Michuano ya Kombe la Dunia imezinduliwa nchini Brazil kwa sherehe za kukata na shoka.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na wacheza dansi 660 ambao walienzi asili ya nchi hiyo, watu wake na soka katika shoo ambayo ilifanyika jijini Sao Paulo kabla ya kuanza kwa mechi baina ya wenyeji na Croatia.
Hafla ilihitimishwa kwa tumbuizo la wimbo rasmi wa Kombe la Dunia lililofanywa na mwanamuziki mahiri Jennifer Lopez na mwanamuziki wa miondoko ya kufoka foka, Pitbull.
Michuano hiyo itakayochukua mwezi mmoja inashirikisha mataifa 32 na michezo itakayochezwa ni 64 kutafuta nani zaidi, timu zikitoka mabara yote ya dunia.
Wakati sherehe zikiendelea, kwingineko kulikuwa na maandamano ya watu ambao hawakupenda mashindano hayo yafanyike kwenye taifa hilo la samba, lakini polisi waliyasambaratisha kwa kufyatua mabomu ya kutoza machozi. Hayakuwa maandamano makubwa, kwani walikuwa watu kadiri ya 50 tu.
Uwanja unaofanyika mechi ya kwanza ambao unajulikana kwa jina la Arena de Sao Paulo unachukua watu 65,000, ambapo watumbuizaji walikuwa wamevalia kana kwamba ni miti, pengine katika kuenzi mazingira.