*Siri za utumiaji dawa zimeumbua wengi
*Wamo washirika, wapinzani wake wakuu
Usain Bolt ni mwanariadha safi, anayeheshimika na mashuhuri sana, kutokana na kasi yake isiyo ya kawaida.
Ameibuka kidedea katika mashindano mengi na rekodi yake katika mbio haijavunjwa. Hajapata kashfa yoyote ya kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Rekodi yake haina utata hata kidogo hadi sasa, zaidi ya wananchi wenzake wa Jamaica, weusi na ulimwengu wa riadha kwa ujumla kumjivunia.
Hata hivyo, wapo wengine maarufu kadhaa kabla yake waliosifika duniani kote kwa uwezo wao mkubwa, na imechukua muda mrefu kubainika kwamba walikuwa wakidanganya, kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku.
Wapo wanaume tisa katika historia waliofanikiwa kukamilisha mbio za mita 100 chini ya sekunde 9.8. wa kwanza ilikuwa miaka 25 iliyopita, Ben Johnson, aliyekimbia sekunde 9.79 na kushinda Fainali ya Olimpiki jijini Seoul, Korea Kusini 1988.
Kilichokuja kumpata baadaye kimefuta mazuri yote, amekuwa kwenye orodha ya watumia dawa za kuongeza nguvu, kabla ya kuja mwenye kashfa mwingine, Lance Armstrong hajampa nafasi, kutokana na wingi wa fedha zake.
Ilichukua zaidi ya muongo mmoja kwa rekodi yake hiyo kuja kuvunjwa, nayo ilivunjwa na Maurice Greene aliyekimbia kwa sekunde 9.79 na huyu hajapata kutiwa hatiani kwa kutumia dawa hizo.
Alikiri siku moja, hata hivyo kumlipa mrusha diski wa mexico, Angel Guillermo Heredia dola 10,000, fedha ambazo raia huyo wa Mexico anadai zilikuwa malipo kwa dawaza kuongeza nguvu, lakini Greene anakana, akisema zilikuwa kwa ajili ya vifaa vya mazoezi kwenye timu yake.
Bingwa wa Olimpiki mwaka 2004, Justin Gatlin alikimbia kwa sekunde 9.79, lakini tunajua kwamba mwaka 2001 alipigwa marufuku kushiriki michezo miwili baada ya kutiwa hatiani kwa kutumia dawa aina ya amphetamines.
Miaka miwili tu baadaye alikamatwa tena na kuzuiwa kushiriki mashindano kwa miaka minne, pale ilipobainika alitumia dawa aina ya testosterone. Alirejea uwanjani, akakimbia na majira yaliyopita ya kiangazi alitwaa medali ya shaba jijini London.
Mfukuza upepo mwingine aliyejipatia umaarufu ni Tim Montgomery aliyekimbia kwa sekunde 9.78, lakini akaja kukiri alitumia testosterone na nyingine za kukuza homoni ya mwanadamu, hivyo rekodi yake hiyo ya kukimbia imefutiliwa mbali.
Mjamaica Nesta Carter (27) aliweka rekodi pia kwa kukimbia kwa sekunde 9.78, na alitwaa medali ya dhahabu mara mbili katika mbio za mita 4 x 100 kwenye Olimpiki na alikuwa mshirika wa Asafa Powell kwenye mazoezi.
Tukija sasa kwa Asafa Powell, aliweka rekodi ya sekunde 9.72, lakini vipimo vikaja kumuumbua kwamba alitumia dawa za kuongeza nguvu, japokuwa mwenyewe anasema hakujua kama ametumia chochote kilichokatazwa.
Tyson Gay alikuja na rekodi ya sekunde 9.69 katika mbio hizo hizo, lakini juzi tu amekiri kwamba vipimo vinaonesha ametumia dawa hizo zilizokatazwa.
Yohan Blake alikimbia kwa sekunde 9.69, lakini akaumbuka baada ya vipimo kuonesha kwamba alitumia 4-Methyl-2-hexanamine katika Ubingwa wa Dunia wa 2009.
Alichotumia hakizuiliwa na Shirika la Kupambana na Dawa za Kuongeza Nguvu Duniani, lakini vipimo hivyo vilisababisha Chama cha Riadha cha Jamaica kumwondoa kumpiga marufuku kwa miezi mitatu. Walikuwa wanariadha wanne waliotiwa hatiani.
Tukirudi kwa Usain Bolt, hadi sasa ni bingwa, yupo kwenye kilele cha mafanikio yake, na washabiki wa mchezo huo wanatakiwa waendelee kuamini kwamba hana matatizo wala hajapata kutumia dawa hizo.
Ameweza kukimbia kwa kasi ya kumi moja la sekunde zaidi ya wapinzani wake wote, wengi wao wakiwa wamechafuliwa kwa namna moja au nyingine na kashfa za kuongeza nguvu.
Kumi hilo la sekunde linaweza kuwa rekodi ya muda mrefu katika mbio za mita 100. Sasa, kuna mawili, tuamini kwamba wapinzani wa Bolt uwanjani wanatumia dawa ili waifikie kasi yake na wanashindwa, au tumtilie shaka Bolt mwenyewe, vipi awe na kasi ya aina hiyo.
Kati ya waliotiwa hatiani kwa kashfa hizo ni wanatimu wenzake na rafikize katika emdani ya kimataifa.
Nadharia moja inaacha maswali; vipi hadhi ya Lance Armstrong ilibaki safi kwa miaka yote hiyo, wakati wenzake kama Tyler Hamilton na Floyd Landis walioendesha baiskeli naye kwenye mashindano ya Tour de France hawakuchukua muda kubainika na kutajwa?
Hata hivyo, pamoja na yote hayo, bado hakuna hoja nzito dhidi ya Bolt, ambaye amekuwa akifanya mazoezi makali na kuibuka mshindi kwenye mashindano. Hata hivyo, ikija kutokea Bolt akagundulika alitumia dawa hizo, sioni jinsi mchezo huu utakavyoweza tena kubaki na heshima; atakuwa ameuporomosha kwa kiasi kikubwa, na sijui wahusika wataficha wapi nyuso zao.