Menu
in , , , ,

Usajili wa Kiangazi EPL 2024:

Sterling na Arteta walipokuwa City Pamoja

Mwisho wa enzi za matumizi ya hovyo?

Hakuna wakati mzuri kwa wafuatiliaji na wapenda soka kama wakati wa dirisha la usajili. Ni wakati wenye hisia, wakifuatilia timu zao wanazoshabikia na kuzifuatilia, zinamsajili nani na kumuacha nani, kwa lengo la kuboresha vikosi.

Na hakuna nyakati nzuri zaidi kama zile saa za mwisho za usajili hasa za dirisha la usajili la majira ya kiangazi la moja ya ligi zinazofuatiliwa zaidi duniani, ligi kuu ya England (EPL). Dirisha la mwaka huu la EPL lililofungwa hivi karibuni lilileta msisimko wa ajabu, wachezaji 20 wakiwemo wenye majina makubwa kuhama ama kuhamia kwenye klabu za Ligi Kuu ya England. Nyota kama Manuel Ugarte, Jadon Sancho, Raheem Sterling, Aaron Ramsdale, Eddie Nketiah, na James Ward-Prowse walihama vilabu vyao na kuhamia vilabu vipya kutafuta changamoto mpya. 

Lilikuwa dirisha lenye utofauti mkubwa ikilinganishwa na madirisha ya usajili ya miaka iliyopita, hasa kutokana na ‘kihoro’ cha matumizi ya fedha kinachotokana na mkazo wa sheria ya ukomo wa matumizi ya fedha (FFF-Financial Pair Play) inayosisitiza usawa katika mapato na matumizi ya fedha chini ya Shirikisho la soka Ulaya (UEFA) na kanuni za faida na uendelevu (PSR). Utofauti huu unaletwa zaidi na namna timu zilivyofanya  usajili, matumizi na aina ya wachezaji. Hivyo Makala hii inachambua jinsi dirisha hili lilivyoathiri usajili wa timu kubwa za Ulaya, kuangalia matumizi na mikakati yao, tukilinganisha na madirisha ya usajili ya ligi nyingine kubwa barani Ulaya, ikihoji usajili wa dirisha la kiangazi mwaka huu ni mwisho wa enzi za matumizi ya hovyo?

Usajili wa ‘Mkono wa birika’

Dirisha la usajili la 2024 lilijaa hekaheka nyingi hasa katika saa za mwisho, lakini hali hii haikuwa inaakisi kipindi kizima cha usajili. Ni kama ulikuwa usajili wa ‘mkono wa birika’ kwa maana ya usajili wa kibahili na uangalifu mkubwa. Ingawa jumla ya matumizi ya klabu za Ligi Kuu ya England kwenye usajili mwaka huu yalifikia karibu £1.98 billion,  lakini yalikuwa ya chini kwa asilimia 16 ikilinganishwa na rekodi ya matumizi ya usajili katika dirisha kama hili kwa mwaka uuliopita (2023). 

Klabu kama Chelsea na Manchester United ziliongoza kwa matumizi makubwa, kwa pamoja zikitumia karibu £400 milioni, lakini vilabu vingine vikubwa kama Manchester City, Liverpool, na Arsenal vilifanya matumizi kwa kiasi na kwa tahadhari. City, bingwa mtetezi wa Ligi Kuu, yenyewe ilitumia pesa kidogo, kiasi ambacho kilikuwa chini, ikizidiwa na timu kama Birmingham City.

Wako wanaodhani, pengine kuwa na kikosi bora, kipana kila idara na chenye ushindani, imefanya klabu hiyo kutumia fedha kiduchu katika dirisha la mwaka huu. Lakini wako wanaodhani kwamba, Sheria na kanuzi za matumizi ya fedha za FFF na PSR zimekuwa ‘zimwi’ kwenye shughuli za usajili za klabu hiyo.

City inakabiliwa na mashtaka 115 ya madai ya kuvunja kanuni ya ukomo wa matumizi ya fedha (FFF), madai ambayo yataanza kusikilizwa na jopo huru baadae mwezi huu (Septemba) yanayoweza kuchukua miezi miwili, kabla ya maamuzi ya mwisho yanayotarajiwa kutolewa kabla msimu huu wa ligi kuu kumalizika mwakani, 2025.

Mashtaka hayo yanahusisha kipindi cha misimu 14, kuanzia msimu wa 2009-10, na yanajumuisha makosa 54 ya kushindwa kutoa taarifa sahihi, makosa 14 ya kushindwa kutoa maelezo sahihi kuhusu malipo ya wachezaji na makocha, makosa 7 ya kukiuka kanuni za faida na uendelevu (PSR) za Ligi Kuu ya England, makosa 5 ya kushindwa kutii kanuni za UEFA ikiwa ni pamoja na sheria za matumizi ya fedha (FFP), na makosa 35 ya kushindwa kushirikiana na timu ya uchunguzi ya Ligi Kuu ya England tangu mwaka 2018. 

