Menu
in , , ,

Ushindi wa kwanza QPR

*Klabu za Manchester nazo roho kwatu

*Liverpool waloa kwa Aston Villa

Queen Park Rangers (QPR) wamepata ushindi wa kwanza msimu huu, wakati klabu za Manchester zikishinda na kubaki kileleni mwa ligi.

QPR wakicheza mechi ya nne chini ya kocha mpya, Harry Redknapp waliwafunga jirani zao wa magharibi mwa London, Fulham, mabao 2-1.

Adel Taarabt alikonga nyoyo za washabiki wa Loftus Road kwa mabao yake ya dakika ya 52 na 62, kabla ya Fulham kufuta machozi dakika ya 88.

Kama hawangeshinda Jumamosi hii, QPR wangevunja rekodi ya miaka 110 kwa timu kutoshinda mechi 17 tangu kuanza msimu wa ligi.

Redknapp aliteuliwa kuchukua nafasi ya kocha Mark Hughes ‘Sparky’ aliyeshindwa kupata ushindi, licha ya imani aliyoonesha kwake mmiliki, Tony Fernandes.

Kwa ushindi huo, QPR wameondoka mkiani, wakiwapa nafasi hiyo Reading. Hata hivyo, Reading wana mchezo mmoja mkononi, Jumatatu hii watakapocheza na Arsenal.

Manchester United na Manchester City wamebaki kileleni, United wakiacha pengo la pointi sita lililokuwapo.

Bao la kwanza la Robin Van Persie dhidi ya Sunderland lilikuwa na historia yake, kwani ni la 1,500 tangu kocha Alex Ferguson aanze kazi Old Trafford.

United wamebadilika tangu mchezo wa wiki iliyopita walipowachapa Chelsea, kwani wanashambulia na kupata mabao tangu awali, tofauti na mtindo waliokuwa nao kufungwa kisha kukomboa na kufunga mabao ya ushindi dakika za mwisho.

Wafungaji wengine wa United walikuwa Tom Cleverley na Wayne Rooney, katika mchezo ambao Man U walitawala. Bao la Sunderland lilifungwa na Fraizer Campbell.

Manchester City walirejea kwenye mwendo wa ushindi baada ya kupigwa na United wiki iliyopita, ambapo waliwanyuka Newcastle mabao 3-1 nyumbani kwao St James’ Park.

Sergio Aguero alifungua kijaluba cha mabao katika dakika ya 10 kabla ya Javi Garcia kufanya matokeo kusomeka 2-0 dakika ya 39.

Newcastle wanaofundishwa na Alan Pardew walikianza kipindi cha pili kwa nguvu, na Demba Ba alifunga kufuta machozi dakika ya 51 kabla ya Yaya Toure kuihitimisha suluba kwa kufunga bao la tatu dakika ya 78.

Liverpool walishitushwa wakiwa nyumbani, kwa kuchezeshwa kichapo cha mabao 3-1 na timu iliyotarajiwa kuwa nyepesi ya Aston Villa.

Christian Benteke alifunga mabao mawili, huku jingine likifungwa na Andreas Weimann, yote kipindi cha kwanza.

Liverpool walijifutia machozi kwa bao la nahodha wao, Steven Gerrard dakika ya 87. Watabaki wanajiuliza, kwani kocha Brendan Rodgers ndio kwanza amesema analenga kumaliza katika nafasi mbili za juu.

Norwich wameendelea kuchanua baada ya kuwafunga Wigan mabao 2-1, wakihitimisha mechi 10 bila kushindwa.

Nao Everton walioanza ligi kwa kasi walishikwa na Stoke City katika sare ya 1-1 na kubaki nafasi ya nne, lakini wanaweza kufurushwa hapo mzunguko huu wa 17 ukikamilika.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version