Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal amekana madai kwamba yeye ni dikteta na kwamba wachezaji wake hawana furaha naye.
Baadhi ya vyombo vya habari vimetoa taarifa za kuwapo msuguano baina yake na wachezaji, ikiwa ni pamoja na kwenye mazoezi na pia tabia yake ya kuwalaumu wachezaji.
Inadaiwa kwamba nahodha na msaidizi wake, Wayne Rooney na Michael Carrick walimwambia kwamba wachezaji hawakuwa na raha.
Hata hivyo, Van Gaal amedai kwamba madai hayo yanashitua kwa sababu wao ndio manahodha, akasema anachofanya ni kutuma ujumbe sahihi kwa wachezaji husika inapotakiwa.
Anasema kwamba walichofanya wachezaji hao wawili ni kwamba walitaka wamsaidie katika mawasiliano na kwamba kuna wachezaji wamemwendea kumwomba radhi kwa makosa waliyofanya.
Katika hatua nyingine, kipa wa klabu hiyo aliyekaribia kujiunga na Real Madrid kiangazi hiki, David De Gea amesaini mkataba mpya na Man United.
De Gea baada ya ndoto zake za kujiunga na Madrid kufa amesaini mkataba wa miaka minne na anatarajiwa kupewa nafasi ya kwanza golini Old Trafford, baada ya kukosa mechi nne za mwanzo.