Ingawa City inakanusha madai hayo ya kukiuka kanuni, adhabu ya kukatwa alama (pointi), kutozwa faini, kusimamishwa kushiriki ligi/michuano na kushushwa daraja ni miongoni mwa adhabu zinatotambulika kikanuni, ambazo zinatia hofu si kwa City tu inayokabiliwa na mashtaka hayo, lakini hata vilabu vingine vikihofu kukumbwa na rungu la aina hiyo, ambalo lilishawahi kuvikumba vilabu kadhaa vya England na  Ulaya.

Everton ni mfano wa hivi karibuni, ambapo ilikatwa alama 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England kwa msimu uliomalizika wa 2023-24, kutokana na kukiuka sheria za PSR, 2019. Hakuna aliyesahau kilichowakumba Paris Saint-Germain (PSG) mwaka 2014, AC Milan (2018), Inter Milan (2015), na Galatasaray (2016). Kanuni hizi za PSR na FFF zinatambulika na Shirikisho la soka duniani (FIFA) na lile la Ulaya (UEFA), na zinatumika kwa mahitaji, mazingira na muktadha wa ligi husika.

Tumeshuhudia pia mwaka 2023, Juventus ililimwa alama 10 kwenye ligi kuu ya Italia (Serie A) kwa kutoa taarifa za kifedha za udanganyifu, hasa juu ya usajili wa wachezaji na malipo ya mishahara huku Barcelona wakizuiwa kusajili wachezaji wapya kwenye dirisha la usajili la Januari kutokana na matatizo ya kifedha yanayohusiana na kanuni za FFP za La Liga. Kwa hivyo, matumizi ya kawaida ya dirisha la sasa kwa kiasi fulani yamejengwa na kanuni na sheria hizi, ambazo makali yake ymaendelea kuonekana. 

Licha ya vilabu vitatu vilivyopanda daraja vya Ipswich Town, Southampton, na Leicester City kujiamini na kutumia karibu £300 milioni kuboresha vikosi vyao, hata hivyo, vilabu vingi ndani ya Ligi Kuu ya England vimesajili kwa tahadhari na kwa mkono wa birika. Kwa ujumla, vilabu vingi vya England vilikuwa na matumizi ya chini ukilinganisha na misimu iliyopita. Kwa mfano tovuti ya Transfermarkt inataja Vilabu sita kupata fedha zaidi ya zile zilizotumika kwenye kusajili. Kwa mujibu wa takwimu za tovuti hivyo,  vilabu vingine sita vilikuwa na matumizi ya chini ya pauni £32milion. Aidha kati ya vilabu 17  vilivyonufaika na fedha za haki ya matangazo ya Televisheni kwa msimu wa 2023-24,  vilabu 13 vilikuwa na matumizi ya chini kwa msimu huu wa kiangazi ikilinganishwa na msimu uliopita. 

Tanzania Sports

Kwa ufupi, baada ya kuzingatia mapato na matumizi (hasa kutokana na mauzo ya wachezaji), matumizi ya jumla ya vilabu 20 vya ligi kuu ya England yalikuwa £490 milioni chini kuliko kipindi cha usajili kama hichi kwa mwaka uliopita, 2023. Baadhi ya vilabu vilivyopunguza matumizi yao ni vile vilivyokuwa karibu kuvunja kanuni za PSR, kama Newcastle United na Everton, lakini pia vilikuwepo vingine vilivyoonekana kuridhika na hali zao za kifedha. City, Arsenal, na Liverpool, vilabu vilivyomaliza kwenye nafasi tatu za juu katika msimamo wa msimu uliopita wa Ligi kuu, vilifanya usajili kwa ‘machale’, City, ikimsajili Savinho kutoka Troyes. Pengine usajili wa aina hii, umeathiri soko huku uhamisho wa Dominic Solanke wa £65 milioni kutoka Bournemouth kwenda Tottenham Hotspur ukibaki kuwa ghali zaidi kwenye dirisha lililofungwa hivi karibuni. Hakukuwa na usajili mkubwa kama wa Declan Rice na Moises Caicedo, viungo wawili waliotikisa dirisha la majira ya kiangazi lililopita la EPL wakigharimu zaidi ya £100 milioni kila mmoja. Usajili ambao umeleta msisimuko msisimko mkubwa msimu huu.

Hata hivyo usajili wa wachezaji hao wawili umeonekana kuwa na athari katika usajili wa dirisha la mwaka huu, ikiwa ni mwaka umepita sasa. Brighton & Hove Albion, iliyomuuza Caicedo kwenda Chelsea ikitengeneza faida ya £85million kweye soko la usajili msimu uliopita, imenufaika zaidi na mauzo hayo yaliyofanya kutumia pesa zaidi katika dirisha la msimu huu. Katika dirisha la mwaka huu timu hiyo imeongoza duniani kwa kumwaga pesa za usajili ikitumia  £200milioni kwenye usajili, ikiwasajili nyota kama Mats Wieffer, Yankuba Minteh and Matt O’Riley. 

