*Arsenal wamtwaa Ozil, Madrid wampata Bale
*Mourinho awatoa kwa mkopo Lukaku na Moses
Dirisha la usajili wa msimu wa kiangazi limefungwa, huku pauni milioni 630 zikitumika kusajili nyota.
Arsenal waliokuwa wakisuasua kufanya usajili wamemnasa kiungo mahiri wa Real Madrid, Mesut Ozil wakati miamba hao wa Hispania wakiwabomoa Tottenham Hotspur kwa kumchukua Gareth Bale.
Bale ameweka rekodi mpya ya dunia, kwa sababu amenunuliwa kwa pauni milioni 85.3 na ushee, akivunja rekodi ya Cristiano Ronaldo aliyeuzwa huko na Manchester United kwa pauni milioni 80.
Ozil kwa upande mwingine, anakuwa faraja kwa washabiki wa Arsenal ambao hawakuwa wametumia hata senti tano hadi siku ya mwisho ya usajili.
Mjerumani huyo amesajiliwa kwa pauni milioni 42.4, akivunja rekodi ya Arsene Wenger katika kusajili.
Ozil, mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani anaingia Emirates akisema amefurahi kuja kucheza Ligi Kuu ya England na kwamba kama mchezaji kijana, atapata changamoto na fursa za kujijenga zaidi kisoka.
Kocha David Moyes wa Manchester United naye ameambulia nusu ya kile alichokitaka kwenye klabu yake ya zamani ya Everton, kwa kumsajili Mbelgiji Marouane Fellaini kwa Pauni milioni 27.5.
Hata hivyo, Kocha aliyemrithi huko Everton, Roberto Martinez amemkatalia kumchukua mlinzi mahiri wa kimataifa wa Uingereza, Leighton Banes.
Arsenal ambao Jumapili waliwafunga mahasimu wao wa kaskazini mwa London, wanajieweka katika hali nzuri kwa kumwongeza Ozil (24), ambapo pia wamemrejesha kiungo wao wa zamani, Mathieu Flamini na kumsajili mshambuliaji wa Auxerre, Yaya Sanogo (20).
Kwa upande mwingine, kocha Jose Mourinho wa Chelsea amewatoa kwa mkopo Romelu Lukaku kwenda Everton na Victor Moses kwenda Liverpool.
Msimu uliopita Lukaku alikuwa kwa mkopo West Bromwich Albion, na inavyoonekana ametolewa ili kumwepusha na benchi, hasa baada ya Chelsea kumsajili Samuel Eto’o.
Liverpool wameendeleza kasi ya kufanya mageuzi kwenye klabu yao kwa kusajili viungo wa kati, Mamadou Sakho na Tiago Ilori kwa pauni milioni 25 jumla.
Katika siku ya mwisho ya usajili pekee, pauni milioni 140 zilitumiwa nchini England, kufikisha jumla ya pauni 630 kwa msimu huu, rekodi iliyovunja ile ya msimu uliopita walipotumia pauni milioni 500.
EPL wametumia pauni milioni 400 zaidi katika manunuzi kuliko mapato yaliyotokana na mauzo ya wachezaji, na kuyazidi matumizi ya klabu za ligi za Hispania (La Liga) na Italia (Serie A) ambayo ni pauni milioni 335, wakati Ligue 1 ya Ufaransa ilitumia £315m na Bundesliga ya Ujerumani kutafuna £230m.
Matumizi ya EPL yameongezeka kwa asilimia 29, lakini klabu zinaelekea kufaidi, kwa sababu matangazo ya televisheni kwa klabu hizo yatazipatia ziada ya mapato ya pauni milioni 600.
Aston Villa wamemsajili mpachika mabao wa Jamhuri ya Czech, Libor Kozak wakati
West Brom wamemnasa Stephane Sessegnon kutoka Sunderland na Victor Anichebe wa Everton.
Spurs ndiyo klabu waliotumia fedha nyingi zaidi msimu huu wa usajili, ambapo waliwekeza pauni milioni 105 kununua wachezaji saba kujiandaa kuziba pengo la Gareth Bale, ambaye peke yake amewaingizia pauni milioni 85.3.
David Moyes ameshindwa katika mkakati wake wa kumsajili kiungo wa Athletic Bilbao, Ander Herrera kabla ya msimu kufungwa na kuachwa bila majibu juu ya kumchukua kwa mkopo beki wa kushoto wa Real Madrid, Fabio Coentrao.
Everton wamemsajili pia Gareth Barry wa Manchester City kwa mkopo na James McCarthy wa Wigan
Mchezaji yota wa Italia, Fabio Borini amejiunga na Sunderland kwa mkopo kutoka Liverpool pamoja na Andrea Dossena, 31 anayetoka Napoli.
Cardiff City waliopanda daraja msimu huu wamemsajili mshambuliaji wa West Brom aliyetaka kuhama tangu Januari, Peter Odemwingie.