Ureno wamefuta ndoto kubwa za wenyeji Ufaransa kutuzwa kwenye Euro
2016, badala yake wakawalaza 1-0 na kutwaa kombe hilo.
Walifanikiwa kufanya vyema licha ya kumpoteza nahodha na mshambuliaji
wao mahiri, Cristiano Ronaldo aliyeumia mapema.
Alikuwa ni Eder aliyefunga bao pekee la mchezo dakika ya 109 katika
muda wa nyongeza, ambapo aliingia akitokea benchi na kuachia mkwaju
mzuri kiufundi.
Ronaldo anayekipiga Real Madrid alitolewa nje kwa machela huku akilia
katika dakika ya 25, zikiwa ni dakika 18 tangu alipoumia goti baada ya
kukabiliana na Dimtri Payet wa Ufaransa katika dakika ya 25 kwenye
dimba la Stade de France jijini Paris.
Ufaransa waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe kutokana na
walivyofanya vyema kwenye mechi zilizotangulia, walishindwa kutumia
pengo la Ronaldo, lakini nusura wafunge bao na kutwaa ubingwa mwishoni
mwa muda wa kawaida, pale Andre-Pierre Gignac alipogonga mwamba kwa
ndani.
Raphael Guerreiro naye aligonga mtambaa wa panya dakika ya 108 kwa
mpira wa adhabu ndogo na dakika moja tu baadaye Eder akamzidi nguvu
kipa Hugo Lloris. Ronaldo alikuwa akiwapa wenzake mbinu akiwa nje,
kama alivyokuwa kocha Fernando Santos.
Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps alieleza kusikitishwa na matokeo
na walivyocheza, akisema walipoteza fursa nzuri za kutwaa ubingwa huo.
Hili ni kombe la kwanza kubwa kwa Ureno kutwaa barani Ulaya, ambapo
wanafanya idadi ya timu zilizopata kulitwaa kufikia 10, lakini
nyingine zikitwaa zaidi ya mara moja.
Eder anakuwa mchezaji wa sita kufunga kwenye fainali ya Ulaya akitokea
benchi. Wengine ni Oliver Bierhoff, Sylvain Wiltord, David Trezeguet,
Juan Mata na Fernando Torres.
Ureno ni timu ya kwanza ya Ulaya kuingia kwenye muda wa ziada mara
tatu katika mashindano hay ohayo. Iliwachukua hadi dakika ya 80
kulenga shuti golini kwa wapinzani wao Jumapili hii, na ni rekodi ya
kwanza katika fainali kukaa muda mrefu hivyo bila shuti langoni.
Mwaka 2004 Ureno wakiwa wenyeji walifika fainali na kuchapwa bao 1-0
na Ugiriki jijini Lisbon katika Stadium of Light.
Mwaka 2006 Ureno walitolewa kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia,
mwaka 2008 wakatolewa kwenye robo fainali ya Euro na nusu fainali ya
2012. Na Jumapili hii ilielekea wangekosa tena ubingwa, hasa Ronaldo
alipolazimika kutoka nje baada ya kujaribu kuendelea kucheza akiwa na
maumivu.
Mechi hiyo ilichezeshwa na mwamuzi mahiri wa England, Mark
Clattenburg. Ronaldo, huku goti lake likiwa limefungwa vilivyo,
aliweza kunyanyua kombe hilo na kuonesha furaha kubwa pamoja na
wenzake.
Ureno walimaliza wa tatu katika kundi lao, wakiondoshwa kwenye ile ya
pili na Iceland waliowashinda Austria. Ni huko England walilazimika
kufunga virago.
Kipa wa Ureno, Rui Patricio na mabeki wake, Pepe na Jose Fonte
walionekana kufanya kazi nzuri, wakiwachanganya vilivyo wachezaji wa
Ufaransa.