitakavyotumika kwenye mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuona uwezekano wa kuvifanyia majaribio ya teknolojia ya VAR.
Awali teknolojia hiyo ilikuwa ikitumika kwenye mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Lakini msimu huu CAF wameamua kwa kauli moja watatumia kuanzia michezo ya robo fainali ya mashindano hayo.
Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam ni miongoni mwa viwanja vitakavyotumika kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ukiwa mwenyeji wa mabingwa wa soka nchini Tanzania, Klabu ya Simba.
Simba wamekuwa wakitumia uwanja huo kama wa nyumbani katika mashindano yote ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia hatua ya mchujo. Na sasa wameingia robo fainali baada ya kumaliza kinara katika kundi A wakiwa wamejikusanyia pointi 13 na kuwapiga kumbo wapinzani wake Al Ahly ya Misri,As Vita ya DR Congo na El Merrekh ya Sudan.
Teknolojia hiyo inaitwa ‘Video Assistant Referees’ au kwa kifupi inaitwa VAR. Matumizi ya utazamaji picha za video kwa matukio yenye utata uwanjani na mwamuzi kuyatolea hukumu yamewapasua pande mbili mashabiki wa soka.
Kwa mara ya kwanza teknolojia hii ya VAR ilitambulishwa katika michuano ya Klabu Bingwa Duniani Desemba mwaka 2016 na kufanyiwa majaribio Kombe la Shirikisho mwaka 2017 kabla ya Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino kusema itatumika kwenye fainali za Kombe la Dunia, ambapo kwa kuanzia ilianza fainali za mwaka 2018.
Kupitia teknolojia hiyo marefa wamekuwa katika nafasi ya kuagiza wasaidizi wao kurejea video za VAR kubaini uhalali na uharamu wa bao, mchezaji anayestahili kuadhibiwa baada ya makabiliano, uhalali na uharamu wa penalti na makosa madogo ambayo si rahisi kuonekana machoni mwa refa aliye katikati ya uwanja.
Shirikisho la soka duniani FIFA lilirasimisha teknolojia kwa malengo ya kutambua makosa na kurekebisha makosa au kumsaidia mwamuzi kufanya uamuzi, kubatilisha uamuzi, kubatilisha adhabu mbalimbali zikiwemo penati kumekuwa na mabadiliko ikiwemo kupunguza malalamiko.
Wapo wadau ambao wanapinga matumizi ya teknolojia hiyo kwa madai imekuja kuharibu ladha ya mpira. Kisa eti kitendo cha mwamuzi kusimamisha mechi na kwenda kutazama tukio lenye utata kupitia picha za video inatosha kuondoa ladha.
Kama yatajitokeza matukio 20 yenye utata uwanjani kwenye mechi husika ni wazi mwamuzi atalazimika kwenda kuyachungulia yote ili kufanya haki itendeke kwa walalamikaji.
Wingi wa matukio unatazamwa kuondoa ladha ya mechi kwa kitendo cha mwamuzi kusimamisha mchezo kila linapotokea tukio ambalo amehisi au kudokezwa si la kawaida.
Hoja nyingine ni kwamba teknolojia ya VAR imejaa ukatili wa hali juu. Rejea mechi ya Hispania dhidi ya Morocco kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi.
Teknolojia ya VAR imekuwa ikizinusuru timu mbalimbali kuchapwa au imepora ushindi wa baadhi ya timu ambazo zilitakiwa kusonga mbele kwenye mashindano.
Maamuzi ya VAR yanawakasirisha washabiki,viongozi na wachezaji kwa upande mmoja, lakini upande mwingine inachukuliwa kama mwokozi na kutoa haki katika mchezo wa soka.
Kocha mkongwe Jose Mourinho anasema “ni mwizi pekee ndiye anastahili kulalamika matumizi ya VAR”. Kumbe VAR inaweza kubadili matokeo ya mechi hata ikiwa imesalia sekunde moja kabla ya kipyenga cha kuashiria mchezo kuisha kupulizwa.
Wanaoitetea VAR wanasema imekuja kutenda haki kwa matukio mengi ambayo yalikuwa hayaonwi na waamuzi uwanjani.
Hoja hiyo inatetewa kwa nguvu kwamba mwamuzi wa kati pamoja na wasaidizi wake wawili wa pembeni bado walikuwa wakishindwa kuona baadhi ya matukio ambayo yanazinyima haki timu mbalimbali.
Ujio wa Teknolojia ya VAR wanautazama kama mkombozi mpya wa haki uwanjani ili kumfanya mwamuzi kuamuru mkwaju wa penalti, faulo au kutoa adhabu ya kadi pamoja na kubatilisha maamuzi aliyofanya awali.
Matamanio tangu awali kwa FIFA ni kuona teknolojia ya VAR inatumika duniani kote ili kuufanya mchezo huo uendelee kuheshima katika kutenda haki.
Kwamba familia ya soka inahitajika kuishi kulingana na wakati na wao wamejipanga kuwapatia waamuzi vifaa vyenye ubora ambavyo vitawawezesha kufanya kazi kwa urahisi na kutoa maamuzi yaliyo sahihi.
Hebu fikiria mechi za Ligi kuu Tanzania Bara ambazo zimekuwa zikiambatana na malalamiko mbalimbali ya waamuzi wa mchezo wa soka, je wakianza kutumia teknolojia hiyo itakuwaje?
Fikiria mechi kama ya watani wa jadi Simba na Yanga. Halafu VAR ipo tayari kuamua baadhi ya mambo kwenye mchezo huo. Unadhani mashabiki wataielewa kweli?
Je, mechi zitavunjika au zitaendelea? Je utamaduni wa kugoimea mechi utakuwepo? Itakuwa siku Yanga na Simba zikitumia VAR? Vipi mashabiki wa soka nchini wataikubali VAR ikiziumiza timu za za Lgi kuu Bara kama ambavyo wanashuhudia timu za Ulaya?
Kwa hulka za jazba za mashabiki wa timu za Yanga na Simba je mwamuzi gani mwenye ujasiri wa kuipa moja ya timu hizo penalti mbili mechi ikiwa bado mbichi kisa ameongozwa na VAR?
Teknolojia hiyo ina safari ndefu kwa soka la Tanzania. Mashabiki wa Simba na Yanga hawana uvumilivu na chochote.
Kweli mashabiki wa bongo wapo tayari kushuhudia teknolojia hiyo ikiamua mshindi wa mechi za Ligi Kuu Tanzania? Hivi tutaridhika na matokeo ambayo yataamuliwa na VAR au tutalalamikia kuwa teknolojia hiyo inahujumu?
Bila shaka siku VAR itakapotumika kuamua kwenye mchezo wa Yanga na Simba au mechi zingine za Ligi kuu Tanzania Bara ndipo itaonyesha utimamu na ustahimilivu wetu kwenye mchezo wa kandanda. Sheria inaumiza na kufurahisha, VAR hatuwezi kuikwepa katika maisha ya soka hapa nchini.