Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jakaya Mrisho Kikwete hii leo amezindua uwanja wa klabu ya Azam FC inayomilikiwa na makampuni ya Said Salim Bakhresa ya jijini Dar es Salam.
Rais Kikwete amezindua rasmi uwanja huo wa unaojulikana kwa jina la Azam Complex uliopo nje kidogo ya mji wa Dar es salam eneo la Mbande,huko Mbagala wilayani Temeke.
Azam ilianza kuutumia uwanja huo mapema mwaka 2011 mara baada ya kupata cheti cha FIFA chenye namba za usajili AF3243.1,ambacho kilithibitisha matumizi wa kiwanja hicho chenye nyasi bandia kutumika mpaka mwezi wa tatu mwaka 2015.
Uwanja huo umekuwa ukitumika kwa michezo mbalimbali ya ligi kuu soka Tanzania bara na pia michuano ya kombe la Kagame linaloshirikisha klabu bingwa Afrika Mashariki na kati pamoja na Michuano ya kombe la CECAFA Senior Challenge ambalo hushirikisha mataifa ya ukanda wa Afrika mashariki na Kati.
Klabu ya Azamu ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kwa miaka ya karibuni toka ipande daraja la ligi kuu soka nchini Tanzania misimu minne iliyopita ambapo mwaka huu kwa mara ya kwanza wamefanikiwa kushiriki michuano ya kimataifa ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita nyuma ya Simba.
Klabu hiyo inayonolewa na kocha Muingereza Stewart Jan Hall,Inakuwa klabu ya kwanza nchini Tanzania kumiliki uwanja wake wa kisasa ambao unawezesha zaidi ya mashabiki elfu 30 kukaa jukwaani kutama mpira.
Kwenye uwanja huo,Azam pia ina hosteli au mabwalo ya kukaa wachezaji ambapo wamejenga kituo maalumu cha kuendeleza timu zao za vijana maarufu kama Academy.
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya Said Salim Bakhresa,Bwana Aboubakari Bakhresa ameiambia Tanzania Sports kuwa,wanajivunia mafanikio ambayo wamekuwa nayo kwa siku za karibuni.
Azam Imekuwa na mchango mkubwa katika timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars ambayo wikiendi hii itakuwa uwanjani kucheza na Morocco katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki kombe la dunia hapo mwakani,ambapo kwenye kikosi cha Kim Poulsen kocha wa timu ya taifa ya Tanzania,Azam ina wachezaji sita kati ya 23 walioitwa kuunda timu hiyo.
Azam inatarajia kucheza mechi yao ya kimataifa majuma mawili yajayo nyumbani,watakapo wavaa BYC ya Liberia katika mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho raundi ya pili ambapo katika mchezo wa kwanza Azam iliichapa timu hiyo kwa mawili kwa moja.
Link ya uwanja wa Azam kuwa miongoni mwa viwanja vilivyothibitishwa na FIFA kwa Ubora wake.