‘Ushahidi wa Terry ulikuwa wa kuchonga’
Sakata la kesi ya Nahodha wa Chelsea, John Terry limechukua sura mpya, ushahidi wake ukipondwa, huku mshirika wake Ashley Cole akitoa matusi.
Terry alimekwishaadhibiwa kukosa mechi nne na faini ya £220,000 kwa kumtukana kibaguzi Anton Ferdinand wa Queen Park Rangers (QPR).
Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England, alikuwa anafikiria kukata rufaa kupinga uamuzi wa jopo huru lililosikiliza mashitaka ya Chama cha Soka (FA) na utetezi wa Terry na Cole.
Wadau wengi wa soka, akiwamo Kocha Mkuu wa Manchester United, Alex Ferguson, wanaona Terry hana haja ya kupinga hukumu kwani adhabu ni ndogo tu.
Alichokuwa akisubiri Terry ni sababu za mashitaka ya FA dhidi yake kukubaliwa, utetezi wake kutupwa na hivyo kupewa adhabu hizo mbili anazoona si haki.
Mwenyewe anadai kwa vile Mahakama ya Hakimu Mkazi Westminster ilimsafisha, hapakuwa na sababu ya FA kuendeleza mashitaka yale yale kwake, ndipo akajiuzulu kuchezea taifa.
Kana kwamba hiyo haitoshi, baada ya FA kutoa sababu za hukumu na adhabu ya jopo hilo, Cole ambaye ni beki wa kushoto wa Chelsea, taifa na swahiba mkubwa wa Terry amewatukana FA.
Katika mawasiliano kupitia mtandao wa jamii wa tweeter, Cole aliwatukana maofisa wa FA, akidai ni genge fulani aliloliwekea tusi la nguoni.
Hata hivyo baadaye, pengine baada ya kushauriwa, Cole ameomba radhi kwa kauli yake hiyo, akidai alitoka mazoezini, akatazama televisheni haraka, akaona maandishi kuhusu uamuzi wa jopo kuhusu ushahidi wake, naye akajibu akiwa bado na jazba.
Baadhi ya sababu za kutupilia mbali utetezi wa Terry na ushahidi wa Cole kuhusu alichosikia Anton akisema dhidi ya Terry, FA inasema ni kama umechongwa vile.
Kile jopo la wataalamu lilichoona katika kesi hiyo kimeelezwa kwa kina kwenye waraka wa kurasa 63 uliotolewa Ijumaa asubuhi.
Kwamba hapakuwa na mantiki katika maelezo ya jinsi na sababu za Terry kutumia maneno ya kibaguzi dhidi ya Anton.
Pia hapakuonekana kuwa na ukweli wowote katika utetezi kwa ujumla, kwa sababu haukuwa na mtiririko wa kawaida, bali kubuni na kupachika maneno ili kukidhi matakwa ya aliyekuwa akitetewa na watetezi wake.
Terry anakiri kutumia neno linalohusiana na rangi au asili ya Anton, lakini madai yake ni kwamba alikuwa anamuuliza beki huyo wa QPR ikiwa alidhani alitumia neno baya dhidi yake.
FA katika ripoti yake, hata hivyo, inasema Terry alitumia neno hilo kama tusi. Kwamba tume ilifikia uamuzi wake na kutoa adhabu kwa vile ina mamlaka ya kutumia uzoefu wake wa maisha na watu kufikia uamuzi kuhusu tabia ya mtu kwa wengine.
Wanajopo walitazama mkanda wa video katika eneo hilo muhimu Terry anapomsemesha Anton, ambapo anadaiwa kuwa mwenye tabasamu awali.
Hata hivyo, baadaye uso wake kubadilika na kumtazama Anton kama kitu kisicho na thamani, kwa dhihaka na kicheko cha bezo.
“Hakuna mahali popote, tabia yake (Terry) kwa mwonekano wa uso wake ilikuwa kama ya mtu aliyekuwa anasononeka, aliyeumia au hata kuonesha mshangao,” taarifa ya FA inasema.
Jopo lilijiridhisha pasipo shaka kwamba utetezi wa Adhabu yake imekuwa ndogo kuliko ya Luis Suarez wa Liverpool aliyefungiwa mechi nane kwa kumtukana Patrice Evra wa Manchester United, kwa sababu Terry alitukana mara moja wakati Suarez alitamka neno la kibaguzi mara saba.
Mwanasheria wa FA, Laidlaw anamchambua Terry na tabia yake, akisema haaminiki.
Anakumbushia alivyopewa kadi nyekundu kwa kumpiga Alexis Sanchez wa Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, kisha akadai haikuwa makusudi, wakati kila mmoja aliona alivyofanya.