*Moyes atakiwa akawanoe mabingwa wa Scotland
*Balotelli kurudi EPL, QPR wawataka Rio, Lampard
WAKATI dirisha la usajili wa majira ya kiangazi likiwa wazi hadi Agosti, timu zimeanza kupigana vikumbo kutafuta wachezaji zinaowataka, huku makocha pia wakitafutwa.
Kwa kuanzia, aliyekuwa Kocha wa Manchester United David Moyes aliyefukuzwa kazi Mei hii, anatakiwa kwenda kujiunga na klabu ya Celtic ambao ni mabingwa wa Scotland. Bosi wa klabu hiyo, Neil Lennon aliachia ngazi baada ya kuwapa ubingwa.
Mmiliki wa Celtic, kwa maana ya mwenye hisa nyingi zaidi, Dermot Desmond alikuwa anatarajiwa kufanya uamuzi wa mwisho wikiendi hii juu ya kufanya mazungumzo na Moyes kwa ajili ya kazi hiyo. Moyes ni raia wa nchi hiyo inayounda Uingereza.
Kocha wa zamani wa Cardiff, Malky Mackay aliyefukuzwa kazi anafikiriwa pia kwa nafasi hiyo.
BALOTELLI KURUDI KWA KISHINDO EPL
Mpachika mabao wa Italia, Mario Balotelli anaelezwa kufikiria kurudi tena katika Ligi Kuu ya England (EPL) ambako alichezea Manchester City kabla ya kuuzwa na Mwitaliano mwenzake, Roberto Mancini kwa klabu ya ACMilan.
Balotelli anadaiwa kwamba haridhiki na mazingira ya Italia ambako amekabiliana mara kadhaa na vitendo vya ubaguzi wa rangi kutoka kwa washabiki, hata majuzi wakati akifanya mazoezi na timu ya taifa.
Balotelli ni mfungaji mzuri na mtaalamu wa penati lakini tatizo lake limekuwa nidhamu ndani na nje ya uwanja, nalo lilimfanya akakosana na kocha Mancini ambaye naye alikuja kufukuzwa kabla ya kwenda kujiunga na Galatasaray ya Uturuki.
Kuna habari kwamba klabu za Arsenal, Chelsea na Liverpool zinafikiria kumnyakua mpachika mabao huyo ili kujiimarisha kwenye safu za ushambuliaji tayari kwa ajili ya ligi kuu msimu ujao.
Wakati Arsenal wameshaanza mazungumzo na Real Madrid kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wao wa kati, Karim Benzema, wanasema kwamba watazungumza pia na ‘watu’ wa Balotelli. Liverpool watamfikiria toto tundu huyo ikiwa Real Madrid au Barcelona watafanikiwa kumchukua Luis Suarez.
QPR YA REDKNAPP YATAKA NYOTA WAKONGWE
Baada ya kupanda daraja na kurejea EPL, Kocha wa Queen Park Rangers (QPR), Harry Redknapp anaonekana kutaka kuchukua wakongwe wanaoachwa na klabu kubwa ili wakakipige Loftus Road.
Tayari amesema angependa kumsajili beki Rio Ferdinand aliyekuwa Manchester United, Frank Lampard (mpwa wake) na Ashley Cole wa Chelsea, Gareth Barry anayecheza Everton kwa mkopo kutoka Man City na Joe Cole anayekipiga West Ham United. Anataka pia kuhakikisha Loic Remy aliyekwenda kwa mkopo Newcastle anabaki Loftus Road.
Redknapp anaamini kwamba ni rahisi zaidi kuwachukua nyota hao ambao mikataba imeisha hivyo awasajili bure hata kama watataka mishahara mikubwa kwani ndiyo njia bora zaidi ya kuimarisha klabu hiyo na kuhakikisha inabaki ligi kuu.
Ashley Cole ambaye ameshaachwa na Chelsea anataka kujiunga na klabu inayocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa walau mkataba wa miaka miwili, ambapo inaelezwa Liverpool na Man City wameonesha kumtaka, lakini pia Tottenham Hotspur wanataka kumchukua. Anaweza pia kwenda Monaco watakaoshiriki UCL msimu ujao.
Katika hatua nyingine, Patrice Evra wa Manchester United ameokoka panga la kocha Louis van Gaal baada ya kupewa mkataba wa mwaka mmoja. Ryan Giggs alikuwa amependekeza Evra na Rio waongezwe mkataba na yeye mwenyewe alitaka kuendelea kucheza, lakini akateuliwa kuwa kocha msaidizi.