Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal amemwondosha mshambuliaji wake wa kati, Robin van Parsie katika jukumu la kupiga penati.
Van Gaal ametangaza uamuzi huo baada ya Mholanzi mwenzake kuwaangusha kwa penati yake kudakwa na kipa wa West Bromwich Albion, Boaz Myhill Jumamosi hii.
Van Persie (31) alibebeshwa majukumu ya kupiga penati kutokana na nahodha Wayne Rooney naye kukosa aliyopiga dhidi ya Liverpool, ukionekan andio mtindo wa kocha huyu aliyepata mafanikio makubwa na klabu kadhaa.
Kocha huyo aliweka msimamo huo baada ya kuulizwa iwapo Van Persie ataendelea na kazi ya kupiga penati zinapotokea, naye akajibu:
“Hapana. Sasa huyu yupo mwisho wa barabara. Ndio hivyo siku zote. Wayne Rooney naye alikosa (penati), kwa ukishakosa unakuwa chini tena.”
Katika mechi hiyo, West Brom waliwapiga United 1-0, ambapo penati ya Van Persie ilikuwa fursa muhimu kwa United kusawazisha, na kila mmoja alidhani angefunga, baada ya Saido Berahino kuunawa mpira.
Van Persie na Rooney ni kati ya washambuliaji tegemeo wa United, lakini walishindwa kufumania nyavu, ambapo Van Gaal alijaribu kuelekea mwisho wa kipindi cha pili kwa pamoja wawili hao na Radamel Falcao, Angel Di Maria, Juan Matta, Marouane Fellaini bila mafanikio ya kupata bao.