West Ham United, iliyomuuza Rice miezi 12 iliyopita yenyewe iko 10 bora ya timu zilizomwaga pesa nyingi za usajili, ikishika nafasi ya 7 duniani kwa kutumia £83million. 

Ipswich, ambayo imetumia zaidi ya £100 milioni katika juhudi za kuwa washindani na sio vibonde katika ligi kuu msimu huu baada ya kuwa nje ya ligi hiyo kwa miaka 22, ni miongoni mwa vilabu vilivyotumia fedha nyingi katika dirisha la sasa, ikienda sambamba na vilabu vikubwa kama Manchester United, Napoli, Lyon, na Paris Saint-Germain.

Chelsea ambayo ilitumia kiasi kikubwa zaidi kwa jumla (kwa mara ya tatu katika madirisha manne ya usajili chini ya utawala wa Todd Boehly-Clearlake), lakini matumizi hayo yalipunguzwa na mauzo makubwa msimu huu yanayofikia £147 milioni. Hakuna klabu duniani iliyoingiza kiwango hicho cha mapato msimu huu, ingawa Leeds United, waliochapwa na Southampton katika fainali ya play-off ya Championship mwezi Mei, wanakaribia kiwango hicho kwa kuingiza £137 milioni mauzo ya wachezaji. Manchester United na Tottenham walimaliza msimu wa kiangazi wakiwa na matumizi makubwa zaidi kuliko Chelsea, zikiwa na matumizi ya jumla ya £219 milioni.

Kuwekeza kwa Vijana muarobaini wa usajili wa ‘mkono wa birika?

Jambo lingine lililoonekana katika dirisha la sasa ni muelekeo wa klabu za Ligi Kuu kusajili wachezaji vijana. Kati ya wachezaji 37 wenye thamani ya zaidi ya £20 milioni, waliohusika kwenye usajili EPL msimu huu, 31 walikuwa na umri wa miaka 24 au chini. Klabu nyingi, kama Manchester United, Spurs, na Chelsea, zilifanya kazi kubwa kuboresha vikosi vyao kwa kusajili wachezaji vijana wenye uwezo unaoweza kudumu kwa muda mrefu. Aidha, idadi ndogo ya wachezaji wenye umri wa miaka 30 au zaidi walihusishwa na usajili. Klabu kubwa kama Manchester United walishindwa kuachana na wachezaji wenye umri mkubwa kama Casemiro kutokana na mishahara yao mikubwa, na hivyo kubaki na mzigo wa kifedha usiohitajika.

Usajili EPL na Ligi zingine kubwa Ulaya

Ikiwa England bado inaonekana kuwa na nguvu kubwa katika soko la usajili, matumizi ya ligi nyingine kubwa za Ulaya yalikuwa  ya kawaida pia. Hispania (La Liga), Italia (Serie A), Ujerumani (Bundesliga), na Ufaransa (Ligue 1) zilijikuta katika hali ngumu kifedha, huku timu nyingi zikipunguza matumizi yao. La Liga, kwa mfano, ilishuhudia klabu nyingi kama Barcelona na Atletico Madrid zikilenga kupunguza mishahara badala ya kufanya usajili mkubwa.

Atletico Madrid ilifanya usajili mkubwa kwa kumsajili Julian Alvarez kutoka Manchester City kwa kiasi kinachoweza kufikia £82 milioni, lakini usajili huu ulionekana kuwa wa kipekee katika ligi hiyo. Huko Italia, timu kama Napoli na Inter Milan zilifanya usajili wa kimaslahi zaidi, wakiepuka matumizi makubwa.

Matumizi ya tahadhari katika dirisha la usajili la kiangazi la 2024 limeleta mwamko mpya wa kifedha katika Ligi Kuu ya England na hata Ulaya kwa ujumla. Ingawa bado kuna matumizi makubwa, mwelekeo wa kupunguza matumizi kwa baadhi ya timu umeonyesha mabadiliko makubwa. Klabu zinakuwa makini zaidi na kanuni za PSR na FFF na kuangalia njia za kuboresha vikosi vyao bila kulazimisha kufanya matumizi makubwa.

Miezi ijayo, itakuwa ya kuvutia kuona jinsi klabu hizi zitakavyokabiliana na changamoto za kifedha na jinsi mabadiliko haya yanaweza kuathiri dirisha la usajili la mwezi Januari, 2025. Wakati Ligi Kuu ya England inabaki kuwa na nguvu za kifedha, ni wazi kuwa enzi za matumizi ya hovyo zinaweza kuwa zinakaribia mwisho wake.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version