*Rooney autaka unahodha lakini…
Kazi ya kuijenga upya Manchester United inaelekea kuwa bado ni mbichi, kwani habari za kusajiliwa kwa Toni Kroos na dili kutengenezwa kumnasa Arjen Robben wote wa Bayern Munich zimekanushwa.
Iliripotiwa jana kwamba tayari Man U walishakubaliana juu ya usajili wa Kroos kwa pauni milioni 20 na kwamba bosi mpya, Lous van Gaal alikuwa akisonga mbele kumnasa Arjen Robben anayetoka nchini mwake Uholanzi kwa pauni milioni 27.
Kroos (24) mwenyewe amesema Ijumaa hii kwamba hajapata kuwa na nia ya kujiunga na United na kuwa msimu ujao ataendelea kuitumikia klabu yake ya Bayern. Mashabiki wa United walipata tumaini zaidi baada ya Bayern kutangaza Alhamisi kwamba wasingemwongezea Kroos mshahara.
Mjerumani huyo alisema kwamba pamekuwa na tetesi nyingi juu yake na Man U, lakini anabaki nyumbani na kwa sasa anajiandaa na michuano ya Kombe la Dunia inayoanza Juni 12 nchini Brazil.
Haijajulikana ikiwa kuna ukweli juu ya uwezekano wa Man U kumpata Robben ambaye Van Gaal ndiye alimsajili hapo klabuni Bayern alipokuwa kocha.
ROONEY ATAKA KUMRITHI VIDIC UNAHODHA
Katika hatua nyingine, mshambuliaji Wayne Rooney amesema wazi kwamba angependa kurithi mikoba ya unahodha iliyoachwa na beki wa kati, Nemanja Vidic aliyemaliza mkataba na anahamia Inter Milan.
Hata hivyo, pamekuwa na taarifa tofauti kwamba Van Gaal anapanga kumpa unahodha raia mwenzake wa Uholanzi, Robin van Persie ambaye pia alikuwa nahodha Arsenal kabla ya kuondoka misimu miwili iliyopita.
Rooney amesema hatakuwa na kinyongo ikiwa Mdachi huyo atapewa unahodha na atafanya naye kazi kwa karibu. Van Persie pia amempora Rooney nafasi ya kwanza kwenye ushambuliaji pale mbele tangu enzi za Sir Alex Ferguson kisha David Moyes aliyefukuzwa kazi.
Nahodha msaidizi ni Patrice Evra ambaye kuna uwezekano wa kuondoka klabuni hapo kwani mkataba wake unamalizika na haonekani kuwa na kiwango kinachotakiwa Old Trafford kwa ajili ya kurudisha heshima iliyoporomoka.
“Ninautaka unahodha. Nimepata kushika wadhifa huo mara chache kwa muda na sasa nikipewa moja kwa moja litakuwa jambo kubwa. Nahisi nipo tayari kuwa nahodha lakini ni uamuzi wa kocha kuchagua. Akimchagua mtu mwingine, basi ukweli ni kwamab sina tatizo na hilo. Nitaheshimu uamuzi.
” Robin (van Persie) ni nahodha wa timu ya taifa kwao, amekuwa nahodha Arsenal na akipewa tena Manchester United naamini atafanya kazi nzuri,” akasema Rooney aliye Ureno kwenye kambi ya England kujiandaa kwa Kombe la Dunia nchini Brazil.
RVP ndiye nahodha wa Uholanzi na amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kukabidhiwa uongozi. Kuteuliwa kwa raia mwenzake kuwa bosi hapo kunampa ahueni, kwani chini ya Moyes ilishaanza kuelezwa kwamba hawakuelewana na alikuwa akifikiria kurudi Arsenal.