Licha ya mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo kurejea kwenye mazoezi, Ureno wanahofia iwapo nyota huyo atahimili mechi zote za Kombe la Dunia.
Ronaldo anakabiliwa na matatizo ya kujirudia rudia ya tendo za goti lake, ambapo kuna hatari ya kujitonesha tena siku zijazo.
Vinginevyo inawezekana Ronaldo akacheza bila kuonesha machachari yake kwa kuogopa kuumia lakini yote yatategemea hali yake kama imetengamaa vilivyo.
Ureno ambao wapo kwenye kundi moja na Ujerumani, Marekani na Ghana, ambapo Ujerumani na Ureno wanapewa nafasi kubwa ya kuvuka.
Marekani wanaofundishwa na Jurgen Klinsman, kwa upande mwingine, wanachekelea kuumia kwa Ronaldo wakijua kwamba ni kikwazo kikubwa kwao, kama alivyokuwa kwa Sweden wakati wa kufuzu kwa fainali hizi.
Washabiki wengi wangependa kumwona Ronaldo akicheza kwenye mechi zote ili kufurahia umahiri wa aina yake, sambamba na akina Lionel Messi wa Argentina na Neymar wa Brazil.
Ronaldo amekuwa akisumbuliwa na goti lake la kushoto na mara kadhaa ameshindwa kuhudhuria mazoezi, ambapo alikuwa ameambiwa akicheza asitumie mguu huo kukaba wala kupiga mpira.
Hata hivyo, Ronaldo mwenyewe anatarajia kwamba atakuwa fiti kwa michezo hiyo na ataweza kutumia miguu yote na kuibeba nchi yake.
Maofisa afya wa timu hiyo ya taifa wanafuatilia kwa karibu na kwa hadhari kubwa kuhakikisha kwamba hawamkosi lakini pia haumii dimbani.
Ronaldo anatarajiwa kuongoza kikosi chake katika Kundi G kwa kucheza na Marekani Juni 22, ambapo Marekani wanataka kuona Ronaldo anakosa mechi hiyo ili watumie udhaifu wa timu kuwafunga na kujiweka pazuri kusonga mbele.